Press Release

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Zanzibar, Septemba 16th, 2020. Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Waheshimiwa viongozi wa dini, wakiwamo maaskofu, masheikh, wachungaji.
Waheshimiwa viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa serikali, wakuu wa vyombo vya usalama na wanahabari. 
Itifaki imezingatiwa!
“Dini mbalimbali, Amani na Upendo, Amani na upendo, Dini mbalimbali!
Kwanza napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kutukutanisha katika kusanyiko hili na kutupa afya njema. 
 Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinayo furaha kubwa na kinatoa shukrani za dhati kwa viongozi wa dini mbalimbali, viongozi wa serikali, wanahabari, vyombo vya usalama na taasisi nyingine zisizo za kiserikali kwa kukubali kujumuika nasi katika warsha hii muhimu. 
 
Ndugu Mgeni Rasmi,
Bila shaka wengi wetu tunafahamu fika kuwa Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba 28 mwaka huu. 
Kutokana na tukio hilo kubwa la kihistoria, TAMWA imeona ni vyema kuhimiza na kukumbusha suala la nafasi ya mwanamke katika uchaguzi na kuishirikisha kamati ya Amani ya Viongozi wa dini nchini ambayo inaundwa na viongozi wa dini mbalimbali. 
Uwepo wako mahali hapa, ndugu mgeni rasmi, viongozi hawa wa dini na wadau wengine wa masuala ya Amani, umeonyesha dhahiri kuwa jambo hili ni zito na linaonyesha  mmeipa uzito ajenda hii na mnathamini nafasi ya mwanamke katika uchaguzi mkuu ujao.  
 
Ndugu mgeni Rasmi,
Ushiriki wa Wanawake katika siasa na katika ngazi za maamuzi, ni eneo lililo na changamoto lukuki na hivyo linahitaji kuhimizwa na viongozi wa ngazi za juu, asasi za kiraia, wanawake wenyewe na viongozi wa dini. 
Makundi niliyoyataja hapo juu yakitimiza wajibu wake katika kuhimiza na kuelimisha juu ya umuhimu wa wanawake katika uongozi, basi ni dhahiri kuwa, tutafikia ule usawa wa 50 kwa 50 ambao tumekuwa tukiupigia kelele kwa muda mrefu. 
Kwa sasa takwimu zinaonyesha kuwa bado ni asilimi 37 tu ya wanawake ndio walioko katika ngazi za maamuzi bungeni, hata hivyo bado tunaona kuna mapengo katika ushiriki wao ambayo hayana budi kuzibwa.
 
 Ndugu mgeni rasmi,
 Mapengo hayo ni pamoja na lugha dhalilishi wakati wa uchaguzi zinazowakatisha tamaa wanawake kuwania nafasi za uongozi, uteuzi usiozingatia jinsia ndani ya vyama vya siasa, hofu na kutojiamini kwa baadhi ya wanawake wenye nia ya kugombea na ilani za vyama zisizozingatia jinsia. 
Mapengo mengine yaliyobainika ni pamoja na rushwa ya ngono inayotajwa kutumika wakati wa uchaguzi, rushwa ya kifedha, uchumi duni kwa wanawake wanaotaka kugombea na hivyo kupelekea kushindwa kufanya kampeni. 
Mapengo mengine ni mila na desturi kandamizi, zinazowazuia kabisa wanawake wasishiriki katika siasa.
 
Ndugu mgeni rasmi,
Ipo pia mitazamo hasi katika jamii kuwa mwanamke anapoingia katika siasa basi amejishushia heshima na hadhi yake kwani hakuumbwa kuwa kiongozi, hayo yote yanachangia kupunguza idadi ya wanawake viongozi. 
Mapengo mengine ni chama kuwa na mapendekezo na utaratibu binafsi kwa kumthamini mwanaume zaidi hususan katika majimbo ambayo chama kina matarajio makubwa ya ushindi.
 
Ndugu mgeni rasmi na viongozi wa dini, 
TAMWA inawasihi kuendelea kuhimiza umuhimu wa wanawake kushiriki siasa na katika ngazi za maamuzi kwani nyinyi mnaaminika katika jamii kutokana na wajibu wenu mkuu. 
Viongozi wa dini, mna nafasi kubwa katika kuhimiza jamii, kuondoa mila na mitazamo potofu inayochochea ushiriki duni wa wanawake katika siasa na katika ngazi za maamuzi. 
 
