Press Release

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Oktoba 11, 2023. Dar Es Salaam.Kila ifikapo Oktoba 11, dunia huadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani. Siku hii inatukumbusha kutambua changamoto zinazowakumba watoto wa kike.

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) inatambua kwamba watoto wa kike hapa nchini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali. Hivyo tunapoadhimisha siku hii, hatuna budi kuziangazia ili kukumbushana kuwa mapambano yanaendelea ili kumfanya mtoto wa kike kupata haki zake katika jamii.

TAMWA katika safari yake ya miaka zaidi ya 35 ya kuhamasisha upatikanaji wa haki za wanawake na watoto wa kike, imekutana na madhila mengi dhidi ya watoto wa kike na miongoni mwa hayo ni ukeketaji, mimba za utotoni, ndoa za utotoni na uminywaji wa haki za kupata elimu kwa watoto wa kike.

Lakini kadri dunia inavyobadilika ndivyo tunavyoona kuwa ili kuyaondoa hayo yote, basi suluhu la kudumu ni kuwekeza katika elimu. Ndiyo maana kauli mbiu ya mwaka huu inasema: “Wekeza katika haki za watoto wa kike: Uongozi wetu, ustawi wetu’

Kauli mbiu hii inajikita katika kuamsha hamasa kwa jamii, asasi za kiraia, serikali na watunga sera kuwekeza katika kuzitambua na kuzitekeleza haki za mtoto wa kike, na pia kutumia nafasi za uongozi kuwastawisha watoto wa kike.

Hivyo basi, TAMWA inaipongeza serikali kwa kuwekeza zaidi katika kujenga mabweni na shule za watoto wa kike, kutoa ufadhili wa masomo na kuwapa watoto wa kike kipaumbele katika nafasi za kielimu. 

Lakini bado kuna mapengo makubwa katika jamii yetu hasa ya kimtazamo kwamba watoto wa kike hawana umuhimu wa kupata elimu. 

“Na hili linakwenda sambamba na mila na tamaduni ambazo zinaamini mtoto wa kike hana haki ya kupata elimu. Hivyo wakati serikali na wadau wengine wakiwekeza katika elimu, wapo wazazi au familia zinazomtupa mtoto wa kike asipate elimu”Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk Rose Reuben

Katika kupata suluhisho la changamoto hizi, TAMWA tumefanya miradi kadhaa inayolenga kumuinua mtoto wa kike kielimu. Kwa mfano, TAMWA imefanya midahalo kadhaa na watoto wa kike, katika shule za Nambilanje na Likunja, mkoa wa Lindi, shule ya sekondari ya Mugabe, Sinza, Dar es Salaam, nia ni kusikiliza sauti zao na kujua wanachotaka. 

“Tunaposikiliza sauti zao, tunajua changamoto wanazopitia na hivyo tunajua wapi pa kuchukua hatua tunapozingatia haja zao, wasichana hawa nao wanaongeza kasi ya kutetea mabadiliko yao katika jamii wanazoishi” Dk Rose Reuben

Kwa mfano, katika mdahalo uliofanywa katika shule ya msingi Likunja, watoto wa kike walibainisha kuwa, wazazi huwaambia waandike makosa katika mitihani yao ya kumaliza darasa la saba, ili wasifaulu. 

Walimu katika shule hiyo walisema, matukio ya wazazi kuwafundisha watoto wa kike waandike ‘makorokocho’ kwenye mitihani yameongezeka baada ya serikali kujenga zaidi shule za sekondari na hivyo wanafunzi wanaofaulu kuongezeka. 

“TAMWA tunaamini katika dunia ambayo watoto wa kike wana nafasi ya kusoma na kuiwajibisha serikali, dunia ambayo watoto wa kike watakuwa viongozi katika ulimwengu wa teknolojia, tafiti na uvumbuzi. Na tunatamani mifano hii isiwe hadithi, bali mifumo yetu ya kawaida” Dk Rose Reuben

TAMWA inasisitiza jamii, hususan wazazi, kuwapa nafasi watoto wa kike na kuendelea kuwekeza katika elimu, kwani sio tu kwamba kundi hili wana uwezo kielimu lakini pia wana uwezo katika uongozi kama tunavyoona sasa Tanzania ina Rais mwanamke, ambaye ni Samia Suluhu Hassan. 

“Nafasi ya Rais Samia Suluhu Hassan kama kiongozi, iwe chachu  na hamasa kwa jamii kuendelea kuwekeza kielimu kwa mtoto wa kike,” Dk Rose Reuben.

Mkurugenzi Mtendaji 

Dk Rose Reuben

TAMWA

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar es Salaam, 15 May, 2022 Wakati dunia  ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA)kinawakumbusha watanzania kutathimini hali ya maendeleo ya familia, na kuwahimiza wazazi na walezi kutoa huduma muhimu za matunzo na kuzuia vitendo vya ukatili kwa watoto ambavyo vimekithiri hapa nchini.
Kama kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inavyosema: Dumisha amani na upendo kwa familia imara, jitokeze kuhesabiwa TAMWA tunawakumbusha wanafamilia kuepuka migogoro inayopelekea kusambaratika na kuacha watoto wakikosa huduma muhimu ikiwamo upendo wa wazazi au walezi.  
“Hivi karibuni kumeripotiwa matukio kadhaa ya ukatili wa watoto ikiwemo vipigo, mauaji, udhalilishaji wa kingono na hata watoto waliojiingiza katika vitendo vya uhalifu maarufu kama Panya Road, ambayo yanaonyesha wazi kuwa ipo hitilafu kubwa iliyoikumba taasisi ya familia Dr. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji-TAMWA
 Kadhalika  kauli mbiu hii ya kitaifa ya Siku ya Kimataifa ya Familia inazikumbusha familia umuhimu wa kushiriki sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu, zoezi ambalo litaiwezesha serikali kubaini takwimu sahihi za watu na kaya ili kupanga mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya familia. 
‘Sensa ni zoezi muhimu la kitaifa kwani ni ukweli usiopingika kuwa maslahi ya watoto na sapoti ya familia kama taasisi vinakamilishwa kwa kubainishwa kwa takwimu sahihi za watu, mipango ya kifedha, na rasilimali nyingine zinazomilikiwa na familia, baada ya zoezi hili TAMWA tunaiomba serikali kutengeza Sera ya familia iyakayoainisha wajibu, maslahi ya kiuchumi na mipango kwa familia kama taasisi Dr. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji- TAMWA
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloangalia maslahi ya watoto (UNICEF) zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya ukatili wa watoto unafanyika majumbani na asilimia 40 unafanyika mashuleni, hivyo kuna umuhimu wa watanzania wote kuthamini na kuimarisha taasisi ya familia kwa upendo na amani.
Pia kwa mujibu wa taarifa za makosa ya ukatili wa jinsia na unyanyasaji zilizotolewa na Jeshi la Polisi katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka 2021 zinaonyesha mikoa ya kipolisi iliyoongoza kwa ukatili dhidi ya watoto ni Arusha 808, Tanga 691, Shinyanga 505, Mwanza 500 na Ilala 489.  
Kadhalika makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ya matukio ni ya ubakaji 5,899, kumpa mimba mwanafunzi 1677, ulawiti 1,114, kumzorotesha mwanafunzi masomo 790 na shambulio 350. 
Familia ni chanzo cha rasilimali watu, na ndio maana Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1993 lilitoa tamko namba 47/237 na  kuitangaza Mei 15 kuwa siku maalumu ya kutathimi hali ya familia, upatikanaji wa huduma muhimu na maendeleo yao.  
TAMWA tunaendelea kusisitiza watanzania, kuthamini ngazi ya familia, kama eneo la kwanza la kuonyesha upendo, kuanzisha maendeleo na kurithisha vizazi vyetu elimu, mali na hekima. 
Ngazi ya familia ndiko kunakoanzia maendeleo, afya na kunakojenga taswira ya tabia ya mtu mmoja mmoja, familia ni muhimu, Dr Rose Reuben. 
Mkurugenzi Mtendaji 
Rose Reuben
TAMWA

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Dar es Salaam, Mei, 20. 2022.  Imekuwa ni ada sasa kwa duru zetu za habari kutawaliwa na  matukio ya ubakaji hasa kwa watoto.

Katika kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu, matukio makubwa yaliyotikisa vyombo vya habari ni pamoja na lile la mkoani Katavi, ambapo mwalimu wa Mafundisho ya dini ya Kikristo Joseph John, kukamatwa kwa kulawiti watoto wanne.

Tukio jingine ni lile la mkazi wa Iringa, kudaiwa kumlawiti mtoto wake  wa kambo na shemeji yake. Kadhalika, liliripotiwa tukio lililobeba vichwa vingi vya habari la mtoto wa miaka 14 mkazi wa Iringa, kuwalawiti watoto wenzake 14 wote wa kiume.

Kadhalika hili la juzi, Mei 18 ambapo mwalimu wa Madrasa Jumanne Ikungi, mkazi wa Arusha kwa tuhuma za kuwalawiti wanafunzi takribani 22 wa shule ya msingi Mkonoo, jijini Arusha. Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda alithibitisha  baada ya kufika katika shule hiyo na kuzungumza na wazazi, walimu na wanafunzi ikiwa ni baada ya kukamilisha alichokiita uchunguzi wake juu ya mwalimu huyo wa madrasa.

 Kwa matukio hayo yaliyoripotiwa kati ya Januari na Mei, inatosha kusema kuwa watoto wetu hawapo salama na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) tunalazimika kusema, ‘watoto hawa hawana pa kukimbilia’.

“Mwenendo huu wa matukio ya ubakaji na ulawiti wa watoto tena na walimu, viongozi wa dini na wazazi au walezi, unadhihirisha kuwa tatizo hili bado ni kubwa nchini na linahitaji maamuzi magumu kutoka kwa watunga sera wetu,” Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk Rose Reuben.

TAMWA pamoja na wadau wengine wa masuala ya jinsia, tumekuwa tukiimba wa kuitaka jamii kuzuia ukatili kwa miaka zaidi ya 30 sasa tukililia mabadiliko ya sera, sheria na hata kutoa elimu kwa jamii. Lakini bado tatizo hili linaendelea, tena sasa likitekelezwa na viongozi waliotegemewa kuwalinda watoto wetu, tuliodhani kuwa ni walimu wa kukuza maadili mema kwa watoto.

“Tunahitaji zaidi ya sheria kukomesha ukatili huu, tunahitaji maamuzi magumu kutoka ngazi zote kuanzia familia, wanajamii, viongozi wa dini zote na serikali kwa ujumla wake kwa sababu watoto walio taifa la kesho, wanaharibiwa kimwili na kisaikolojia” Dk Rose Reuben.

Wakati huo huo, taarifa za makosa ya ukatili wa jinsia na unyanyasaji zilizotolewa na Jeshi la Polisi katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2021 zinaonyesha mikoa ya kipolisi iliyoongoza kwa ukatili dhidi ya watoto ni Arusha 808, Tanga 691, Shinyanga 505, Mwanza 500 na Ilala 489. 

Kadhalika makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ya matukio ni ya ubakaji 5,899, kumpa mimba mwanafunzi 1677, ulawiti 1,114, kumzorotesha mwanafunzi masomo 790 na shambulio 350.

Wakati tukiendelea kutafuta suluhisho la janga hili, TAMWA inaendelea kutoa elimu katika shule za sekondari na msingi, kuhusu mada za ukatili wa kijinsia, lakini bado hakuna mitaala shuleni inayogusa masuala ya afya ya uzazi moja kwa moja.

“Utafiti uliotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Haki Elimu, unaonyesha kuwa watoto wengi hawafundishwi elimu ya afya ya uzazi, lakini  zaidi hasa walimu nao wanaogopa kufundisha wanafunzi mada hizo, hapa ndipo mzizi wa tatizo ulipo,”

“Ni dhahiri kuwa mambo yanayouhusu afya ya uzazi na ukatili wa kingono hayazungumzwi ndani ya familia wala shuleni tena wengine wanaona ni mambo ya aibu yasiyostahili kujadiliwa, hivyo yanabaki kuwa masuala ya wadau na serikali ambao nao husuluhisha tatizo na sio mzizi wa tatizo,” Dk Rose Reuben.

