Press Release

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Dar es Salaam, Novemba 12, 2020. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinalaani vikali, matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoendelea hapa nchini katika kipindi cha miezi miwili.

Hivi karibuni, vyombo vya habari vimeripoti matukio kadhaa ya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji wa watoto yanayoashiria kuwa bado vitendo hivi vinaendelea licha ya kuwepo sheria, matamko na sera zinazopinga vikali matukio hayo.

Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na lile la Novemba 11, mwaka huu, ambapo  Mwenyekiti wa Kijiji cha Ijinga, Wilaya ya Magu, Badri  Masengo (40) anayedaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita,Shule ya Msingi Ijinga mwenye umri wa miaka 15 .

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar es Salaam, Machi 29, 2021. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mwanahabari wa IPP Media, Blandina Sembu.
 
Taarifa ya Jeshi la Polisi inasema kuwa, mwili wa Sembu, aliyekuwa mtangazaji wa kipindi cha Wanawake, kinachorushwa na ITV, uliokotwa katika maeneo ya Bamaga usiku wa kuamkia Machi 28, hali ambayo inaonyesha utata wa mazingira ya kifo chake. 
 
TAMWA kimesikitishwa na tukio hilo lililompoteza mwanaharakati wa masuala ya wanawake, masuala ya watu wenye ulemavu na mwanahabari aliyeipenda kazi yake. 
 
"TAMWA ikiwa ni mdau mkuu wa wanahabari wanawake nchini , kimeguswa na tukio hilo na tunaziomba mamlaka husika kuchukua hatua za uchunguzi ili kujua undani wa kifo cha Sembu ikiwa kimesababishwa na watu basi hatua kali zichukuliwe kwa watekelezaji wa tukio hilo" Rose Reuben, Mkurugenzi wa TAMWA
 
TAMWA  itamkumbuka Sembu kwa mchango wake mkubwa katika masuala ya Ushiriki wa Wanawake katika Siasa na Uongozi kwani alikuwa ni mjumbe wa kamati ya  Muungano wa Ushiriki Tanzania iliyoangazia Ushiriki wa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana katika siasa na uongozi. 
 
 Kuondoka kwa Sembu ni pengo kubwa kwa tasnia ya habari, jumuiya za watu wenye ulemavu na pia katika jumuiya zinazotetea haki za wanawake nchini kwani alijitoa kwa dhati na alihakikisha anasemea haki za makundi hayo, pale inapobidi.
 
TAMWA inatoa salamu za pole kwa wanafamilia wote wa Blandina Sembu, Watendaji na Wanahabari wa IPP Media, wanaharakati wa masuala ya jinsia, watu wenye ulemavu na wanahabari  wote  nchini.
 
Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji- TAMWA.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Septemba 3, 2021. 
Dar Es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinampongeza Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe kwa kusimamia kidete masuala ya ukatili wa kijinsia yanayotokea wilayani humo.
 Mchembe akitimiza majukumu yake ya kazi wilayani humo, ameweza kuibua ukatili unaofanywa na baadhi ya askari polisi wilayani humo, wanaodaiwa kuwashika sehemu za siri wasichana, kuwabaka, kuwapiga na kuwalazimisha kuwa na mahusiano ya kimapenzi. 
Mchembe ambaye pia kisheria ndiyo mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya, amenukuliwa akisema wazi katika mkutano huo kuwa; Mimi kama Mkuu wa wilaya, unyanyasaji wa kijinsia Handeni, Hapana.
Mkuu huyo wa Wilaya alichukua hatua za kuitisha mkutano baada ya kuwepo kwa madai ya  askari kuwapiga   na kuwajeruhi wasichana wawili katika ukumbi wa starehe wilayani humo kwa kile kinachodaiwa walikataa kuwa na mahusiano na askari hao. 
Katika mkutano huo walikuwepo wasichana ambao walitoa ushahidi wa wazi kuwa wanalazimishwa kuwa na mahusiano na askari na endapo wanawakataa basi wanawekwa mahabusu bila sababu ya msingi.
 Mashahidi wengine katika mkutano huo wamesema kuwa baadhi ya askari polisi huingia kwenye kumbi za starehe na kuwapiga wasichana bila sababu anuwai yenye mashiko.  
 Kadhalika, DC Mchembe alisimamia kidete tukio la mwezi Agosti mwaka huu, la mtoto wa miaka 10 kubakwa  mara kadhaa na kijana wa miaka 20 wilayani humo. 
TAMWA tunaamini kwamba utendaji kazi wa namna hii unaofanywa na Mheshimiwa Mchembe, utasaidia kupunguza matukio ya  ukatili wa kijinsia ambao umekuwa ukisababisha madhara makubwa ya kimwili na kiakili kwa watoto wa kike na wanawake. 
 Kadhalika, tunakemea vikali vitendo vya askari polisi kutumia madaraka yao vibaya  na kufanya ukatili wa kijinsi kama huu. 
Hakuna aliye juu ya sheria, na ndiyo maana askari wana dhamana ya kusimamia sheria hizi, lakini cha ajabu baadhi wamekuwa wa kwanza kuzivunja, Dkt Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji, TAMWA.
Dkt Reuben amesema ukatili wa namna hii sio tu unavunja haki za binadamu lakini pia ndicho chanzo cha madhara mengi ikiwamo mimba zisizotarajiwa, mimba za mapema, magonjwa ya kuambukiza na wakati mwingine madhara ya kimwili kama majeraha. 
Polisi wasimamie maadili yao ya kulinda raia na mali zao, wasiwe washika bendera wa kuendeleza ukatili wa kijinsia, hakuna aliye juu ya sheria, amesema Dkt Reuben. 
TAMWA tunaomba askari watakaobainika kufanya ukatili huo wachukuliwe hatua huku tukiendelea kumtia moyo Mheshimiwa Mchembe kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto wilayani humo. 
Dkt Rose  Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinaungana na Watanzania wote kuomboleza kifo cha Mwanadiplomasia Mkongwe, mwanahabri mahiri na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.

TAMWA inakumbuka mchango wa Rais Mstaafu Hayati BWM katika kuijenga nchi hii kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni lakini hasa inaukumbuka mchango wake katika kujenga na kuhimiza usawa jinsia, kisheria, kisera na katika ngazi za maamuzi.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Septemba 13, 2021. Dar Es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuteua wanawake wawili katika Baraza la Mawaziri.
 
Uteuzi huo umefanyika jana ambapo Dkt Ashatu Kijaji ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na  Teknolojia ya Habari, wakati Dkt Stergomena Tax ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. 
 
Uteuzi huu unafanya idadi ya mawaziri wanawake kufikia saba, kutoka watano walioteuliwa awali. 
 
TAMWA tunampongeza Rais Samia pia kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, kumteua mwanamke kushika wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. 
 
"Uteuzi alioufanya Rais, wa kuongeza mawaziri wawili katika baraza unaonyesha dhahiri kuwa wanawake wanaaminika na wana uwezo wa kuleta mabadiliko katika Nyanja zote, kisiasa, kiuchumi na kijamii" Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk Rose Reuben. 
 
TAMWA tunaamini kuwa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi ndiyo nguzo muhimu ya kuleta usawa na ndicho chanzo cha kuleta mabadiliko chanya katika jamii ambayo yataletwa katika usawa, haki na uwajibikaji. 
 
"Rais Samia, ameweza kuonyesha lile ambalo lilidhaniwa haliwezekani kwa kuwaweka mawaziri wanawake katika wizara nyeti  kama ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, pia kwa kuendelea kuteua mawaziri wanawake, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala" amesema Dkt Reuben
 
Kadhalika tunampongeza Rais kwa ile kauli yake wakati akiwaapisha mawaziri hao aliposema: Nimeamua kuvunja taboo (mwiko), iliyoaminika kwamba wizara ya ulinzi lazima akae mwanaume mwenye misuli yake, kazi ya wizara ile si kupiga mizinga au kushika bunduki,  nimevunja taboo(mwiko) hiyo na kumteua dada yetu Tax kutokana na upeo wake mkubwa alioupata akiwa Jumuiya ya Nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara
 