 Ndugu mgeni rasmi,
Viongozi wa dini wanategemewa kuhubiri Amani na mshikamano katika kipindi cha uchaguzi na amani hiyo itapatikana iwapo makundi yote maalum wakiwamo watu wenye ulemavu na wanawake, watashiriki kikamilifu katika uchaguzi. 
Ndugu mgeni rasmi.
 Kwa kuwa Tanzania imesaini mikataba mbalimbali inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa na mikataba mbalimbali ya amani,  hivyo basi, tunaomba yafuatayo yazingatiwe ili kuondoa vikwazo vyote vinazouia ushiriki wa wanawake katika siasa. 
 
1. Taasisi za dini kutoa elimu kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa na kuondoa mitazamo yote potofu inayokwamisha ushiriki wao  na kutoa mafundisho katika Quran na Biblia yanayomuonyesha mwanamke kama shupavu na mleta mabadiliko ili kuwajengea wanawake kujiamini. 
 
2. Serikali  na viongozi wa dini kukemea na kuwachukulia hatua  wanaotoa lugha dhalilishi  kwa wagombea wanawake wakati wa uchaguzi.
 
3. Vyama vya Siasa vitambue kwamba vina wajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha haki na usawa wa Wanawake ndani ya vyama vyao na katika jamii kwa ujumla, kwa kuwa Wanawake ndiyo kundi kubwa la wapiga kura Tanzania. 
 
4. Vyama vya siasa vizingatie mchakato wa uteuzi wa wagombea kwa kuzingatia mrengo wa jinsia, kama Sheria Mpya ya Uchaguzi inavyoainisha.
 
5. Tunawaomba wanahabari kutumia kalamu zao kimaadili kwa kuepuka kuchochea lugha dhalilishi na kuidunisha taswira ya mwanamke katika jamii. 
 
6. Vyombo vya vya habari na wanahabari wanapaswa kupaza sauti zao kuhimiza ushiriki wa wanawake katika siasa na kulinda utu wake ili kuleta Amani na ushiriki kamilifu katika uchaguzi.
 
7. Wanawake waondoe dhana chonganishi zinazoenezwa kuwa hawapendani na hawawezi bali waendelee kusimama imara na kujitokeza kwa wingi katika chaguzi zijazo.
 
TAMWA tunaliombea Taifa likatawaliwe na upendo, Amani na mshikamano katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 28.
 Mungu ibariki Tanzania!
 
Rose Reuben.
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar es Salaam Agost 12, 2020. Wakati macho na masikio ya Watanzania yakiisubiri kwa hamu Oktoba 28 ambayo ni siku ya uchaguzi mkuu nchini, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) pamoja na Global Peace Foundation (GPF) tunaoa mapendekezo kwa  vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, kuondoa changamoto zote zinazochagiza ushiriki duni wa wanawake katika siasa. 
Uchaguzi Mkuu unafanyika wakati ambapo kati ya wagombea 16 waliochukua fomu kugombea urais, wapo wanawake wawili mpaka sasa ambao ni Queen Cathbert Sendinga wa Chama cha ADC, na Cecilia Augustino wa Demokrasia Makini walioteuliwa na vyama vyao kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi huo. Kadhalika, wapo wanawake watano wanaowania umakamu wa Rais, katika mchakato huu wa uchaguzi. 
Lakini TAMWA, WiLDAF  na GPF  taasisi ambazo malengo yake ni kuwepo kwa jamii yenye amani, inayoheshimu haki za binadamu kwa mtazamo wa kijinsia, na amani zimeona ni vyema kuikumbusha jamii, wadau wa masuala ya siasa na ya jinsia  kuzifanyia kazi changamoto zinazochangia ushiriki duni wa wanawake katika siasa. 
 TAMWA WiLDAF  na GPF  chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Afrika, (AWDF) kupitia mradi wa ‘Wanawake Sasa’ imeendesha midahalo mbalimbali ya wanawake kutoka  vyama vya siasa ,wakiwamo wanawake wanasiasa, viongozi wa dini na kubaini kuwa bado kuna changamoto  zinazopelekea ushiriki mdogo wa wanawake katika siasa.
Midahalo tuliyofanya  katika  kanda za Dodoma, Arusha, Zanzibar na Dar es Salaam, iliibua changamoto zinazowakabili wanawake katika siasa ikiwamo lugha dhalilishi  zinazowavunja moyo wanawake  wanaogombea au walio katika nafasi za uongozi pamoja na familia zao kuwania nafasi mbali mbali za uongozi.
Wanawake wanaogombea nafasi za uongozi, hukutana na changamoto  ya lugha dhalilishi wakati wa kampeni, na hata wakati wa utendaji wao wa kazi ili tu kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma. Kama tunataka uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia, ni muhimu kwa tume ya uchaguzi na vyombo vya usalama kupiga marufuku na kutoa adhabu kali kwa wanasiasa watakaotoa lugha hizi dhidi ya wanawake, Rose Reuben, Mkurugenzi TAMWA.
Katika midahalo hiyo, TAMWA , WiLDAF  na GPF  tumebaini kuwepo kwa rushwa ya kifedha katika shughuli za kawaida za siasa na hasa wakati wa chaguzi mbali mbali za ndani ya vyama, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. Hii ni pamoja na tabia za wajumbe wanaotegemewa kupiga kura kuwa na hulka ya kudai au kujenga mazingira ya kupewa kitu kidogo ili waweze kutoa ushirikiano kwa mgombea. Hii inaathiri  wanawake ambao wengi wao hawana kipato cha kutosha hasa wanawake vijana. 
 