Wakati tukijiandaa na zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, ifikapo Agosti 23,  ni wakati muhimu kwa  viongozi, wazazi, walezi, wasimamizi wa sheria, wadau wa masuala ya jinsia na watoto kujitathmini wapi penye mapengo, ili tuzibe ombwe hili la ubakaji wa watoto.

TAMWA imesikitishwa na ubakaji huu wa watoto unaoendelea hapa nchini na tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kutamka kuwa hili ni janga na kutoa maamuzi magumu kunusuru watoto wetu.

 Dk Rose Reuben

Mkurugenzi Mtendaji

TAMWA

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar Es Salaam, Oktoba 11, 2022. Watanzania leo wanaungana na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike. Siku hii inaadhimishwa  ifikapo Oktoba 11 kila mwaka kama wakati wa kukumbushana kuhusu nafasi ya mtoto wa kike katika nyanja mbalimbali, za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
 
 Hivyo basi kwa kuzingatia umuhimu wa siku hii, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kwa kushirikiana na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) tunaikumbusha jamii, wadau na serikali kuwa bado matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike yanaendelea kushika kasi nchini.
 
Kadhalika, kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo: Muda Wetu ni sasa, haki zetu, Mustakabali Wetu”. TAMWA na WFT tunalenga kuikumbusha jamii kuendelea kuibua na kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia, hasa rushwa ya ngono, ubakaji, ulawiti, vipigo na ndoa za mapema kwa watoto wa kike. 
 
TAMWA na WFT tumebaini kuwa licha ya  vyombo vya dola kuchukua hatua na kupinga vikali vitendo hivyo dhidi ya watoto wa kike lakini bado matukio ya rushwa ya ngono, ubakaji, ulawiti, mimba za mapema na udhalilishaji yanazidi kushamiri huku watuhumiwa wengi wakiwamo wazazi, walezi, walimu pamoja na watu wao wa karibu ambao ndio wamepewa jukumu la kulinda watoto hao.
 
Imeshuhudiwa kuwepo kwa matukio kadhaa ya ukatili wa kijinsia kwa  watoto  wa kike katika kipindi cha  Julai hadi  Septemba mwaka huu  jambo ambalo linatupa wasiwasi kuwa huenda elimu ya kulinda haki za mtoto wa kike bado haijawafikia wengi.
 
Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na lile la mwanafunzi wa darasa la saba, Shule ya msingi Shahende, Geita, Helena Mashaka (13) anayedaiwa kuchomwa  moto mikononi na mama yake hali iliyosababisha kushindwa kufanya mitihani yake ya darasa la saba. 
 
Kadhalika, mtoto Farida Makuya (16)  anadaiwa kuuwawa usiku wa Jumanne, Oktoba 4, 2022 nyumbani kwao Mtumba jijini Dodoma na watu wasiojulikana. 
 
Wakati huo huo, Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwabaka na kuwalawiti watoto zaidi ya 10 wa mafundisho ya kipaimara na kisha kuwapa fedha kiasi cha kati ya Sh 3,000 hadi 5, 000. 
 
Tukio jingine ni la mwanafunzi wa darasa la sita, (12), wa Shule ya Msingi Mbagala Kuu, Dar es Salaam,  anadaiwa kubakwa na Mwalimu wake, ambapo  Mwalimu huyo amekuwa akimpatia binti huyo ufunguo wa makazi yake binafsi ili endapo akimuhitaji aweze kufika kwake kwa urahisi.
 
Hata hivyo, tunaipongeza serikali kupitia vyombo vya sheria kwa kutumia muda mfupi kusimamia na kutoa hukumu dhidi ya mwalimu wa shule ya msingi ya Global, Dar es Salaam, aliyehukumiwa kifungo cha maisha kwa kubaka na kulawiti mwanafunzi wa miaka minane. 
 
Utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) umebaini kuwa wasichana milioni 120, duniani wamewahi kulazimishwa kufanya ngono bila ridhaa yao.
 
Pamoja na ukatili huo kwa watoto wa kike, WFT na TAMWA  bado wanasisitiza jamii kuepuka rushwa ya ngono hasa kwa watoto wa kike. 
 
Mwaka 2020, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilichapisha ripoti ya utafiti na kuibua kuwepo kwa rushwa ya ngono katika Vyuo Vikuu viwili vya umma nchini, ambavyo ni Chuo kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
 
Kadhalika, mwaka 2021, TAMWA kwa kushirikiana na (WFT) ilitekeleza mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari. TAMWA ilifanya utafiti na kubaini wanahabari wanakabiliwa kwa kiasi kikubwa na rushwa ya ngono na ukatili mwingine ndani ya vyombo vyao vya habari. 
 
TAMWA tumebaini kuwa wasichana wanahabari vyuoni  hukumbana na vitendo vya rushwa ya ngono na kusababisha wengi kuikimbia taaluma  hiyo wakihofia vitendo vya rushwa ya ngono ambayo hukumbana navyo kuanzia wakiwa vyuoni Mkurugenzi wa TAMWA, Dk Rose Reuben. 
 
TAMWA na WFT bado tunaendelea kuipongeza TAKUKURU kwa kufanya mabadiliko ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.  Hii ni dhamira chanya kwa serikali katika kushughulikia uovu huu katika nchi yetu. Kwa njia hii, inabakia kuwa sheria ya msingi katika kujenga msingi wa maadili ya taifa katika ngazi na taasisi zote. 
 
“Hata hivyo katika kifungu kidogo cha 2,cha sheria hii,  tumeona kuwa uchambuzi wa sheria unachanganya  neno ukahaba na ngono: Pale ambapo kuna makubaliano ya pande zote, ya kubadilishana ngono kwa ajili ya huduma, au pesa, (katika kesi hii hakuna unyang'anyi wa mamlaka). Hivyo tunaomba kuondolewa kwa kifungu kinacholeta utata kati ya rushwa ya ngono na ukahaba Rose Marandu, Mkurugenzi Mtendaji, WFT
 
Hivyo basi tunapoadhimisha siku hii ya mtoto wa kike, tunatamani dunia itambue thamani yao katika maendeleo, afya yao, elimu yao, uchumi wao na ushiriki wao katika siasa, jamii ikiutambua mchango wao, itasimamia katika ulinzi wao na hivyo kupunguza matukio haya ya rushwa ya ngono. 
Tunaomba serikali kupitia Takukuru, kuendelea kujikita katika mapambano haya wakishirikiana na wadau, ili jamii iwe na taarifa za kutosha kuhusu usalama wa watoto wa kike Rose Marandu,WFT
Hatutaacha, hatutanyamaza, hadi uwepo usalama wa watoto wa kike Tanzania!
 
 
Dkt. Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA)
 
 
Rose  Marandu
Mkurugenzi Mtendaji
Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT)
Mwisho

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
June 10th, 2022, Dar es Salaam. The Tanzania Media Womens Association (TAMWA) calls on the Tanzanian government to continue to use the negotiation, and reconciliation process and to follow the procedures for the transfer of land and national resources.
 
The request comes after reports from June 8, 9 and today 10, 2022, showing pastoralists of the Loliondo Maasai tribe and army forces protesting the implementation of the border marking of 1500 square kilometers of their villages for natural resource conservation trending in social media. 
 
We understand and agree with the Prime Minister Kassimu Majaliwa that the loss of peace in any area is causing inconvenience to women, the elderly and children and therefore calls on the government to return to the negotiating table to end the Loliondo conservation crisis with the Maasai community.
 
TAMWA have witnessed many conflicts being resolved through dialogue and reconciliation in this country so we believe that even this conflict can also be resolved without resorting to force or inciting violence that is smearing the nation with human rights abuses.
 
Dr Rose Reuben,
 
 
Executive Director
 
TAMWA

Search