- TAMWA
- Hits: 1161
Chama cha wanahabari wanawake Tanzania TAMWA, kinaungana na watanzania wote , wakiwemo watoto wa tanzania, kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika. Hii ni siku muhimu sana kwa sababu wadau, jamii na nchi kwa ujumla wake, tunapaswa kutafakari masuala mbalimbali yanayohusu watoto kupitia siku hii.
Dar Es Salaam , Oktoba 2, 2020.
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) tunachukua fursa hii, kuutambulisha kwenu mradi wa “Rushwa ya ngono miongoni wanahabari wanawake katika vyombo vya habari” unaofadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania - Women Fund Tanzania (WFT).
TAMWA ilianzishwa 1987, na wanahabari wanawake, kwa lengo la utetezi wa ustawi wa haki za wanawake na watoto kupitia taaluma yao na vyombo vya habari.
“Kwa kuwa TAMWA kiini chake ni wanahabari, hivyo basi jukumu la utekelezaji wa mradi huu, unaowalenga wanahabari litakwenda kutekelezwa kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na nyinyi wanahabari na vyombo vya habari,” Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji, TAMWA.
TAMWA tunakwenda kuutekeleza mradi huu tukifahamu kabisa kuwa zipo tafiti mbalimbali zinazoonyesha kuwa bado kuna rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari.
“Wakati huo huo, wanahabari wameonekana kuwa kimya kuhusu matukio hayo, aidha kwa kuogopa kupoteza ajira zao au pengine wakichelea kuaibika zaidi pindi watakapoweka wazi masahibu yao,” Reuben
Kimsingi, rushwa ya ngono haikubaliki na ni tabia isiyopendeza inayoshusha utu na kuwafanya waathirika kudhalilika, kupata msongo wa mawazo na kukosa kujiamini mahala pa kazi, lakini baya zaidi ni kuwa matukio mengi hayaripotiwi.
Baadhi ya watafiti, kama Barton A na Storm, (2014) walibaini kuwa asilimia 48 ya wanahabari wanawake waliohojiwa walikiri kuwa wamewahi kukumbana na rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari kwa namna moja au nyingine na asilimia 83 kati ya hao, walisema hawakuripoti matukio hayo.
“Ombwe hili ni kubwa na huenda likawaathiri hata wanahabari wachanga walio vyuoni, ambao huenda wakakataa tamaa ya kuingia katika tasnia hii na hivyo kuizorotesha tasnia lakini baya zaidi, kukosa wanahabari wanawake katika nafasi za juu za uongozi na wenye mafanikio katika tasnia hiyo,”Reuben
Kadhalika, imebainika kuwa vyombo vyingi vya habari nchini havina sera madhubuti zilizowekwa kuwaongoza wanahabari katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinapowakumba ikiwamo masuala ya rushwa ya ngono katika mazingira ya kazi na hivyo kuchangia kuongezeka kwa visa vya rushwa ya ngono.
“Hivyo basi, kukiwa na ombwe kama hilo, TAMWA katika utekelezaji wa mradi huu, itafanya tathmini kwa kupitia maswali, ili kujua yanayowasibu wanahabari” Reuben
Kadhalika, TAMWA itawajengea uwezo wanahabari, wakiwamo wahariri na wanawake wanahabari walio katika vyombo vya habari.
Kisha, TAMWA itashirikiana na vyombo vya habari kufanya uchechemuzi, kufanya mazungumzo na wamiliki wa vyombo vya habari ili kuwashirikisha matokeo ya tathmini na kuelimisha jamii kuhusu rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya Habari na kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Katika mradi huo TAMWA itashirikisha wadau mbalimbali wa habari wakiwamo, MISA, TEF, MCT, TCRA na OSHA.
Mradi huo utatekelezwa jijini Dar es salaam ambapo ni kitovu cha vyombo vyingi vya habari nchini zikiwamo Redio, Runinga, magazeti na mitandao ya kijamii.
TAMWA inaamini kuwa kwa kufanya tathimini ya rushwa ya ngono katika vyombo vya habari na kuwajengea kuwajengea uwezo wanahabari, itawawezesha pia kufichua na kuandika vyema habari zinazohusu rushwa hii ambayo kwa mujibu wa mila na desturi za watanzania walio wengi imekuwa ikizungumzwa kwa kwa kificho au kutokuzungumzwa kabisa.
TAMWA inatambua kuwa uwepowa Sheria ya Rushwa ya ngono ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)
Lakini zaidi hasa, tunataka wanahabari wapaze sauti zao, tuvunje ukimya, wayazungumze yanayowasibu, na kuondoa kabisa ukatili wa kijinsia wa aina hii ambao unachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya tasnia ya habari ikiwa ni pamoja na kuua vipaji.
Pasipo kuvunja ukimya uliotanda dhidi ya suala la rushwa ya ngono, waathirika kujengewa uwezo wa kukusanya vidhibiti visivyokuwa na mashaka yoyote taasisi yenye mamlaka ya kushughulikia makosa haya haziwezi kufanya kazi yake kwa ufasaha na kuleta mabadiliko katika jamii yetu.