“Hakika Rais amevunja dhana ya kuwa wanaume pekee ndiyo wenye uwezo wa kushika wizara hii, na kwa hili tunategemea Dkt Tax hatatuangusha, bali atasimamia vyema nafasi hiyo na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika masuala ya ulinzi na usalama,kwa kuwa ana uwezo na upeo" Dk Reuben 
Kadhalika TAMWA tunampongeza Rais Samia kwa kusikiliza kilio cha wanahabari na kuunganisha Wizara ya Habari, Mawasiliano na ile ya Teknolojia ya Mawasiliano, kuwa moja. 
Hatua hiyo itawafanya wadau wa habari kufanya kazi kwa ufanisi na wepesi zaidi kuliko hapo awali. 
TAMWA tunaamini kuwa Ushiriki wa Wanawake katika Siasa na Uongozi na katika ngazi za maamuzi ndicho chanzo cha haki, usawa na uwajibikaji na maendeleo  ya nchi. 
Wanawake Wanaweza! Kazi Iendelee!
Dkt Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji - TAMWA

User Rating: 3 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar InactiveStar Inactive
Dar Es Salaam, Julai 20, 2021.
Leo Julai 20, gazeti la Jamhuri, linalotolewa kila wiki, katika ukurasa wake wa kwanza na kuendelea ukurasa wa tatu limeandika habari yenye kichwa  kinachosema: Mambo ya Nje haijamchukulia hatua Balozi".
Katika habari hiyo, inayomtuhumu Balozi wa Libya nchini Tanzania, Bwana Kamal Ramadan Krista kuhusika katika usafirishaji haramu wa wasichana na unyanyasaji wa kingono, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Dk Rose Reuben amenukuliwa akisema kuwa: Sina maoni yoyote kwa sababu habari hii haikufanyiwa uchunguzi wa kutosha
Taarifa hiyo ikaeleza zaidi kuwa Dk Rose“Alipoelezwa kuwa suala hilo ni la kukiukwa kwa haki za watoto wa kike na kusafirishwa nje ya nchi kinyume na sheria huku TAMWA ikijipambanua kuwa watetezi wa haki za wanawake, alishauri watafutwe Polisi wa Kimataifa(Interpol) na Idara ya Uhamiaji. 
Aya ya mwisho ya habari hiyo imesema: Mkurugenzi huyo ameonyesha kutofurahishwa na gazeti la Jamhuri kuandika tuhuma dhidi ya mwanadiplomasia huyo.
Mkurugenzi wa TAMWA anakiri kupigiwa simu na kutembelewa na mwandishi wa Habari wa gazeti hilo Bwana Alex Kizenga tarehe 16 Julai mwaka huu majira ya mchana ambako alihitaji maoni dhidi ya Habari iliyochapishwa katika gazeti hilo wiki tatu nyuma iliyomtuhumu Balozi Krista kusafirisha wasichana wa kitanzania kwenda kufanya biashara ya ngono nchini mwake.   
Mbali na kukataa kutoa maoni kuhusu Habari hiyo kwa msimamo kuwa haikuwa na taarifa kutoka vyanzo vya msingi ama vilelezo. Mkurugenzi wa TAMWA hakukubali kutoa maoni wala kuzungumza maneno kama ilivyonukuliwa na gazeti hilo na  badala yake mhariri na mwandishi  wa Jamhuri Media ambao walidhamiria kumuandika katika taarifa hiyo wamemlisha maneno Mkurugenzi wa TAMWA Dk Rose Reuben.
Ifahamike kuwa chama hiki ni cha kihabari na hivyo kinafahamu misingi yote ya taaluma ya habari na mawasiliano na hivyo tunasikitishwa na mmonyonyoko huu wa maadili uliofanywa  na gazeti la Jamhuri.
Kwa unyenyekevu tunawataka waombe radhi katika gazeti hilo. 
Kadhalika, TAMWA inafanya kazi na wanahabari kila siku na imekuwa ikiruhusu mahojiano na Mkurugenzi Dk Rose Reuben bila kuweka vikwazo, lakini endapo chama hakijatoa ruhusa ya kunukuliwa, basi maombi hayo yaheshimiwe kama maadili ya kihabari yanavyofundisha. 
Kwa kuwa TAMWA ni sehemu ya wanahabari, tunapenda kutoa wito kwa wanahabari wote kufuata misingi na maadili ya habari pindi wanapotimiza majukumu yao. 
Dkt. Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji ~ TAMWA.

Search