News/Stories

TAMWA YAWAPONGEZA WANAWAKE WALIOJITOKEZA KUWANIA URAIS NA UBUNGE UCHAGUZI WA OKTOBA 29

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Dar es Salaam, Septemba 9, 2025Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinawapongeza wanawake wote waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais.

Mchakato wa uteuzi wa watia nia na uchukuaji fomu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, umefanyika hapa Tanzania, na TAMWA imeona ari kubwa kwa wanawake kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali.

Taasisi ya Ulingo Wanawake, imefanya majumuisho na kupata takwimu zinazoonyesha ongezeko la wanawake waliojitokeza kwenda majimboni.

Takwimu zinaonyesha kuwa,  wanawake 231 walijitokeza kuchukua form za ubunge kupitia chama cha CCM na kati yao walioshinda na kupitishwa na chama ni wanawake 25. Kati ya hao 25, wanane ni wapya. 

Pamoja na ubunge kadhalika, mwaka huu umeona mwamko wa vyama vya siasa kuwateua wanawake kama wagombea wenza,Eveline Wilbard Munis- NCCR, Husna Mohamed Abdallah-CUF, Aziza Haji Selemani-MAKINI, Amani Selemani Mzee-TLP, Chausiku Khatibu Mohamed-NLD, Sakia Mussa Debwa-SAU

Wengine ni Chuma Juma Abdallah na Devotha Minja- CHAUMA. Huku CCM ikiteua mgombea urais mwanamke, ambaye ni Samia Suluhu Hassan. Licha ya baadhi ya watia nia wanawake kuenguliwa na vyama vyao, TAMWA imeona dhamira na ujasiri wao wa kushiriki katika uchaguzi. Kwa wanawake waliopitishwa na vyama vyao kuwania uongozi, tunawapa pongezi kwa kuonyesha moyo wa uthubutu na nia ya kushiriki nafasi za juu za uongozi.

Kwa bahati mbaya, hatukuweza kupata takwimu sahihi za waliojitokeza kuwania ubunge katika vyama vingine. 

Kwa muda mrefu, TAMWA imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi kupitia warsha, makongamano, mijadala ya wazi pamoja na kutumia vyombo vya habari ili kufikisha ujumbe wa kuondoa vikwazo vinavyowanyima wanawake fursa ya kushiriki kikamilifu katika ngazi za maamuzi.

Kwa nafasi ya Urais, TAMWA inawapongeza wanawake wote waliojitokeza na kuteuliwa na vyama vyao kugombea nafasi ya juu kabisa ya uongozi, akiwamo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa upande wa CCM, na Bi Saum Rashid wa UDP. Aidha, tumeona pia idadi kubwa ya wanawake waliojitokeza kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi, jambo linaloashiria mwelekeo chanya wa ushiriki wa wanawake katika siasa.

Kwa TAMWA, hatua hizi ni mafanikio makubwa kwa sababu ajenda yetu kuu ni kuona wanawake wanashika nafasi za juu za uongozi na maamuzi, ili kuleta mabadiliko yenye kuzingatia usawa wa kijinsia.

Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) inaonyesha kuwa, hadi kufikia Februari  2024, wanawake walishikilia asilimia 37.4 ya viti vya Bunge nchini Tanzania, ikiwa ni jumla ya wabunge 148 kati ya 392 ambapo uwakilishi mkubwa unatokana na viti maalum. 

Idadi ya wanawake katika nafasi za uwaziri inatofautiana, ambapo ripoti ya NBS Aprili 2024 na Julai 2024 zinaonyesha kuwa kulikuwa na mawaziri saba na kwamba asilimia 37.5 ya mawaziri ni wanawake, mtawalia. 

Licha ya mafanikio haya makubwa lakini bado tunaamini wapo wanawake wanaozuiwa kushiriki nafasi za uongozi kutokana na mfumo dume, wapo wanawake wanaodhalilishwa mitandaoni kutokana na nafasi zao za uongozi. 

Hivyo basi tunapoendelea kupata mafanikio haya, bado juhudi za dhati zinahitajika kuhakikisha wanawake wanasiasa wanafanya siasa kwa usalama  kama wanaume katika mchakato wa uchaguzi ikiwa ni pamoja kupiga kura, kuchagua na wanaotaka kutia nia kwenye uongozi hawabaguliwi kutokana na jinsia zao. 

Tunaamini kwa dhati kwamba uwepo wa wanawake katika ngazi za juu za uongozi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa kwa sababu wanawake huleta mtazamo wa kipekee katika uongozi, husimamia kwa uwajibikaji zaidi, na mara nyingi hulinda maslahi ya makundi yote ya jamii, hususan watoto, vijana na wanawake wenzao.

“Kukosekana kwa wanawake katika ngazi za juu za uongozi kunadhoofisha utekelezaji wa sheria na sera zinazolenga kulinda haki za wanawake na watoto. Uwepo wao utahakikisha uimarishaji wa sheria za kuzuia ukatili wa kijinsia, ikiwemo ndoa na mimba za utotoni, ukeketaji, ubakaji, ulawiti pamoja na udhalilishaji wa kijinsia unaoenea kupitia mitandao ya kijamii.”

Kwa msingi huo, TAMWA inaendelea kusisitiza kuwa ni wajibu wa jamii nzima, vyama vya siasa, serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi sawa ya kushiriki kwenye siasa na kushika nafasi za uongozi, ili kujenga taifa lenye usawa, amani na maendeleo endelevu.

Kadhalika wakati tayari kampeni zikiwa zimeanza, TAMWA tunahimiza siasa safi, jumuishi, zenye staha zinazolenga kujenga ustawi, utu wa jamii nzima badala ya kampeni zenye matusi, dhalili na kebehi. 

Mkurugenzi Mtendaji

Dkt Rose Reuben

TAMWA

Latest News and Stories

Search