Kadhalika serikali, taasisi za habari na za jinsia, zinatakiwa kushirikiana kumaliza tatizo hili ambalo halijazungumzwa kwa kina ili tuvunje ukimya huu.
Mkurugenzi Mtendaji
Rose Reuben
TAMWA
Dar es Salaam, Mei, 20. 2022. Imekuwa ni ada sasa kwa duru zetu za habari kutawaliwa na matukio ya ubakaji hasa kwa watoto.
Katika kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu, matukio makubwa yaliyotikisa vyombo vya habari ni pamoja na lile la mkoani Katavi, ambapo mwalimu wa Mafundisho ya dini ya Kikristo Joseph John, kukamatwa kwa kulawiti watoto wanne.
Tukio jingine ni lile la mkazi wa Iringa, kudaiwa kumlawiti mtoto wake wa kambo na shemeji yake. Kadhalika, liliripotiwa tukio lililobeba vichwa vingi vya habari la mtoto wa miaka 14 mkazi wa Iringa, kuwalawiti watoto wenzake 14 wote wa kiume.
Kadhalika hili la juzi, Mei 18 ambapo mwalimu wa Madrasa Jumanne Ikungi, mkazi wa Arusha kwa tuhuma za kuwalawiti wanafunzi takribani 22 wa shule ya msingi Mkonoo, jijini Arusha. Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda alithibitisha baada ya kufika katika shule hiyo na kuzungumza na wazazi, walimu na wanafunzi ikiwa ni baada ya kukamilisha alichokiita uchunguzi wake juu ya mwalimu huyo wa madrasa.
Kwa matukio hayo yaliyoripotiwa kati ya Januari na Mei, inatosha kusema kuwa watoto wetu hawapo salama na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) tunalazimika kusema, ‘watoto hawa hawana pa kukimbilia’.
“Mwenendo huu wa matukio ya ubakaji na ulawiti wa watoto tena na walimu, viongozi wa dini na wazazi au walezi, unadhihirisha kuwa tatizo hili bado ni kubwa nchini na linahitaji maamuzi magumu kutoka kwa watunga sera wetu,” Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk Rose Reuben.
TAMWA pamoja na wadau wengine wa masuala ya jinsia, tumekuwa tukiimba wa kuitaka jamii kuzuia ukatili kwa miaka zaidi ya 30 sasa tukililia mabadiliko ya sera, sheria na hata kutoa elimu kwa jamii. Lakini bado tatizo hili linaendelea, tena sasa likitekelezwa na viongozi waliotegemewa kuwalinda watoto wetu, tuliodhani kuwa ni walimu wa kukuza maadili mema kwa watoto.
“Tunahitaji zaidi ya sheria kukomesha ukatili huu, tunahitaji maamuzi magumu kutoka ngazi zote kuanzia familia, wanajamii, viongozi wa dini zote na serikali kwa ujumla wake kwa sababu watoto walio taifa la kesho, wanaharibiwa kimwili na kisaikolojia” Dk Rose Reuben.
Wakati huo huo, taarifa za makosa ya ukatili wa jinsia na unyanyasaji zilizotolewa na Jeshi la Polisi katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2021 zinaonyesha mikoa ya kipolisi iliyoongoza kwa ukatili dhidi ya watoto ni Arusha 808, Tanga 691, Shinyanga 505, Mwanza 500 na Ilala 489.
Kadhalika makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ya matukio ni ya ubakaji 5,899, kumpa mimba mwanafunzi 1677, ulawiti 1,114, kumzorotesha mwanafunzi masomo 790 na shambulio 350.
Wakati tukiendelea kutafuta suluhisho la janga hili, TAMWA inaendelea kutoa elimu katika shule za sekondari na msingi, kuhusu mada za ukatili wa kijinsia, lakini bado hakuna mitaala shuleni inayogusa masuala ya afya ya uzazi moja kwa moja.
“Utafiti uliotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Haki Elimu, unaonyesha kuwa watoto wengi hawafundishwi elimu ya afya ya uzazi, lakini zaidi hasa walimu nao wanaogopa kufundisha wanafunzi mada hizo, hapa ndipo mzizi wa tatizo ulipo,”
“Ni dhahiri kuwa mambo yanayouhusu afya ya uzazi na ukatili wa kingono hayazungumzwi ndani ya familia wala shuleni tena wengine wanaona ni mambo ya aibu yasiyostahili kujadiliwa, hivyo yanabaki kuwa masuala ya wadau na serikali ambao nao husuluhisha tatizo na sio mzizi wa tatizo,” Dk Rose Reuben.
Wakati tukijiandaa na zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, ifikapo Agosti 23, ni wakati muhimu kwa viongozi, wazazi, walezi, wasimamizi wa sheria, wadau wa masuala ya jinsia na watoto kujitathmini wapi penye mapengo, ili tuzibe ombwe hili la ubakaji wa watoto.
TAMWA imesikitishwa na ubakaji huu wa watoto unaoendelea hapa nchini na tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kutamka kuwa hili ni janga na kutoa maamuzi magumu kunusuru watoto wetu.
Dk Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA