Gallery

User Rating: 2 / 5

Star ActiveStar ActiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Novemba 25, 2021, Dar es Salaam. Leo Dunia inanza madhimisho ya  Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia. 
 
Maadhimisho haya  yanayobebwa na kauli mbiu isemayo; Ewe Mwananchi, Pinga ukatili wa kijinsia Sasa yanakuja wakati ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kukithiri kwa matukio ya ukatili wa kijinsia, ikiwamo ubakaji hapa nchini.
 
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinasikitishwa na ongezeko la ukatili huu hasa kwa watoto na wanawake ambao ndio tegemeo katika mustakabali wa kimaendeleo nchini. 
 
Akiwa bungeni, Naibu Waziri wa Afya, Mwanaidi Ali Khamis alinukuliwa akisema, kati ya Januari hadi Septemba mwaka huu, watoto 6168 walifanyiwa ukatili wa kijinsia na kati yao, 3524 walibakwa. Wakati huo Naibu Waziri alisema, wanafunzi 1887 walipata ujauzito katika kipindi hicho hicho. 
 
Takwimu hizi zinaamanisha nini? Zinamaanisha kwamba, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa basi katika kipindi cha mwaka mmoja, zaidi ya watoto 7000 watakuwa wamebakwa au watoto zaidi ya 12,000 watakuwa wamefanyiwa ukatili.
 
Takwimu hizi mpya zinaogofya na kutufanya TAMWA tuone pengine wadau, ikiwamo serikali, wazazi na walezi, tukubaliane na kutamka kuwa; Ubakaji sasa ni janga.
 
TAMWA tunaona ni wakati sahihi sasa, kwa wadau wa masuala ya ukatili wa kijinsia, kukaa pamoja na kupanga mikakati mipya na madhubuti zaidi ya kumaliza au kupunguza matukio haya kwani sheria na sera nzuri zipo lakini ukatili huo bado unaendelea katika jamii yetu. 
 
Hata hivyo tunaipongeza mahakama kwa kutoa hukumu na kufuatilia kwa ukaribu kesi hizi za ubakaji, kwani ipo mifano ya waliohukumiwa kwa kufanya matukio haya. Tunayapongeza madawati ya jinsia kwa kusimamia upelelezi na kutoa ushauri kuhusu matukio au kesi hizi za ubakaji na ukatili mwingine.  Hata hivyo bado matukio haya yanaendelea kuongezeka kila kukicha. Je tatizo lipo wapi? 
 
Ni muhimu kwa taifa, sasa kuendelea kubuni njia mbadala na mpya za kukabiliana na janga hili. Tunaliita janga kwa sababu, watoto 3524 kubakwa si lelemama, bali ni tatizo kubwa katika jamii yetu ambalo linaharibu kabisa mustakabali wa maisha ya kizazi kijacho.
 
Wakati huo huo, bado kinamama wanaendelea kupokea vipigo, kubakwa, kupewa lugha dhalilishi katika jamii yao hali inayowafanya kuwa kundi linaloomboleza na wakati mwingine kuichukia jinsia yao. 
 
"Ukatili huu, una madhara ya muda mfupi, muda mrefu, kiuchumi, kimwili na kisaikolojia kwa wanawake na wasichana na watoto wote kwa ujumla, kwani inawazuia kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika jamii yao," Dk Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji, TAMWA. 
 
"Hakuna namna nyepesi ya kuelezea madhara haya ya ukatili wa kijinsia, tumewahi kuona, pengine tumesikia lakini bado jamii nzima haijajua madhara yake kwa kina labda kwa sababu, matukio haya hayatokei kwa wingi mara moja. Lakini tungewapata waathirika hawa na kuwakusanya pamoja, basi Tanzania ingelia," Dkt Reuben.
 
"Ubakaji huu wa watoto ni janga. Serikali itambue kuwa hili ni janga kwa sababu madhara yake yanaweza yasionekana kwa sasa lakini yataonekana baadaye wakati ambapo kizazi hiki cha sasa kitakapokuwa kimeshika usukani" Dkt Reuben.
 
