Dar es Salaam, Mei, 20. 2022. Imekuwa ni ada sasa kwa duru zetu za habari kutawaliwa na matukio ya ubakaji hasa kwa watoto.
Katika kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu, matukio makubwa yaliyotikisa vyombo vya habari ni pamoja na lile la mkoani Katavi, ambapo mwalimu wa Mafundisho ya dini ya Kikristo Joseph John, kukamatwa kwa kulawiti watoto wanne.
Tukio jingine ni lile la mkazi wa Iringa, kudaiwa kumlawiti mtoto wake wa kambo na shemeji yake. Kadhalika, liliripotiwa tukio lililobeba vichwa vingi vya habari la mtoto wa miaka 14 mkazi wa Iringa, kuwalawiti watoto wenzake 14 wote wa kiume.
Kadhalika hili la juzi, Mei 18 ambapo mwalimu wa Madrasa Jumanne Ikungi, mkazi wa Arusha kwa tuhuma za kuwalawiti wanafunzi takribani 22 wa shule ya msingi Mkonoo, jijini Arusha. Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda alithibitisha baada ya kufika katika shule hiyo na kuzungumza na wazazi, walimu na wanafunzi ikiwa ni baada ya kukamilisha alichokiita uchunguzi wake juu ya mwalimu huyo wa madrasa.
Kwa matukio hayo yaliyoripotiwa kati ya Januari na Mei, inatosha kusema kuwa watoto wetu hawapo salama na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) tunalazimika kusema, ‘watoto hawa hawana pa kukimbilia’.
“Mwenendo huu wa matukio ya ubakaji na ulawiti wa watoto tena na walimu, viongozi wa dini na wazazi au walezi, unadhihirisha kuwa tatizo hili bado ni kubwa nchini na linahitaji maamuzi magumu kutoka kwa watunga sera wetu,” Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk Rose Reuben.
TAMWA pamoja na wadau wengine wa masuala ya jinsia, tumekuwa tukiimba wa kuitaka jamii kuzuia ukatili kwa miaka zaidi ya 30 sasa tukililia mabadiliko ya sera, sheria na hata kutoa elimu kwa jamii. Lakini bado tatizo hili linaendelea, tena sasa likitekelezwa na viongozi waliotegemewa kuwalinda watoto wetu, tuliodhani kuwa ni walimu wa kukuza maadili mema kwa watoto.
“Tunahitaji zaidi ya sheria kukomesha ukatili huu, tunahitaji maamuzi magumu kutoka ngazi zote kuanzia familia, wanajamii, viongozi wa dini zote na serikali kwa ujumla wake kwa sababu watoto walio taifa la kesho, wanaharibiwa kimwili na kisaikolojia” Dk Rose Reuben.
Wakati huo huo, taarifa za makosa ya ukatili wa jinsia na unyanyasaji zilizotolewa na Jeshi la Polisi katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2021 zinaonyesha mikoa ya kipolisi iliyoongoza kwa ukatili dhidi ya watoto ni Arusha 808, Tanga 691, Shinyanga 505, Mwanza 500 na Ilala 489.
Kadhalika makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ya matukio ni ya ubakaji 5,899, kumpa mimba mwanafunzi 1677, ulawiti 1,114, kumzorotesha mwanafunzi masomo 790 na shambulio 350.
Wakati tukiendelea kutafuta suluhisho la janga hili, TAMWA inaendelea kutoa elimu katika shule za sekondari na msingi, kuhusu mada za ukatili wa kijinsia, lakini bado hakuna mitaala shuleni inayogusa masuala ya afya ya uzazi moja kwa moja.
“Utafiti uliotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Haki Elimu, unaonyesha kuwa watoto wengi hawafundishwi elimu ya afya ya uzazi, lakini zaidi hasa walimu nao wanaogopa kufundisha wanafunzi mada hizo, hapa ndipo mzizi wa tatizo ulipo,”
“Ni dhahiri kuwa mambo yanayouhusu afya ya uzazi na ukatili wa kingono hayazungumzwi ndani ya familia wala shuleni tena wengine wanaona ni mambo ya aibu yasiyostahili kujadiliwa, hivyo yanabaki kuwa masuala ya wadau na serikali ambao nao husuluhisha tatizo na sio mzizi wa tatizo,” Dk Rose Reuben.
Wakati tukijiandaa na zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, ifikapo Agosti 23, ni wakati muhimu kwa viongozi, wazazi, walezi, wasimamizi wa sheria, wadau wa masuala ya jinsia na watoto kujitathmini wapi penye mapengo, ili tuzibe ombwe hili la ubakaji wa watoto.
TAMWA imesikitishwa na ubakaji huu wa watoto unaoendelea hapa nchini na tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kutamka kuwa hili ni janga na kutoa maamuzi magumu kunusuru watoto wetu.
Dk Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA