Press Release

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar Es Salaam, Oktoba 29, 2021.
 
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinalaani  tukio la Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, kudaiwa kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wa kike chuoni hapo.
 
Taarifa iliyotolewa na Chuo hicho baada ya kusambaa kwa jumbe za uwepo wa tukio hilo chuoni hapo katika mitandao ya jamii,  imeeleza kuwa Mhadhiri huyo, Petrol Mswahili, amefanya vitendo hivyo kwa wanafunzi wa kike, jambo linalodhihirisha uwepo wa rushwa ya ngono. 
 
TAMWA ikiwa ni taasisi inayopinga unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake ikiwamo rushwa ya ngono, tunalaani  tukio hilo linalovunja maadili ya utumishi wa umma na zaidi hasa kudhalilisha watoto wa kike katika taasisi hii ya elimu ya juu.
 
Kadhalika, TAMWA tunasikitishwa na  vitendo hivyo ambavyo sio tu vimekuwa chanzo cha kuharibu mustakabali wa kitaaluma wa watoto wa kike, lakini pia ndicho chanzo cha magonjwa ya kuambukiza, sonona na kurudisha nyuma kundi hilo. 
 
Mwaka 2019 TAMWA ilifanya tathmini ya kuangazia ukubwa wa rushwa ya ngono kwenye vyumba vya habari, maeneo ya kazini na taasisi za elimu ya juu, na kubaini kuwa tatizo hilo lipo kwa ukubwa wake.
 
Kadhalika TAMWA ilibaini kuwa ukimya umetawala kwa wale waathirika wa rushwa ya ngono kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo woga wa kukosa vibarua, kufukuzwa shule au kufeli mitihani yao. 
 
Hivyo tunalaani vikali vitendo hivi huku tukiupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuchukua hatua za haraka dhidi ya mhadhiri huyo lakini pia tunaushauri uongozi wa chuo hicho kuweka mikakati itakayokomesha vitendo hivyo.
 
TAMWA inaomba pindi uchunguzi utakapokamilika basi sheria ichukue mkondo wake ili iwe funzo kwa wahadhiri wengine wanaoharibu watoto wa kike. Pia tunaiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) iendelee kushirikiana na wadau kutoa elimu kuhusu rushwa ya ngono na udhalilishaji mwingine wa kijinsia. 
 
"Digrii bila rushwa ya ngono, ni digrii yenye tija"
 
Imetolewa na;
 
Mkurugenzi Mtendaji waTAMWA,
 
Dk Rose Reuben.
 

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar Es Salaam, April 13, 2021. Wakati kukiwa na mabadiliko ya teknolojia ulimwenguni kote, matukio ya ukatili wa kijinsia nayo yamekuja katika muundo mwingine wa njia ya mitandao ya kijamii.
Kutokana na mabadiliko hayo, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Friedrich Ebert Stiftung (FES), leo kinazindua kampeni maalum ya kupambana na ukatili wa kijinsia unaofanywa kwa njia ya mitandao ZUMICA #ZuiaUkatiliMtandaoni. 
Kampeni hiyo ya  mwezi mmoja, kuanzia mwezi 4 hadi 6 mwaka, 2021 inalenga, kupinga  vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike mitandaoni.
Ilizoeleka kuwa ukatili wa kijinsia unafanywa katika hali ya kudhuru mwili,  kama vile vipigo, ubakaji/ulawiti, ukeketaji, ndoa za utotoni, mimba za mapema, rushwa ya ngono na matusi, Roes Reuben, Mkurugenzi Mtendaji -TAMWA
Lakini baada ya kukua kwa teknolojia, ukatili huo sasa unafanyika kwa njia ya mtandaoni ambapo wanawake/ wanaume na hata watoto huweza kudhalilishwa kwa namna mbalimbali kwa kutumia mitandao ya internet kama vile facebook, whatsap, instagram, you tube na twitter.
 Wakati huo huo, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la watumiaji wa intaneti ambapo mpaka mwaka 2017, watumiaji waliongezeka kwa asilimia 16 na kufikia 23 milioni na asilimia 82 kati yao walitumia mitandao hiyo kwa njia ya simu. 
Takwimu za Globalstats  Feb 2020 - Feb 2021, zinaonyesha watanzania wanaotumia mtandao wa Facebook ni  38.81% ukifuatiwa na twitter 20.95% ,Youtube 11.25% na mwisho kabisa Instagram 5.78%.
 
