Press Release

Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Familia

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Dar es Salaam, 15 May, 2022 Wakati dunia  ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA)kinawakumbusha watanzania kutathimini hali ya maendeleo ya familia, na kuwahimiza wazazi na walezi kutoa huduma muhimu za matunzo na kuzuia vitendo vya ukatili kwa watoto ambavyo vimekithiri hapa nchini.
Kama kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inavyosema: Dumisha amani na upendo kwa familia imara, jitokeze kuhesabiwa TAMWA tunawakumbusha wanafamilia kuepuka migogoro inayopelekea kusambaratika na kuacha watoto wakikosa huduma muhimu ikiwamo upendo wa wazazi au walezi.  
“Hivi karibuni kumeripotiwa matukio kadhaa ya ukatili wa watoto ikiwemo vipigo, mauaji, udhalilishaji wa kingono na hata watoto waliojiingiza katika vitendo vya uhalifu maarufu kama Panya Road, ambayo yanaonyesha wazi kuwa ipo hitilafu kubwa iliyoikumba taasisi ya familia Dr. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji-TAMWA
 Kadhalika  kauli mbiu hii ya kitaifa ya Siku ya Kimataifa ya Familia inazikumbusha familia umuhimu wa kushiriki sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu, zoezi ambalo litaiwezesha serikali kubaini takwimu sahihi za watu na kaya ili kupanga mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya familia. 
‘Sensa ni zoezi muhimu la kitaifa kwani ni ukweli usiopingika kuwa maslahi ya watoto na sapoti ya familia kama taasisi vinakamilishwa kwa kubainishwa kwa takwimu sahihi za watu, mipango ya kifedha, na rasilimali nyingine zinazomilikiwa na familia, baada ya zoezi hili TAMWA tunaiomba serikali kutengeza Sera ya familia iyakayoainisha wajibu, maslahi ya kiuchumi na mipango kwa familia kama taasisi Dr. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji- TAMWA
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloangalia maslahi ya watoto (UNICEF) zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya ukatili wa watoto unafanyika majumbani na asilimia 40 unafanyika mashuleni, hivyo kuna umuhimu wa watanzania wote kuthamini na kuimarisha taasisi ya familia kwa upendo na amani.
Pia kwa mujibu wa taarifa za makosa ya ukatili wa jinsia na unyanyasaji zilizotolewa na Jeshi la Polisi katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka 2021 zinaonyesha mikoa ya kipolisi iliyoongoza kwa ukatili dhidi ya watoto ni Arusha 808, Tanga 691, Shinyanga 505, Mwanza 500 na Ilala 489.  
Kadhalika makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ya matukio ni ya ubakaji 5,899, kumpa mimba mwanafunzi 1677, ulawiti 1,114, kumzorotesha mwanafunzi masomo 790 na shambulio 350. 
Familia ni chanzo cha rasilimali watu, na ndio maana Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1993 lilitoa tamko namba 47/237 na  kuitangaza Mei 15 kuwa siku maalumu ya kutathimi hali ya familia, upatikanaji wa huduma muhimu na maendeleo yao.  
TAMWA tunaendelea kusisitiza watanzania, kuthamini ngazi ya familia, kama eneo la kwanza la kuonyesha upendo, kuanzisha maendeleo na kurithisha vizazi vyetu elimu, mali na hekima. 
Ngazi ya familia ndiko kunakoanzia maendeleo, afya na kunakojenga taswira ya tabia ya mtu mmoja mmoja, familia ni muhimu, Dr Rose Reuben. 
Mkurugenzi Mtendaji 
Rose Reuben
TAMWA

Search