TAMWA inaamini kuwa taifa salama ni lile linalojenga kizazi salama, ambacho waliopo wanawalinda watoto na kumlinda mwanamke. Hivyo basi, ili kuwa na jamii hiyo hatuna budi kuchagizana kwani; waswahili walisema; Kichango ni kuchagizana Kila mmoja ashiriki kwa namna yake kumaliza ukatili huu.
 
Kidunia hali ni kama hii, takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wanawake(UN-Women)zinaonyesha kuwa ukatili wa wanawake aghalabu hufanywa na mwenza, mume wa zamani au wa sasa. Inaelezwa kuwa wanawake zaidi ya milioni 640 wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea waliwahi kufanyiwa ukatili na wenza.
 
Ukatili huu unatajwa kusababisha msongo wa mawazo, kihoro, mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa ikiwamo UKIMWI na wakati mwingine waathirika kujiua. 
 
Takwimu hizo kadhalika zinaeleza kuwa, zaidi ya wanawake 87,000 duniani waliuawa na nusu yao, (50,000) waliuawa na mwenza au mwanafamilia. Zaidi ya thuluthi, waliuawa kwa makusudi na mwenza/mume wa sasa au wa zamani. 
 
TAMWA imeona zaidi kuwa unyanyasaji huu kwa hapa Tanzania umeendelea kujikita pia katika mashindano ya ulimbwende, vyuo vikuu, vyombo vya habari ikiwemo  mitandaonii pamoja na mahala pa kazi. Haya yote yasipofanyiwa kazi, basi tutakuwa na dunia isiyo salama kwa kundi hili.
 
"Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha wazi kuwa anasimamia vyema haki za wanawake na watoto, tumemuona na kumsikia akipinga lugha dhalilishi kwa wanawake na udunishwaji wa kundi hilo katika nafasi za siasa na uongozi. Kongole Rais wetu,"Dkt Rose Reuben
 
TAMWA hatutaacha kusimamia haki za wanawake, watoto na wanahabari, tutaendelea kupaza sauti hadi tutakapoona amani imetawala tukiendelea kusema "Ewe Mwananchi, Pinga ukatili wa kijinsia Sasa”.
 
Kazi iendelee. 
 
Dk. Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji - TAMWA
 

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania kwa kushirikiana na Mtandao wa wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani Tanzania na kuratibiwana Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) kwa pamoja tunaungana na watanzania wote na Dunia kwa ujumla kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka Wahanga wa ajali za Barabarani.

Siku hii huadhimishwa kimataifa, kila ifikapo Jumapili ya wiki ya tatu (3) ya mwezi Novemba kila mwaka Kwa ajili ya kuwakumbuka waathirika wa ajali za barabarani na kuwaenzi mamilioni ya watu waliopoteza maisha na wengine wengi walioathirika kwa njia moja au nyingine kutoka na ajali hizo.

Kauli mbiu ya kimataifa kwa mwaka huu inasema; ‘Kumbuka, Saidia,Chukua Hatua’.

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
Ndugu mgeni rasmi,
Wawakilishi wa FES,
Mkuu wa Dawati la Jinsia,
Mwakilishi wa Takukuru,
Wanahabari,
Nawasalimu kwa jina la JMT!
 
Dar Es Salaam, 2nd December, 2021. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Friedrich-Ebert-Stiftung (FES) Tanzania, wanaungana na watanzania wote kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
 
Maadhimisho haya, hufanyika kila ifikapo Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka.  Kwa mwaka huu, maadhimisho haya yamepambwa na kauli mbiu isemayo: Pinga ukatili wa kijinsia Sasa 
 
Hata hivyo wakati maadhimisho haya yakiendelea, TAMWA pamoja na FES tumebaini kuwa tatizo la rushwa ya ngono mahala pa kazi linaendelea kushika mizizi katika jamii yetu. 
 