 
“Tumeona  mara kadhaa video za utupu za wanawake, watoto wakike zikisambazwa katika mitandao hiyo. Tumeshuhudia matukio ya video za ngono za wanawake zikisambazwa kwa makusudi kabisa, huu ni udhalilishaji unaofanyika kwa njia ya mtandao, Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji -TAMWA.
Udhalilishaji huu una madhara kisaikolojia na hata kupelekea waathirika kuathirika kisaikolojia, hata kupelekea kujiua au kupoteza mwelekeo katika maisha. 
Nia ya TAMWA na FES ni kuzuia ukatii, kuongeza uelewa kwa jamii kujua madhara ya ukatili huu , lakini hasa wanawake kujua mbinu za kuepuka udhalilishaji wa aina hiyo, Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji -TAMWA.
Tunafahamu kuwa zipo sheria zinazozuia ukatili huu, kwa mfano, Sheria ya Maudhui ya Mitandaoni (Online Content Regulation) inakataza na kutoa adhabu kurusha maudhui ya udhalilishaji ikiwamo picha/video za utupu, lugha za udhalilishaji zinazokwenda kinyume na utamaduni wa Mtanzania.
Hata hivyo, bado udhalilishaji huu unaendelea, pengine ni kwa waathirika kutoifahamu sheria hii, au kuona aibu katika kutafuta haki au hofu ya kudhalilika zaidi pindi kesi itakapopelekwa mahakamani.
TAMWA tunasema, ni vyema kujua kuwa udhalilishaji huu haukubaliki, ni muhimu kutambua kuwa zipo sheria zinazotulinda, na ni muhimu zaidi kujua kuwa wapo wadau wanaoweza kukusaidia kuipata haki yako, Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji-TAMWA.
 
Aidha, kuna adhabu kwa wanaotumia mitandao hii ya kijamii vibaya ikiwamo faini ya Sh 5milioni au kifungo kisichopungua miezi 12 au kwa vyote kwa pamoja. 
Ukatili huu wa mtandaoni umeonekana kuwaathiri zaidi watoto wa kike na wanawake kutokana na namna ya makuzi na desturi za jamii yetu.
Baadhi  ya watekelezaji wa udhalilishaji huu  hutumia mitandao ya kijamii kama fimbo ya kuwachapia wanawake na watoto wa kike pale wanapofanikiwa katika jambo fulani au kupata nyadhifa mbalimbali za uongozi. Wakati mwingine, wanawake na watoto wa kike hudhalilishwa kwa sababu tu, ya wivu wa kimapenzi. 
Kwa mfano unapofika msimu wa uchaguzi ndiyo wakati ambao video au picha  za wagombea wanawake za udhalilisha husambazwa zaidi mitandaoni  kuonyesha kuwa hawafai kupata nafasi  za uongozi wanazowania, Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji-TAMWA.
 
Mifano mingine ni baadhi ya wasanii wa muziki na maigizo nchini hasa wanawake, ambao picha zao kusambaza picha za wanawake za kuwadhalilisha katika mitandao yao ya kijamii. 
Haya matukio yasichukuliwe ya kawaida, yakaonekana kama ada na sehemu ya desturi zetu, tunaiomba serikali iyavalie njuga na kuwapa adhabu kali wanaokutwa na hatia, Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji-TAMWA
TAMWA inatoa wito kwa serikali na asasi za kiraia  kuzungumzia madhara ya vitendo vya ukatili wa mitandaoni na kutoa elimu kwa jamii na kwa kizazi cha sasa, kuhusiana na madhara ya kutumia mitandao ya kijamii kama njia ya  kufanya vitendo vya ukatili ya kijinsia.
 “Wito wetu kwa jamii ni kuwa masuala ya ukatili wa kijinsi ni jukumu la kila mmoja wetu,  Asasi za kiraia, madawati ya kijinsia,Serikali, jeshi la polisi,Wasaidizi wa kisheria pamoja na watu maarufu kama wasanii katika  fani mbalimbali  tushirikiane  kwa vitendo kukemea vitendo hivyo.”
Kwa taarifa zaidi,
Rose Reuben.
E-mail:  This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar Es Salaam, Machi, 19, 2021. Bodi ya wanachama, wanachama na Sekretariati ya Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa Makamu wa Rais, ameapishwa leo, Machi 19, 2021 baada ya kifo cha Hayati Rais John Magufuli ikiwa ni utekelezaji wa hatua za kikatiba na kisheria inayoeleza kuwa, Makamu wa Rais ataapishwa kuwa Rais, endapo Rais aliyeko madarakani atafariki dunia. 
 
TAMWA tunampongeza Rais huyu wa awamu ya sita, tukiamini kuwa ni kiongozi amestahili, makini na  anayekwenda kusimamia maadili, kusimamia katiba na kuzisimamia haki za wanawake na watoto. 
 
