Gallery

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Wakati dunia ikiadhimisha wiki ya Umoja wa Mataifa ya Usalama Barabarani, viongozi wa ngazi mbalimbali nchini wametakiwa kuchukua hatua katika kudhibiti ajali za barabarani ili kuokoa maisha ya wananchi yanayopotea kila kukicha kwa kusababishwa na ajali za barabarani nchini.

Wiki ya Umoja Wa Mataifa ya Usalama Barabarani ilianzishwa kupitia Azimio la Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Oktoba 2005 ikiwa na lengo la kuboresha usalama wa barabarani duniani. Azimio hili liliitaka Tume ya Umoja wa Mataifa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuandaa kwa pamoja wiki hiyo. Kwa mara ya kwanza wiki ya umoja wa mataifa ya usalama barabarani iliazimishwa mwaka 2007 , ya pili mwaka 2013, ya tatu 2015, na ya nne 2017. Mwaka huu ni maadhirimisho ya tano, ambayo yanaadhimishwa kuanzia tarehe 6 mpaka tarehe 12 mwezi huu wa tano 2019.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Wakati dunia ikisherehekea Siku ya Wanawake Duniani, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA) kinakuletea wanahabari wakongwe waanzilishi wa TAMWA. Hiki ndicho wanachokisema katika maadhimisho haya ya Siku ya Wanawake Duniani.

Ummy Mahfoudh.  Ni mwanahabari mkongwe, Mwanachama wa Chama cha Wanahabari  Wanawake tangu 1988. Amewahi kufanya kazi katika taasisi zisizo za kiserikali za kitaifa na kimataifa katika nchi za Uingereza, Denmark, Tunisia na Afrika Kusini.
Ni miongoni mwa walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika mkutano wa kidunia wa haki za mwanamke, maarufu mkutano wa Beijing mwaka 1995. Amewahi kushiriki utafiti wa chanzo cha mauaji ya wanawake wazee kutokana na imani za kishirikina na mauaji ya albino Tanzania. 
 Kwa sasa ni mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya magazeti Zanzibar
Ni mshairi, ana mume na watoto wanne. 
Anachokisema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Tanzania;
“Katika kuadhimisha Siku ya Mwanamke  Duniani, tukumbushane kushughulika na kizazi cha sasa. Tupo kisasa kiasi cha kusahau sisi tulilelewa vipi. Watoto wa kike wafundishwe masuala chanya ya kimila badala ya kufikiri kila kitu cha kimila ni kibaya,”
“Mimi watoto wangu wote nawalea sawa bila kujali wa kike au wa kiume. Wale wa kiume wote wakifikisha miaka 14 wanajua kukuna nazi, kupika nk” (Ummie Mahfoudh)
 

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Florence Majani, TAMWA.

Ruangwa. Licha ya serikali kujenga shule za kata kwa wingi ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari, wazazi wilayani Ruangwa, wamelalamikiwa kuwajengea watoto wao mazingira ya kufeli mitihani ya darasa la saba ili wasiendelee na shule na waolewe.

Hayo yalibainika wakati wa mdahalo kwa wanafunzi kuhusu mila na desturi zinazochochea mimba za utotoni ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA) wilayani Ruangwa.

Kwa nyakati tofauti wanafunzi hao walisema baadhi ya  wazazi huwalazimisha watoto wao kukataa shule au kuwashauri wajifelishe mitihani ya darasa la saba ili waolewe.

“Kuna mwenzetu mmoja, alikuwa na akili sana lakini matokeo yalipotoka hakufaulu kujiunga na sekondari, tulipomuuliza kulikoni alisema mama yake alimwambia aandike 0000 ili afeli na aolewe,” alisema Zahara Chigope, Mwanafunzi wa Kidato cha nne, Sekondari ya Nambilanje.

Mwanafunzi mwingine, Nasma Kumkana, alisema suala la wazazi kuwashawishi wanafunzi wafeli kwa makusudi ni kubwa na wanalisikia kutoka kwa wanafunzi wenzao.

“Sio hivyo tu, hata baadhi ya wazazi tunawasikia wanasema bora mtoto afeli kwa sababu hawana hela za kumhudumia atakapoingia sekondari, hata wakiambiwa elimu ni bure watasema hawana fedha za sare za shule,” alisema

Nasma alisema mila hizo zinaambatana na ile ya baadhi ya wazazi kumshauri mtoto atafute mboga kwa jasho lake.

“Hii ina maana kwamba, mama anamwambia mtoto leo zamu yako kutafuta mboga, kwa maana nyingine,  mtoto wa kike anapewa ruhusa ya kuwa na mwanaume ili apate fedha ya kusaidia familia,” alisema.

Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nambilanje, Charles Chitawala alisema tatizo hilo ni kubwa kwa kata ya Nambilanje na maeneo mengine ya Ruangwa.

“Sisi kama viongozi suala hilo linatuudhi, inabidi tutoe elimu, ili tabia hizo waziache. Ilifikia mahali ikabidi tuitishe vikao vya wazazi na wazazi wajaze mikataba,” alisema.

Alisema mwaka 2018, wazazi walijaza mikataba na kukubaliana kuwa iwapo mzazi atabainika kuwa alimshauri au kumlazimisha mwanafunzi kufeli kwa namna yoyote ile, basi atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwalimu Chitawala alisema mikataba hiyo ilitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na kusainiwa na wazazi wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka jana.

Mratibu wa Elimu kata ya Nambilanje, Lista Mziwanda alisema suala la wazazi kuwalazimisha wanafunzi kuandika  ‘utumbo’ kwenye mitihani ya taifa lipo kwa kiasi kikubwa eneo hilo ingawa hakuna takwimu rasmi.

“Tulizibaini kesi hizo baada ya kuwabana wanafunzi ambao tuliwategemea kufaulu lakini hawakufaulu. Ukikaa na mtoto vizuri anakuambia ukweli kuwa alilazimishwa na mama,” alisema

Alisema kesi hizo ni za wanafunzi ambao walifaulu vizuri kwenye mitihani ya ndani na ile ya kujipima ‘Mock’ lakini mitihani ya taifa walifeli.

“Kinachofanyika sasa ni kutoa elimu lakini na hizo sheria ndogondogo kama kuwasainisha wazazi mikataba kuwa wakibainika kuwalazimisha watoto wafeli, watachukuliwa hatua. Tumeanza suala la mikataba mwaka jana, tutaangalia mwaka huu,”alisema.

Mwalimu Mziwanda alisema kati ya wanafunzi 76 waliomaliza darasa la saba mwaka 2018, 66 walifaulu kwenda Sekondari na wanne wamekwenda Chuo cha ufundi Nkoye.

Mmoja wa wazazi, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama ya kata, Esha Chigope, alisema kesi hizo zipo nyingi.

Esha alisema kuna mkazi mwenzao aliyefahamika kama Tendele, alikiri kumshauri mtoto wake aandike 1111, ili afeli mtihani wa darasa la saba.

“Tendele mwenyewe anasema wazi, alitaka mtoto wake afeli kwa sababu hakuna umuhimu kwa mtoto wa kike kusoma, kwa hiyo kweli mtoto akafeli,” alisema Esha.

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilu alisema watawachukulia hatua wazazi wanaorubuni wanafunzi wafeli na kusema kuwa hiyo  jamii ya wazazi inayohujumu watoto.

“Ndiyo maana tuliingia mikataba kati ya serikali na mzazi, kwamba hata mtoto akifeli, mzazi awajibike kwa kutoa maelezo kwa nini kijana amefeli,” alisema.

Alisema hali ya mwamko wa elimu kwa ukanda wa kusini hasa vijiji vya Nambilanje, Namichiga, Nachienjele na Nanjaro bado ni ndogo  na inahitajika elimu ya kutosha.

Alisema hata katika ziara zake alizofanya katika vijiji 81 vya Wilaya ya Ruangwa, alibaini suala la unyago ndilo linachochea kufifia kwa elimu wilayani humo.

“Watoto wanatolewa kupelekwa unyago kipindi cha masomo. Nilikamata wazazi waliokaidi agizo langu pamoja na watoto 22 waliokuwa wanachezwa huo unyago,”alisema Mgandilu.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) leo Aprili 5, kwa kushirikiana na Hospitali ya Narayani India wametoa  elimu ya afya pamoja na ushauri wa kitaalamu kwa wanahabari wanawake kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya afya ya uzazi na magonjwa na magonjwa ya saratani.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika  jijini Dar es salaam, mwenyekiti wa TAMWA, Bi. Alakok Mayombo alisema washiriki wa mafunzo hayo watajengewa uwezo kuhusu afya ya uzazi pamoja na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

“Katika kipindi cha siku mbili za mkutano mkuu wa chama chetu,  Tulizungumza na marafiki wa TAMWA Narayana hospital ambao walikubali kutoa elimu ya afya uzazi kwa wakina mama kupitia kipengele chao cha awareness kuhusu hasa magonjwa ya kansa" Alisema Bi. Mayombo. 

Alisema kupitia elimu ambayo itatolewa kwa washiriki hao itawawezesha kuwasaidia kujilinda na kupambana  kansa kwa akina mama. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Rose Reuben, alisema, mbali na mafunzo hayo ya afya ya uzazi pia watatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya ya mitandao ya kijamii.

“Ni lazima jamii itambue sheria ya maudhui ya mtandao pamoja na sheria za vyombo vya habari katika mitandao ya kijamii.  Lengo letu ni kujiongezea ujuzi katika maeneo haya, hivyo  watu wa TCRA watakuja kutusaidia kutoa mafunzo kuhusu  matumizi ya mtandao ni”. Alisema Rose.

Nae daktari kutoka Hospitali ya Narayana, Bwana Limbanga Freddie alisema, tafiti zinaonyesha kumekuwepo na ongezeko kubwa la wagonjwa wa kansa kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha pamoja na kutofanya mazoezi, kutokufanya kazi ngumu na kutumia vyakula ambavyo ni hatari kwa afya.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Mkurugenzi wa Chama Cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) aliyemaliza muda wake, Edda Sanga, amepewa tuzo ya heshima ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake katika Asasi za kiraia. Tuzo hiyo imetolewa leo na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP), wakati wa tamasha la 14 la Jinsia. 

“Nimefurahi kupokea tuzo hiyo nawashukuru sana na kuwapongeza pia wale ambao wameona nimestahili kupokea tuzo hiyo,” Amesema Edda Sanga. Pia amewataka wengine waliopata tuzo hiyo kuendeleza mapambano ya kumkomboa mtoto wa kike, kumlinda na kumpa haki yake.

TAMWA tunampongeza Edda Sanga kwa kutwaa tuzo hii adhimu na pia tunawapongeza TGNP Mtandao kwa kuona umuhimu wa kuandaa tuzo hizi.

Search