Hilo lilibainika hata wakati TAMWA ilipofanya mradi na Asasi ya Habari ya Internews mnamo mwaka 2019 na kuwashirikisha wanahabari kufanya habari za uchunguzi kuhusu rushwa ya ngono mahala pa kazi.
Makala za wanahabari hao, zilibainisha wazi, rushwa hiyo ipo lakini imegubikwa na ukimya hasa kutoka kwa waathirika. 
Kadhalika, mwaka 2021, TAMWA kwa kushirikiana na Women Fund Tanzania, (WFT) ilitekeleza mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari. TAMWA ilifanya utafiti na kubaini wanahabari wanakabiliwa kwa kiasi kikubwa na rushwa ya ngono na ukatili mwingine ndani ya vyumba vyao vya habari.
Utafiti  uliofanywa na asasi ya EBA nchini Tanzania mwaka 2020 ulibaini kuwa, suala la rushwa ya ngono linafahamika na limetanuka kuanzia katika sekta ya elimu na katika sekta ya ajira. 
 
Tatizo la rushwa ya ngono ni kubwa lakini limegubikwa na ukimya, wahanga wengi hawatoi taarifa wakiogopa kudhalilishwa zaidi, Dr Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA.
 
TAMWA tunasema, rushwa ya ngono vyuoni ndicho chanzo cha kuwa na wanafunzi wasio na tija katika sekta ya ajira, lakini pia ndicho chanzo cha kuzalisha wanaataluma wasio na sifa za kuajiriwa. 
 
Rushwa hii ya ngono mahala pa kazi na vyuoni, ndicho chanzo pia cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa, Dr Rose Reuben. 
Katika tafiti zetu, TAMWA tumegundua kuwa rushwa ya ngono hufanyika sio tu mahala pa kazi, bali wakati mwingine, hata katika kambi za wakimbizi, katika shule za sekondari.
Rushwa ya ngono hurudisha nyuma maendeleo ya mtu mmoja mmoja na nchi kwa sababu matokeo ya ukatili wa aina hii ni kurudisha nyuma ari ya utendaji kazi wa wanafunzi, wafanyakazi au waumini, Dr Rose Reuben
 TAMWA tumeona pia zipo changamoto katika kukabiliana na aina hii ya ukatili, kwanza ni ukimya. Wahanga wengi kushindwa au kuhofia kutoa ushahidi na kuzungumzia suala hili. Lakini pili, ukosefu wa takwimu zitakazowezesha wadau kufanyia kazi aina hii ya ukatili.
Ipo sheria ya makosa ya rushwa, inayogusa rushwa ya ngono, nayo ni sheria namba 11 ya mwaka 2007, kifungu cha 25. Dr Rose Reuben
 
Ukatili kwa njia ya mtandao
Wakati huo huo, tunakemea vikali ukatili kwa njia ya mtandao unaoendelea. Tumeona, tumesikia na wakati mwingine sisi ndiyo tumekuwa waanzilishi wa ukatili huu. Kutumia picha za wanawake vibaya, kutumia lugha dhalili kwa kundi Fulani mitandaoni, kutumia picha za watoto na kuweka maudhui yanayomdhalilisha. Haya ni baadhi tu ya matendo yanayochagiza ukatili wa kijinsia mitandaoni.
 
TAMWA ni wanahabari na wanahabari ni TAMWA, hivyo tunawaomba wadau wetu wa habari, mkatumie kalamu zenu kukemea rushwa ya ngono  ndani ya vyumba vyenu vya habari  na kuvaa joho la kupinga aina zote za ukatili wa kijinsia ikiwamo ule wa kwa  njia ya mtandao. 
 