Tunaamini Rais wetu mpya ni muumini wa usawa wa kijinsia na hivyo atakwenda kuwa mstari wa mbele kusimamia sheria na haki zinazolinda watu wote, ikiwa ni pamoja na mwanamke hakika hatuna shaka na utendaji wake, TAMWA inaamini   ‘Wanawake Wanaweza  na sio kwa kuwezeshwa pekee bali waliaminika tangu enzi kwa kupewa madaraka ya kuwa  wasimamizi wakuu wa familia, kuanzia ngazi ya malezi,  jambo ambalo linawafanya kuwa imara, wanyenyekevu, wavumilivu na makini  zaidi hata katika nafasi za kisiasa na uongozi katika maeneo mengine.
 
Tangu akiwa Makamu wa Rais, amekuwa chachu kwa watoto wa kike na wanawake wa Tanzania katika kuwaza makubwa kwenye kuleta mabadiliko katika jamii ya kijinsia.
 
Hatuna  shaka na  utendaji kazi wa Rais wetu mpya na  historia yake ya kufanya kazi katika taasisi zisizo za kiserikali, kwa zaidi ya miaka kumi ambapo alijikita zaidi katika harakati za usawa kijinsia. 
Hivyo basi tunaamini kuwa atakwenda kusimamia ajenda hizo akiwa anaelewa kwa kina umuhimu wa usawa wa kijinsia na umuhimu wa kumaliza ukatili wa kijinsia,
 
Rais Samia Suluhu Hassan ameweka historia Afrika Mashariki  kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais, jambo ambalo  litaacha alama kwa vizazi vijavyo na kisha kuulinda  na kuuheshimisha mfumo wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi. 
Wakati tukiendelea kuomboleza msiba wa Hayati Rais John Magufuli, TAMWA ina imani kuwa, Rais Mama Samia Suluhu ataendelea kusimamia kauli yake  ile ya kuitaka jamii  kupinga na kupambana na vitendo vya ukatili katika maeneno yao.
 
Hongera Rais Samia Suluhu Hassan! Hongera Tanzania!
 
Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji,
TAMWA.

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
Dar Es Salaam, October 11, 2021. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinawakumbusha, wazazi, walezi, wadau, serikali na waandishi wa habari kuchukua hatua ili kuondoa aina mpya ya ukatili kwa njia ya mitandao ya kijamii.
 
Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Oktoba 11, ambapo kwa mwaka huu, kauli mbiu ya kitaifa na kimataifa ni: Kizazi cha Kidijitali, Kizazi Chetu!.
 
Kauli mbiu hii inalenga kuikumbusha jamii kutoa haki sawa kwa watoto wote kwenye teknolojia ya kidijitali ili waitumie  kwa Maendeleo na kwa usahihi.  
 
Zipo faida lukuki za matumizi ya mitandao ya kijamii, kama vile elimu kwa njia ya mitandao, taarifa muhimu za kitaifa na kimataifa lakini  bado watoto wa kike wameonekana kuachwa nyuma katika ulimwengu wa kidijitali kwa kukosa  fursa sawa hasa katika matumzi ya intanenti, kumiliki simu janja, na uhuru wa  kutumia mitandao ya kijamii kama ilivyo kwa watoto wa kiume. 
 
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya wanawake, (UN-Women) Julai mwaka huu, ilionyesha kuwa kuna ongezeko la ukatili wa kijinsia kupitia mitandao ya kijamii. 
 
Ripoti hiyo imeeleza: Upatikanaji  wa intaneti kwa watoto wa kike na wanawake, umesababisha kundi hilo kukumbana na udhalilishaji wa kingono zaidi, ukilinganisha na wanaume,
 
Kadhalika ripoti hiyo imeonyesha zaidi kuwa, watoto wa kike wamekuwa wakitishiwa kimwili, kutumiwa picha za ngono, na kupewa lugha dhalili katika mitandao ya kijamii.
 
Kwa hapa Tanzania, matukio kadhaa ya udhalilishaji wa kingono kwa njia ya mtandao yamewahi kuripotiwa ikiwamo kusambazwa kwa video za ngono zikiwaonyesha watoto wa kike, huku mwanaume akifichwa uso.
 
Aina nyingine ya ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao ni kashfa na matamshi ya chuki, jina la akaunti kuibwa na  na kisha kutumiwa na watu kwa njia za utapeli au kurushwa kwa video za ngono. Hili limewakuta zaidi watoto wa kike wenye majina makubwa au maarufu katika jamii. 
 