Pia tumebaini uwepo wa vitendo vya kuomba au kutengeneza mazingira ya rushwa ya ngono kwa baadhi ya wanaume wenye dhamana za kusimamia michakato ya chaguzi au mamlaka ndani ya vyama vya siasa.Changamoto hiyo husababisha wanawake kudhalilishwa na kuharibiwa ndoto zao za kisiasa na wakati mwingine familia au wenzi wao kuwazuia kushiriki katika siasa. 
Hayo na mengine mengi, yanachangia wanawake, kuvunjika moyo na hivyo kutoshiriki shughuli za siasa au kukosa nafasi za uongozi pale wanapokuwa na msimamo wa kutotoa rushwa.
Katika hili tunapenda kutoa rai kwa wanawake wenzetu kukataa kabisa kudhalilishwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ya fedha au ngono na pia tunashauri jumuiya za wanawake ndani ya vyama vya sisasa kuvunja ukimya na kuhakikisha hoja za rushwa katika siasa inazungumzwa katika kila vikao vya jumuiya na vikao vingine muhimu. 
Pia tunaviomba vyama vya siasa viweke utaratibu madhubuti na wa siri wa kutoa taarifa za vitendo hivi na kuwe na kamati huru ndani ya vyama zisizofungamana na yeyote zitakazoratibu upokeaji, ufuatiliaji na utoaji adhabu kwa wale ambao bado wanaendekeza vitendo hivi vya kuwadhalilisha wanawake.   
Changamoto nyingine zilizoibuliwa katika midahalo hiyo,  ni Ilani za vyama vya siasa ambazo hazitoi nafasi kwa wanawake kuwa viongozi na kupata nafasi ya kugombea katika majimbo. Tumebaini wanawake wengi wanashindwa kushiriki uchaguzi kwa kutopata baraka hii kuanzia ndani ya vyama.
Wakati huo huo tunavitaka, vyama hivyo viwachague wanawake wenye uwezo wa kisiasa na wa uongozi.
Tunapenda kuvipongeza vyama vya siasa ambavyo vimetoa nafasi za wanawake kugombea nafasi za udiwani na ubunge na hata urais katika kura za maoni. 
“Mwaka huu wanawake wengi wamejitokeza. Tungependa kuviomba vyama vya siasa kuhakikisha kuwa wale wanawake wenye uwezo wasimamishwe kugombea nafasi hizo na tunawaomba wananchi wote kuwachagua wanawake waliosimamishwa kugombea nafasi za ubunge na udiwani, na wengine wapewe nafasi za teuzi mbalimbali Mkurugenzi wa GPF , Martha Nghambi. 
Tunavikumbusha vyama kuendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake ambao hawakupata nafasi mwaka huu ili waweze kusimama na kugombea chaguzi zijazo ndani ya vyama vyao, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kadhalika tunapenda kuwaasa wanawake kuepuka kugawanywa na zile kauli kuwa, hawapendani badala yake waendelee kushirikiana na kupeana fursa mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na masuala ya kijamii.
Kauli hizi za kuwa wanawake hatupendani si za kweli bali zimekuwa zikitumika katika jamii kuwagawa wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, Reuben 
Tunatarajia kuwa serikali, wadau wa siasa, vyombo vya usalama vitazingatia kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DK John   Pombe Magufuli ya kuwepo kwa mazingira wezeshi kwa wanawake katika uchaguzi mkuu na katika nafasi za uongozi na maamuzi. Pia tunampongeza kwa kuendelea kumchagua Mama Samia Suluhu kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu ujao. 
 