Kadhalika, tunaipongeza serikali kwa kupitia wadau wake wakiwamo Takukuru, wamefanyia kazi suala la rushwa ya ngono kwa kufanya tafiti kadhaa lakini pia kwa kufanyia kazi makosa ya aina hii. Hongereni! lakini tunatamani  matokeo zaidi, kesi zaidi zipelekwe mahakamani, hukumu itolewe  ili kufanya mahala pa kazi pawe sehemu salama na penye tija. 
Pia tunampongeza  Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kuzindua mwongozo wa madawati ya rushwa ya ngono vyuoni. Tunaomba yakatumike kwa tija. 
Ewe Mwananchi, pinga ukatili wa kijinsia sasa,
 
#KaziIendelee
#ZuiaUkatiliMtandaoni
#ZuiaUkatili
 
Dr Rose Reuben
 
 
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar es Salaam, Machi 29, 2021. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mwanahabari wa IPP Media, Blandina Sembu.
 
Taarifa ya Jeshi la Polisi inasema kuwa, mwili wa Sembu, aliyekuwa mtangazaji wa kipindi cha Wanawake, kinachorushwa na ITV, uliokotwa katika maeneo ya Bamaga usiku wa kuamkia Machi 28, hali ambayo inaonyesha utata wa mazingira ya kifo chake. 
 
TAMWA kimesikitishwa na tukio hilo lililompoteza mwanaharakati wa masuala ya wanawake, masuala ya watu wenye ulemavu na mwanahabari aliyeipenda kazi yake. 
 
"TAMWA ikiwa ni mdau mkuu wa wanahabari wanawake nchini , kimeguswa na tukio hilo na tunaziomba mamlaka husika kuchukua hatua za uchunguzi ili kujua undani wa kifo cha Sembu ikiwa kimesababishwa na watu basi hatua kali zichukuliwe kwa watekelezaji wa tukio hilo" Rose Reuben, Mkurugenzi wa TAMWA
 
TAMWA  itamkumbuka Sembu kwa mchango wake mkubwa katika masuala ya Ushiriki wa Wanawake katika Siasa na Uongozi kwani alikuwa ni mjumbe wa kamati ya  Muungano wa Ushiriki Tanzania iliyoangazia Ushiriki wa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana katika siasa na uongozi. 
 
 Kuondoka kwa Sembu ni pengo kubwa kwa tasnia ya habari, jumuiya za watu wenye ulemavu na pia katika jumuiya zinazotetea haki za wanawake nchini kwani alijitoa kwa dhati na alihakikisha anasemea haki za makundi hayo, pale inapobidi.
 
TAMWA inatoa salamu za pole kwa wanafamilia wote wa Blandina Sembu, Watendaji na Wanahabari wa IPP Media, wanaharakati wa masuala ya jinsia, watu wenye ulemavu na wanahabari  wote  nchini.
 
Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji- TAMWA.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Abeda Rashid Abdallah.....
Ndugu wadau wa masuala ya jinsia.
Viongozi wa serikali,
Wanahabari, 
Itifaki imezingatiwa!
 
Zanzibar, February 4, 2021. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kina furaha kubwa kupata fursa hii adhimu,  leo Februari 4th, 2021, ya kukutana tena na wadau wake muhimu walioshiriki katika utekelezaji wa mradi wa Wanawake Sasa’ uliofadhiliwa na taasisi ya kimataifa ya African Women, Development Fund (AWDF).
 
Mradi wa ‘Wanawake Sasa’ umehitimishwa kwa mafanikio makubwa na kamwe mafanikio hayo yasingepatikana bila nyinyi wadau muhimu ambao mlishiriki katika kuhimiza Amani, ushirikiano  katika chaguzi na ushiriki wa wanawake katika siasa, uongozi na maamuzi.
 
Kutokana na ushirikiano wenu, tumeona namna ambavyo Rais, John Maguuli ameendelea kuteua viongozi wanawake, na hilo limethibitishwa katika kauli yake aliyoitoa Novemba, 2020 mara baada ya uchaguzi kuwa; ataendelea kuwaamini wanawake. 
Kwa msingi huo napenda nitumie fursa hii kuahidi kuwa, serikali ninayoiongoza itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za uongozi, alisema Rais JPM.
 