Lakini pia, imekuwa ni tamaduni kwa watoto wa kike kurushiwa lugha dhalilishi kwa njia ya mtandao, ikiwamo zile zinazohusisha baadhi ya maungo yao ya mwili.
 
Picha za watoto wa kike zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii na kugeuzwa mjadala jambo ambalo limeonekana kuchangia kuongezeka kwa lugha dhalili dhidi yao.
 
Kutokana na kuongezeka kwa matukio haya yanayoendana na ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii, hatuna budi kupunguza udhalilishaji huu na kuendelea kuhimiza matumizi sahihi, salama na yenye faida, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben.
 
Reuben ameomba  wazazi, walezi, serikali, asasi za kijinsia, asasi za kiraia, wapatanishi na wanahabari, kusimamia usalama wa watoto kike mitandaoni. 
 
Inawezekana tabia hizi zinaonekana kuwa ni za kawaida au kugeuzwa utamaduni lakini zimeleta madhara kwa watoto wa kike ikiwamo kukatisha masomo, kujiua, kutengwa na jamii na baadhi kuathirika kisaikolojia, Dkt, Reuben
 
TAMWA inaamini katika usawa wa kijinsia, haki za watoto na wanawake, hivyo katika kuadhimisha siku hii, tunaikumbusha serikali kutunga sheria zinazoendana na kasi ya teknolojia ili kuwabana wale watakaofanya ukatili wa kingono kwa njia ya mtandao.
 
Sheria isifumbe macho katika masuala haya, lakini si hayo tu, bado tunasisitiza hata ile sheria ya ndoa  ibadilishwe ili kumpa mtoto wa kike haki ya kusoma na kuolewa katika umri wa utu uzima Dkt. Reuben
 
TAMWA inapenda kutoa wito kwa jamii kuona umuhimu wa matumizi ya dijitali katika jamii yetu ili kuendana na uhalisia wa dunia, pia  kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kutoa na kuwezesha watoto wote kupata elimu ya masuala ya dijitali pia kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya kidijitali  kwa kuzingatia jinsi zote bila ubaguzi.
 
TAMWA inaamini kuwa, maadhimisho ya mwaka huu, yataangazia  changamoto na fursa za kidijitali  kwa mtoto wa kike lakini bila kusahau, kuwa kumbe; malezi bora, elimu kwa mtoto wa kike ndicho chanzo cha leo kuwa na Rais wa kwanza mwanamke, ambaye ni Mama Samia Suluhu.
 
Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ni siku ya kimataifa iliyotangazwa na Umoja wa Mataifa; pia inaitwa Siku ya Wasichana na Siku ya Kimataifa ya Wasichana. Siku hii huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 11.
 
Umoja wa Mataifa ulianza kuadhimisha siku hii baada ya kuonekana kuna changamoto nyingi zinazomuandama mtoto wa kike ikiwamo kunyimwa fursa ya kupata elimu, ubakaji, ulawiti,  ndoa za mapema, mimba za mapema na kukosa haki nyingine ikiwamo ya kucheza na kushauri katika ngazi ya familia. 
 
Maadhimisho hayo pia yanaangalia  mafanikio ya watoto kike kidunia, ikiwamo Tanzania kama vile  kuongezeka kwa idadi ya watoto wa kike wanaopata elimu ya juu, watoto wa kike kuendelea kupata elimu ya afya ya uzazi na kufikiwa na taasisi mbalimbali zinazogusa maisha ya mtoto wa kike.
 
Kizazi cha Kidijitali, Kizazi Chetu!
 
Dkt Rose Reuben.
Mkurugenzi Mtendaji - TAMWA

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania kwa kushirikiana na Mtandao wa wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani Tanzania na kuratibiwana Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) kwa pamoja tunaungana na watanzania wote na Dunia kwa ujumla kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka Wahanga wa ajali za Barabarani.

Siku hii huadhimishwa kimataifa, kila ifikapo Jumapili ya wiki ya tatu (3) ya mwezi Novemba kila mwaka Kwa ajili ya kuwakumbuka waathirika wa ajali za barabarani na kuwaenzi mamilioni ya watu waliopoteza maisha na wengine wengi walioathirika kwa njia moja au nyingine kutoka na ajali hizo.

Kauli mbiu ya kimataifa kwa mwaka huu inasema; ‘Kumbuka, Saidia,Chukua Hatua’.