Tungependa kumalizia kwa kusisitiza kauli zilizotolewa na Rais, viongozi wa vyama mbali mbali na tume ya taifa ya uchaguzi kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa ni  huru, haki na wa amani. 
Tunawakumbusha wagombea wote kuhakikisha kuwa hawatoi kauli zozote za uvunjifu wa Amani, kuchochea vurugu, kuwagawa watu kwa dini au makabila yao au matusi na udhalilishaji wa kijinsia kwa wagombea wengine. 
Wakati huo, TAMWA, WiLDAF na GPF  inaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendelea kuhimiza uchaguzi huru, wa haki na usawa na kutengenezwa kwa mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea wote.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ubariki Uchaguzi Mkuu wa Octoba 2020. 
 
Rose Reuben Mkurugenzi Mtendaji - TAMWA
Anna Kulaya Mkurugenzi - WILDAF
Martha Nghambi Mkurugenzi - GPF

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Ndugu Wanahabari,

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia uzima, afya njema na kuniwezesha kukutana nanyi ili niweze kuongea na watoto, wazazi/walezi na jamii kupitia kwenu wanahabari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2020.

Ndugu Wanahabari,

Tarehe 16 Juni, ya kila mwaka, Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ikiwemo Tanzania huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika. Chimbuko la maadhimisho haya ni mauaji ya watoto takribani 2,000 yaliyofanywa na Utawala wa Makaburu katika Kitongoji cha Soweto, nchini Afrika Kusini tarehe 16 Juni, 1976. Mauaji hayo yalitokea wakati wa maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakipinga mfumo wa elimu ya kibaguzi nchini humo. Mwaka 1991 viongozi wa Umoja wa Nchi za Afrika walifanya uamuzi wa kuienzi siku hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya watoto hao. Maadhimisho haya yanatumiwa na wadau wote katika nchi za Afrika kutathmini ya hali ya upatikanaji wa haki na ulinzi kwa watoto kwa lengo la kuboresha ustawi na Maendeleo ya watoto.

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
WAJIBIKA KULINDA UTU WA MWANAMKE UPATE KURA YAKE
01/09/2020
Wanamtandao wa Katiba, Uchaguzi na Uongozi ambao ni watetezi wa haki za wanawake na wasichana, yakiwemo masuala ya kukuza ushiriki wao katika uongozi wa kisiasa,    na pia tukiwa ni  wadau wakuu wa uchaguzi kama wapiga kura na wagombea katika nafasi mbalimbali za uchaguzi. Tumekuwa  tukifuatilia  kwa ukaribu mkubwa sana mchakato mzima wa uchaguzi tangu ulipoanza na matukio mbalimbali ambayo tayari yameshajitokeza ikiwemo utumiaji wa lugha za matusi na kauli mbaya za udhalilishaji dhidi ya wanawake wanaogombea na wafuasi wa vyama kwa ujumla. Kwa mfano, kumekuwepo na lugha za kutukana Wanawake wagombea wakiitwa “Malaya”, n.k 
 
Ni vema tutambue kwamba kasumba hii mbali na kwamba ni kinyume na haki za binadamu na ni kosa kisheria, inarudisha nyuma jitihada za serikali katika kufikia usawa wa kijinsia na kurudisha nyuma ari ya wanawake wengi kugombea nafasi za uongozi kwa sababu ya kuogopa kudhalilishwa. Halikadhalika,  inanyamazisha sauti za wanawake ambao ni zaidi ya nusu ya watanzania wote ambao ni wapiga kura wakuu na ambao wanahaki ya ushirki salama katika masuala ya kisiasa, suala ambalo halina tija kwa taifa letu. Kutokana na hali hii, tunaona umuhimu wa vyombo na mamlaka zinavyohusika kuwawajibisha kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi kwa wote wanaotumia matusi na lugha za kudhalilisha wanawake.
 
 Sisi, Wanamtandao watetezi wa haki za wanawake nchini, tunachukulia matukio haya kama kuvunjwa kwa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), inayokataza ubaguzi wa aina yoyote, na  tunaikumbusha jamii  kwamba Kanuni ya Makosa ya Adhabu, Sura ya 16, kifungu cha 89 kinataja kutumia lugha chafu dhidi ya mtu mwingine kuwa ni kosa la jinai. 
 
