News/Stories

UJUMBE WA HALIMA SHARIFF: SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Wakati dunia ikisherehekea Siku ya Wanawake Duniani, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA)kinakuletea wanahabari wakongwe waanzilishi wa TAMWA. Hiki ndicho wanachokisema katika maadhimisho haya ya Siku ya Wanawake Duniani.

Halima Shariff, yeye ni mtafiti, kiongozi na mwalimu . Ni miongoni mwa waasisi wa TAMWA aliyezaliwa kutoka katika familia ya kawaida kabisa, mkoani Tanga.
 
Akiwa ni mtaalamu na nguli wa habari nchini, Halima amewahi kuandika katika gazeti la Daily News miaka ya 80 na mtangazaji wa  Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani(Deustche Welle).
 
Pamoja na fani ya habari, Halima amewahi  kushika nafasi kubwa katika taasisi za kimataifa  na kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mradi wa Uzazi wa Mpango wa Advanced Family Planning Project(AFP).
 
Ni miongoni mwa wanawake waliosimamia kidete maendeleo ya wanawake na watoto katika masuala ya elimu, afya ya uzazi na Virusi vya Ukimwi. 
 
Amewahi kuongoza miradi mikubwa ya afya  ikiwamo ya Shirika la Misaada la watu wa Marekani USAID. Ameshiriki katika kutetea hadi  kufanikisha kupitishwa kwa muswada wa  masuala ya Ukimwi, kuanzishwa kwa sera ya HIV/AIDS katika maeneo ya kazi. Amewahi pia kuwa Kamishna wa Tume ya Ukimwi Tanzania (TACAIDS). 
 
Anachokisema katika kuadhimisha Sharif katika kuadhimisha Siku ya Wanawake duniani: 
 
“Kuimarisha nafasi ya mwanamke katika nyanja zote katika jamii ni harakati endelevu zinazohitaji jitihada za pamoja zenye kasi inayoongezeka kizazi hadi kizazi. Kwa mantiki hiyo Tanzania tumefanikiwa kujenga uelewe wa jamii kuhusu nafasi muhimu ya mwanamke katika kujenga familia na katika maendeleo kwa ujumla” 
 
“Lakini bado hatujawekeza vya kutosha katika kuhakikisha afya ya mwanamke inapewa kipaumbele ukizingatia kwamba bado wastani wa kuzaa wa taifa ni watoto sita kwa mwanamke wa rika la uzazi (15-49). 
 
“Inatia moyo kwamba serikali imekuwa ikielekeza nguvu huko lakini ni eneo linalohitaji kutazamwa zaidi kwani mara nyingi wanawake hukosa fursa za kujiendeleza kutokana na changamoto za uzazi,”

Latest News and Stories

Search