User Rating: 4 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Inactive
Dar es Salaam, Oktoba 1, 2020. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kina furaha kubwa kuutambulisha umma wa Watanzania, kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa ‘Wanawake Wanaweza’, unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wanawake (UN-Women).
Hii ni fursa adhimu kwa TAMWA ambayo baadhi ya malengo yake makuu ni utetezi wa haki za wanawake na watoto, kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, kuondoa mifumo kandamizi inayochochoea ukatili kwa makundi hayo maalum, kwa kutumia vyombo vya habari. 
Hivyo basi jukumu  la TAMWA  katika mradi huu ni kuongeza uelewa kwa umma kuhusu umuhimu wa ushiriki wa Wanawake katika siasa na katika uongozi na madhara ya magonjwa ya mlipuko kama Covid-19 kwa wanawake na wasichana.
“Katika kufanikisha lengo kuu la mradi huu, TAMWA itawajengea uwezo wanahabari  katika kuripoti habari za jinsia na ufuatiliaji wa ushiriki wa wanawake katika uongozi na siasa,Rose  Reuben, Mkurugenzi Mtendaji, TAMWA. 
Kadhalika ili kufanikisha hayo, TAMWA itaendesha midahalo ya kihabari kwa ajili ya kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi. 
Mikoa 16 ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Mtwara, Wilaya 112 za mikoa hiyo na kata 458, ndiyo maeneo  yatakayotumika kama sampuli ya utekelezaji wa malengo ya mradi huu.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, kuwa malengo ya mradi huu yatatimizwa kwa kutumia vyombo vya habari, hivyo basi TAMWA itashirikiana na wadau wake wakuu ambao ni vyombo vya habari, zikiwamo runinga 10, redio za kijamii 50, radio za masafa marefu 10 , magazeti 20 na mitandao ya kijamii, ili kuifikia jamii. 
TAMWA inatambua kuwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi (hasa ya kisiasa) bado ni mdogo, hali ambayo inakinzana na azma ya kujenga jamii isiyokuwa na ubaguzi kama ilivyobainishwa kwenye dira ya Taifa 2025, Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, pamoja na sheria mbalimbali za nchi. 
Kwa mfano, ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC: 2016) inaonyesha kuwa, asilimia 17 ya mawaziri ni wanawake, makatibu wakuu wanawake ni asilimia 11, wakuu wa mikoa ni asilimia 23, wakuu wa wilaya ni asilimia 28 na hii inaonyesha kuwa bado nafasi ya mwanamke katika ngazi za uongozi ni mdogo. 
“Hata hivyo, bado tunaupongeza  uongozi wa awamu ya tano, kwa mara ya kwanza alichaguliwa Makamu wa Rais mwanamke nchini, Mama Samia  Suluhu Hassan Reuben
Hivyo basi katika kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji wa mradi huu, TAMWA, inatarajia kutumia nyenzo zake muhimu kuongeza uelewa kwa jamii na kuhakikisha wanawake wanaonekana kuwa viongozi halali na madhubuti katika jamii yetu Reuben 
Kama tulivyoainisha awali, kuwa wadau ni muhimu katika utekelezaji wa mradi huu, hivyo wadau wengine tutakaowashirikisha ni Chuo Kikuu cha Dar es Salam, kitivo cha Sayansi ya Jamii, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Shirika la  Wanasheria Wanawake na Maendeleo Afrika, (WILDAF), Viongozi wa dini na Mtandao wa radio za kijamii nchini (TADIO), Wizara ya Habari na Wizara ya Afya.
Wengine ni Mtandao wa Wanawake Viongozi Afrika (AWLN) na machampioni wa GEWE, Viongozi wa kimila, Kituo cha Demokrasia nchini(TCD).
 Hawa wote ni wadau ambao TAMWA itafanya nao kazi wakati wa utekelezaji wa mradi huu, na kwa nafasi yao watakuwa na mengi ya kuishirikisha TAMWA na umoja huu ndicho chanzo cha mafanikio ya utekelezaji wa mradi huu, Rose Reuben
TAMWA ambayo kiini chake ni wanahabari, inatarajia kushirikiana na vyombo vya habari ili kufikisha hii ajenda ya ushiriki wa wanawake katika siasa na katika uongozi kwa jamii, tukiamini kwamba, wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii. 
Viongozi wa dini, taasisi za habari, taasisi za jinsia, ambazo TAMWA inakwenda kushirikiana nazo, ni nguzo muhimu katika kufanikisha adhma kuu ya mradi huu,Reuben.
Bila kuwasahau viongozi wa kimila na viongozi wa mikoa, wilaya na kata mbalimbali ambazo tutazifikia, TAMWA inatarajia ushirikiano mkubwa kutoka kwao. 
Mkurugenzi Mtendaji 
Rose Reuben
TAMWA.
 

Search