Tunaomba Umma wa Watanzania na Vyombo mbalimbali vinavyosimamia uchaguzi wa taifa hili utambua kwamba, ushiriki wa wanawake katika michakato ya uchaguzi ni haki yao ya kikatiba, na zimebainishwa katika sheria mbalimbali za nchi. 
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi huweka  wazi Kanuni mbalimbali za uchaguzi na Maadili ya vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kwa  lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa Watanzania wote, wakike na wakiume, kushiriki katika mchakato huu wa uchaguzi na kutoa mchango wao, kwa uhuru, uwazi na amani. Vile vile, Sheria ya Vyama vya Siasa, iliyorekebishwa mwaka 2018, katika kifungu chake cha 9, inakataza viongozi na wanachama wake kutamka au kutumia lugha za matusi, maneno ya kudhalilisha, uchochezi, au alama ambazo zinaweza kusababisha au kuhatarisha amani na ukosefu wa umoja wa kitaifa.
 
 Vilevile  Kanuni za  maadili ya Uchaguzi zilizotolewa katika Gazeti la Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania la tarehe 5/06/2020 zimebainisha mambo yaliyokatazwa kufanywa na vyama vya siasa kifungu ca 2.2 (b)  kinakataza kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjfu wa amani au kuashiria ubaguzi wa jinsia, ulemavu, rangi au maumbile kwenye mikutano na kwenye shughuli zote za kampeni.
 
Kwa kuzingatia hili katazo, na kwa kuzingatia haki zetu za kikatiba na sheria za nchi, Sisi kama watetezi wa  haki za wanawake na usawa wa kijinsia hapa nchini, tunataka yafuatayo yazingatiwe ili kutokomeza udhalilishaji wa wanawake hasa kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu: 
Tunazitaka mamlaka zinazohusika (Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama Vya Siasa, na Taasisi nyingine husika kuwachukulia hatua kali kwa wagombea, pamoja na wapambe wao, wanaotoa lugha za kudhallisha na kutukana wanawake kwenye kampeni au mahali popote wakati huu wa uchaguzi m
Tunawataka viongozi wa taasisi mbalimbali zikiwemo za dini, na hasa vyama vya siasa, Asasi za Kiaraia, na Jamii yote kwa ujumla ya Tanzania kukemea vikali tabia hizi za kudhalilisha wanawake hasa kipindi hiki cha uchaguzi.
 
Vyama vya Siasa vitambue kwamba vina wajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha haki na usawa wa Wanawake ndani ya vyama vyao na katika jamii kwa ujumla, kwa kuwa Wanawake ndiyo kundi kubwa la wapiga kura Tanzania. Kwahiyo lazima viheshimu UTU wa mwanamke  na kutoa fursa na kuweka mazingira yaliyo ya wazi na wezeshi ili wanawake wengi washiriki kikamilifu katika kutimiza haki yao ya kikatiba kama wagombea  na wapiga kura.
 
Mwisho na siyo kwa daraja, sisi wanawake wote kwa ujumla wetu, bila kujali Imani za kiitikadi, tukemee, tukatae na kuwajibisha wale wote wenye kutudhalilisha kwa njia yoyote ile, ikiwa ni pamoja na kututukana  
 
Tunawataka wanahabari na vyombo vya Habari kutumia taaluma yao vizuri kutetea UTU, HAKI ya mwanamke na hususani kipindi hiki cha uchaguzi. Vyombo vya Habari visishiriki katika kusambaza taarifa zenye lugha za matusi na udahlili zilizodhamiria katika kumdalilisha mwanamke wa Taifa hili.
 
 
Tamko hili la kukemea lugha za matusi dhidi ya wanawake ni mwendelezo wa matamko ambayo Wanamtandao tumeshayatoa tangu uchaguzi huu uanze. TUNALAANI NA KUKEMEA KWA NGUVU ZOTE MATUMIZI YA LUGHA ZA MATUSI, LUGHA ZA KEJELI, UDHALILISHAJI,  KATIKA KIPINDI CHOTE CHA UCHAGUZI
 
 
Imetolewa leo Septemba 1, 2020
Mtandao wa Wanawake Katiba Uchaguzi na Uongozi.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinaungana na Watanzania wote kuomboleza kifo cha Mwanadiplomasia Mkongwe, mwanahabri mahiri na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.

TAMWA inakumbuka mchango wa Rais Mstaafu Hayati BWM katika kuijenga nchi hii kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni lakini hasa inaukumbuka mchango wake katika kujenga na kuhimiza usawa jinsia, kisheria, kisera na katika ngazi za maamuzi.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Chama cha wanahabari wanawake Tanzania TAMWA, kinaungana na watanzania wote , wakiwemo watoto wa tanzania, kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika. Hii ni siku muhimu sana kwa sababu wadau, jamii na nchi kwa ujumla wake, tunapaswa kutafakari masuala mbalimbali yanayohusu watoto kupitia siku hii.

Search