Press Release

UONGOZI WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN UWE CHACHU KWA JAMII KUWEKEZA KIELIMU KWA MTOTO WA KIKE

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Oktoba 11, 2023. Dar Es Salaam.Kila ifikapo Oktoba 11, dunia huadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani. Siku hii inatukumbusha kutambua changamoto zinazowakumba watoto wa kike.

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) inatambua kwamba watoto wa kike hapa nchini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali. Hivyo tunapoadhimisha siku hii, hatuna budi kuziangazia ili kukumbushana kuwa mapambano yanaendelea ili kumfanya mtoto wa kike kupata haki zake katika jamii.

TAMWA katika safari yake ya miaka zaidi ya 35 ya kuhamasisha upatikanaji wa haki za wanawake na watoto wa kike, imekutana na madhila mengi dhidi ya watoto wa kike na miongoni mwa hayo ni ukeketaji, mimba za utotoni, ndoa za utotoni na uminywaji wa haki za kupata elimu kwa watoto wa kike.

Lakini kadri dunia inavyobadilika ndivyo tunavyoona kuwa ili kuyaondoa hayo yote, basi suluhu la kudumu ni kuwekeza katika elimu. Ndiyo maana kauli mbiu ya mwaka huu inasema: “Wekeza katika haki za watoto wa kike: Uongozi wetu, ustawi wetu’

Kauli mbiu hii inajikita katika kuamsha hamasa kwa jamii, asasi za kiraia, serikali na watunga sera kuwekeza katika kuzitambua na kuzitekeleza haki za mtoto wa kike, na pia kutumia nafasi za uongozi kuwastawisha watoto wa kike.

Hivyo basi, TAMWA inaipongeza serikali kwa kuwekeza zaidi katika kujenga mabweni na shule za watoto wa kike, kutoa ufadhili wa masomo na kuwapa watoto wa kike kipaumbele katika nafasi za kielimu. 

Lakini bado kuna mapengo makubwa katika jamii yetu hasa ya kimtazamo kwamba watoto wa kike hawana umuhimu wa kupata elimu. 

“Na hili linakwenda sambamba na mila na tamaduni ambazo zinaamini mtoto wa kike hana haki ya kupata elimu. Hivyo wakati serikali na wadau wengine wakiwekeza katika elimu, wapo wazazi au familia zinazomtupa mtoto wa kike asipate elimu”Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk Rose Reuben

Katika kupata suluhisho la changamoto hizi, TAMWA tumefanya miradi kadhaa inayolenga kumuinua mtoto wa kike kielimu. Kwa mfano, TAMWA imefanya midahalo kadhaa na watoto wa kike, katika shule za Nambilanje na Likunja, mkoa wa Lindi, shule ya sekondari ya Mugabe, Sinza, Dar es Salaam, nia ni kusikiliza sauti zao na kujua wanachotaka. 

“Tunaposikiliza sauti zao, tunajua changamoto wanazopitia na hivyo tunajua wapi pa kuchukua hatua tunapozingatia haja zao, wasichana hawa nao wanaongeza kasi ya kutetea mabadiliko yao katika jamii wanazoishi” Dk Rose Reuben

Kwa mfano, katika mdahalo uliofanywa katika shule ya msingi Likunja, watoto wa kike walibainisha kuwa, wazazi huwaambia waandike makosa katika mitihani yao ya kumaliza darasa la saba, ili wasifaulu. 

Walimu katika shule hiyo walisema, matukio ya wazazi kuwafundisha watoto wa kike waandike ‘makorokocho’ kwenye mitihani yameongezeka baada ya serikali kujenga zaidi shule za sekondari na hivyo wanafunzi wanaofaulu kuongezeka. 

“TAMWA tunaamini katika dunia ambayo watoto wa kike wana nafasi ya kusoma na kuiwajibisha serikali, dunia ambayo watoto wa kike watakuwa viongozi katika ulimwengu wa teknolojia, tafiti na uvumbuzi. Na tunatamani mifano hii isiwe hadithi, bali mifumo yetu ya kawaida” Dk Rose Reuben

TAMWA inasisitiza jamii, hususan wazazi, kuwapa nafasi watoto wa kike na kuendelea kuwekeza katika elimu, kwani sio tu kwamba kundi hili wana uwezo kielimu lakini pia wana uwezo katika uongozi kama tunavyoona sasa Tanzania ina Rais mwanamke, ambaye ni Samia Suluhu Hassan. 

“Nafasi ya Rais Samia Suluhu Hassan kama kiongozi, iwe chachu  na hamasa kwa jamii kuendelea kuwekeza kielimu kwa mtoto wa kike,” Dk Rose Reuben.

Mkurugenzi Mtendaji 

Dk Rose Reuben

TAMWA

Search