Ndugu Mgeni Rasmi,
Si hayo tu, tumeona kivitendo, ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi na tumeshuhudia idadi ya wanawake zaidi ya 230 katika bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwamo mawaziri wanawake.
Kwa upande wa Zanzibar, tuliona uthubutu wa kinamama wawili, waliojitokeza na kuchukua fomu za kuwania urais. 
 
Ndugu mgeni rasmi,
TAMWA inaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na ile ya bara kwa kushiriki katika matukio ya utekelezaji wa mradi huu katika maeneo manne, ikiwamo Zanzibar, Arusha, Dar es Salaam na Dodoma. 
 
Viongozi wa Serikali wameshiriki kwa kiasi kikubwa katika kufungua, kutoa nasaha na kutoa ushauri kwa TAMWA katika ajenda hii ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, Amani na mshikamano. Tunawashukuru!
 
Ndugu Mgeni Rasmi
Kupitia midahalo ya wanawake wanasiasa iliyofanywa katika maeneo yetu manne ya mradi, wanawake wanasiasa zaidi ya 150 kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini,  walipata fursa ya kujifunza umuhimu wa kutumia vyombo vya habari kueneza ajenda zao za kisiasa.
 
Pia kupitia midahalo hiyo, waliweza kujifuza changamoto za kila mmoja hasa katika mrengo wa ukatili wa kijinsia, ikiwamo rushwa ya ngono na kujua namna ya kukabiliana na changamoto za aina hiyo.
Wanawake wanasiasa waliopata mafunzo waliteuliwa kuanzia ngazi ya kanda hadi kitaifa. 
 
Ndugu Mgeni Rasmi,
TAMWA iliwaleta pamoja viongozi wa dini 50 kutoka maeneo hayo manne ambao walishiriki kikamilifu kueneza Amani wakati wa uchaguzi na kusisitiza ushiriki wa wanawake katika siasa, uongozi na maamuzi. Haya kwetu ni mafanikio kwani, nafasi ya viongozi wa dini katika kuhubiri Amani na kuwaleta watu pamoja, vilisaidia katika kufanyika kwa uchaguzi wa Amani, huru na wa haki. 
 
Ndugu mgeni rasmi, 
Kama ujuavyo TAMWA inatumia silaha yake kuu, ambayo ni vyombo vya habari katika kufikisha ajenda kwa jamii, na hivyo iliwapa mafunzo wanahabari zaidi ya 70 kutoka katika maeneo hayo manne. Wanahabari hao walifundishwa na kupata ujuzi kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.
 
Wanahabari hao baada ya mafunzo walifanikisha kuchapishwa kwa Makala za magazeti 40, vipindi vya redio  na televisheni, talk show na kuongeza wigo wa  idadi ya wanahabari tuliofanya nao kazi awali na kuwafikia wa wanahabri zaidi kutoka Zanzibar, Arusha hadi  Dodoma ambao waliandaa Makala za kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi. 
 
Ndugu mgeni rasmi, 
TAMWA na wanahabari kupitia kazi zao, walishirikiana na kuwafikia wanawake ambao awali waliogopa kushiriki katika siasa na uongozi. Hii iliongeza idadi ya wanawake waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi kuanzia ngazi za chini hadi nafasi za ubunge. 
 
Taarifa fupi ya mradi Wanawake Sasa
Wanawake Sasa ni mradi uliotekelezwa kwa ushirikiano wa asasi tatu, TAMWA, WiLDAF na GPF Tanzania, chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake wa Afrika (AWDF).
Mradi huu ulikuwa na malengo makuu matatu, kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi, kwa kuwahamasisha na kuwawezesha wanawake, wanawake wenye ulemavu na vijana kuwa viongozi.
 
Lengo la pili, ni kuwahamasisha na kuwawezesha wanawake katika vyama vya siasa kuwania nafasi za uongozi katika vyama vyao. 
Lengo la tatu ni, kukuza wanawake kisiasa, kuhamasisha Amani katika chaguzi kupitia vyombo vya habari kwa kuishirikisha jamii. Mradi huu wa mwaka mmoja, ulianza kutekelezwa Januari Novemba 2020 na utekelezaji wake ulivihusisha vyama vitano vya siasa (CCM,ACT WAZALENDO,CUF,CHADEMA NA NCCR-MAGEUZI) katika kanda nne Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar.
 
Mkurugenzi Mtendaji,
 
Rose Reuben.
 
TAMWA.

User Rating: 3 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar InactiveStar Inactive
Dar Es Salaam, Julai 20, 2021.
Leo Julai 20, gazeti la Jamhuri, linalotolewa kila wiki, katika ukurasa wake wa kwanza na kuendelea ukurasa wa tatu limeandika habari yenye kichwa  kinachosema: Mambo ya Nje haijamchukulia hatua Balozi".
Katika habari hiyo, inayomtuhumu Balozi wa Libya nchini Tanzania, Bwana Kamal Ramadan Krista kuhusika katika usafirishaji haramu wa wasichana na unyanyasaji wa kingono, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Dk Rose Reuben amenukuliwa akisema kuwa: Sina maoni yoyote kwa sababu habari hii haikufanyiwa uchunguzi wa kutosha
Taarifa hiyo ikaeleza zaidi kuwa Dk Rose“Alipoelezwa kuwa suala hilo ni la kukiukwa kwa haki za watoto wa kike na kusafirishwa nje ya nchi kinyume na sheria huku TAMWA ikijipambanua kuwa watetezi wa haki za wanawake, alishauri watafutwe Polisi wa Kimataifa(Interpol) na Idara ya Uhamiaji. 
Aya ya mwisho ya habari hiyo imesema: Mkurugenzi huyo ameonyesha kutofurahishwa na gazeti la Jamhuri kuandika tuhuma dhidi ya mwanadiplomasia huyo.
Mkurugenzi wa TAMWA anakiri kupigiwa simu na kutembelewa na mwandishi wa Habari wa gazeti hilo Bwana Alex Kizenga tarehe 16 Julai mwaka huu majira ya mchana ambako alihitaji maoni dhidi ya Habari iliyochapishwa katika gazeti hilo wiki tatu nyuma iliyomtuhumu Balozi Krista kusafirisha wasichana wa kitanzania kwenda kufanya biashara ya ngono nchini mwake.   
Mbali na kukataa kutoa maoni kuhusu Habari hiyo kwa msimamo kuwa haikuwa na taarifa kutoka vyanzo vya msingi ama vilelezo. Mkurugenzi wa TAMWA hakukubali kutoa maoni wala kuzungumza maneno kama ilivyonukuliwa na gazeti hilo na  badala yake mhariri na mwandishi  wa Jamhuri Media ambao walidhamiria kumuandika katika taarifa hiyo wamemlisha maneno Mkurugenzi wa TAMWA Dk Rose Reuben.
Ifahamike kuwa chama hiki ni cha kihabari na hivyo kinafahamu misingi yote ya taaluma ya habari na mawasiliano na hivyo tunasikitishwa na mmonyonyoko huu wa maadili uliofanywa  na gazeti la Jamhuri.
Kwa unyenyekevu tunawataka waombe radhi katika gazeti hilo. 
Kadhalika, TAMWA inafanya kazi na wanahabari kila siku na imekuwa ikiruhusu mahojiano na Mkurugenzi Dk Rose Reuben bila kuweka vikwazo, lakini endapo chama hakijatoa ruhusa ya kunukuliwa, basi maombi hayo yaheshimiwe kama maadili ya kihabari yanavyofundisha. 
Kwa kuwa TAMWA ni sehemu ya wanahabari, tunapenda kutoa wito kwa wanahabari wote kufuata misingi na maadili ya habari pindi wanapotimiza majukumu yao. 
Dkt. Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji ~ TAMWA.

Search