Gallery

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Florence Majani, TAMWA.

Ruangwa, Lindi. Ni Januari 17 mwaka 2018, saa sita mchana. Kundi la wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za Nambilanje, wameketi mbele ya walimu wao, wakijadiliana kuhusu mila na desturi zinazokwamisha maendeleo na kuchochea mimba za utotoni katika kata hiyo.

Walimu walikuwa kimya wakifuatilia kwa umakini majadiliano hayo.  Wanafunzi  nao hawakuwa na hofu bali walitoa ya moyoni na kueleza kinagaubaga kinachoendelea majumbani.

Majadiliano hayo yaliandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA)  ili kuangalia mila na desturi zinazochochea mimba za utotoni na ukatili kwa wanawake na watoto.

Wanafunzi hao waliweka bayana kuwa, baadhi ya  wazazi ndicho  chanzo cha wao kufeli kwani huwalazimisha kufeli na kuwataka kuandika ‘madudu’ ili wasiendelee na masomo ya sekondari.

Mwanafunzi wa kidato cha nne, shule ya Sekondari Nambilanje, Zahara Chigope anaweka bayana  kuwa wapo wanafunzi wenzake ambao wanashurutishwa na wazazi waandike ‘madudu’ kwenye mitihani ya taifa ili wasiendelee na masomo ya sekondari.

“Mzazi wake alimwambia aandike 11111 kila swali, ili afeli na asiendelee na sekondari,” alisema.

Alisema hata kwa wale wanaofaulu darasa la saba, wapo wazazi wanaokataa kwa makusudi kuwapeleka shule wakidai hawajalipwa fedha za korosho lakini kimsingi, ni ujanja tu ili wasiendelee na masomo.

Zahara alisema mwenzao mmoja aliyekuwa anafaulu vizuri kwenye masomo wakati wakiwa shule ya msingi, alifeli na alipomdodosa imekuwaje, ndipo alipomtobolea siri hiyo kuwa aliambiwa na mama yake aaandike ‘madudu.’

“Kweli alifeli kwa sababu aliniambia aliandika 11111 katika kila swali na sasa hivi yupo mitaani amezaa na wala hajaolewa,” alisema

Mwanafunzi mwingine wa kidato cha tatu wa shule hiyo, Zena Mitawa anasema mwenzao aliyetakiwa kuwa nao kidato cha tatu, alifeli  darasa la saba kutokana na ushauri wa mama yake.

“Alikuwa anatuambia hata kabla hatujafanya mtihani wa taifa kuwa, mama yake hataki aendelee na shule kwani tayari yupo mwanaume wa kumuoa. Kweli matokeo yalipotoka, hakufaulu na sasa ameolewa huko Lindi mjini,” anasema.

Mwanafunzi mwingine, Nasma Kumkana, alisema suala la wazazi kuwashawishi wanafunzi wafeli kwa makusudi ni kubwa na wanalisikia kutoka kwa wanafunzi wenzao.

“Sio hivyo tu, hata baadhi ya wazazi tunawasikia wanasema bora mtoto afeli kwa sababu hawana hela za kumhudumia atakapoingia sekondari, hata wakiambiwa elimu ni bure watasema hawana fedha za sare za shule,” anasema

Nasma anasema mila hizo zinaambatana na ile ya baadhi ya wazazi kumshauri mtoto atafute mboga kwa jasho lake.

“Hii ina maana kwamba, mama anamwambia mtoto leo zamu yako kutafuta mboga, kwa maana nyingine,  mtoto wa kike anapewa ruhusa ya kuwa na mwanaume ili apate fedha ya kusaidia familia,” anasema.

Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nambilanje, Charles Chitawala anasema tatizo hilo ni kubwa kwa kata ya Nambilanje na maeneo mengine ya Ruangwa.

“Sisi kama viongozi suala hilo linatuudhi, inabidi tutoe elimu, ili tabia hizo waziache. Ilifikia mahali ikabidi tuitishe vikao vya wazazi na wazazi wajaze mikataba,” anasema.

Anasema mwaka 2018, wazazi walijaza mikataba na kukubaliana kuwa iwapo mzazi atabainika kuwa alimshauri au kumlazimisha mwanafunzi kufeli kwa namna yoyote ile, basi atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwalimu Chitawala anasema mikataba hiyo ilitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na kusainiwa na wazazi wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka jana.

Mratibu wa Elimu kata ya Nambilanje, Lista Mziwanda anasema suala la wazazi kuwalazimisha wanafunzi kuandika  ‘utumbo’ kwenye mitihani ya taifa lipo kwa kiasi kikubwa eneo hilo ingawa hakuna takwimu rasmi.

“Tulizibaini kesi hizo baada ya kuwabana wanafunzi ambao tuliwategemea kufaulu lakini hawakufaulu. Ukikaa na mtoto vizuri anakuambia ukweli kuwa alilazimishwa na mama,” anasema

Anasema kesi hizo ni za wanafunzi ambao walifaulu vizuri kwenye mitihani ya ndani na ile ya kujipima ‘Mock’ lakini mitihani ya taifa walifeli.

“Kinachofanyika sasa ni kutoa elimu lakini na hizo sheria ndogondogo kama kuwasainisha wazazi mikataba kuwa wakibainika kuwalazimisha watoto wafeli, watachukuliwa hatua. Tumeanza suala la mikataba mwaka jana, tutaangalia mwaka huu,”anasema.

Mwalimu Mziwanda anasema kati ya wanafunzi 76 waliomaliza darasa la saba mwaka 2018, 66 walifaulu kwenda Sekondari na wanne wamekwenda Chuo cha ufundi Nkoye. Mwananchi ilibaini kuwa, mazingira ya kielimu wilayani humo ni magumu kwa baadhi ya wanafunzi ambao hulazimika kubaki  peke yao kwa muda mrefu baada ya  wazazi wao kuondoka nyumbani na kwenda kukaa shambani msimu wa kilimo.

 Mwanafunzi wa shule ya msingi Nambilanje Swaumu Ibadi anasema  mazingira ya kielimu kwake  ni magumu kwa sababu mama yake yupo shambani kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

“Jana usiku sijala, mpaka mchana huu kwa sababu nakaa peke yangu, mama amehamia mashambani na dada yangu niliyeachwa naye, ameondoka,” anasema

Anasema akibahatika kula, basi ni milo miwili tu kwa siku na wakati huo akitembea umbali wa karibu kilometa10 kutoka nyumbani hadi shuleni.

Saumu ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba, anasema hana mahitaji muhimu ya shule kama sare, madaftari na chakula kwa sababu mama yake hajamnunulia.

Kwa mujibu wa Mtendaji wa Kijiji cha Nambilanje, Constatine Odilo, desturi za wazazi kuhamia shambani kipindi cha kilimo zinachangia  kushuka kwa kiwango cha elimu na hata mmomonyoko wa maadili.
“Tunapokea kesi nyingi hapa kijijini za watoto wadogo wa kike kuachwa peke yao nyumbani wakati wazazi wakiwa wamehamia shambani, hili linachangia watoto hawa kuwa huru na hata wasipoenda shule, nani atawajibika?” anasema.

Familia zachangia kushuka kwa elimu, kuvunjika kwa maadili

Pamoja na wazazi kuhujumu elimu ya watoto wao, mambo mengine yanayotajwa kusababisha mimba za utotoni  na kushuka kwa kiwango cha elimu eneo hilo ni wazazi kutengana.

Kwa mfano, Mtendaji wa Kata ya Nambilanje, Abdallah Tamba anasema  kesi nyingi za wazazi kutengana ni nyingi na hali hiyo husababisha watoto kubaki bila malezi.

“Kwa mila za huku, kuachana ni kitu rahisi tu, kama ilivyo kuoa. Kwa hiyo mara nyingi wazazi wanapotengana, watoto ndiyo hupata tabu, wanakosa malezi kabisa,” anasema

Anasema mara nyingi baba anapobaki na watoto, huoa mke mwingine na kama mama huyo hatajali suala la elimu, basi watoto huacha shule.

Lakini watoto wa eneo hilo wanasema wazi kuwa mfumo wa  matrilineal (mama kuwa kichwa cha familia) wa kabila za kusini, ndiyo huchangia changamoto hizo.

Kwa mfano, Nasra Juma, Mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Nambilanje anasema baadhi ya kinamama ndiyo wanaowaambiwa watoto wao wa kike wasiende shule bali washiriki kuleta mboga nyumbani.

“Sasa mama anamwambia binti yake kuwa leo zamu yako kuleta mboga, hiyo ina maana kuwa anamruhusu kwenda kufanya chochote ili alete mboga nyumbani,” anasema

Mila nyingine zinazotajwa kuchangia kushuka kwa elimu ni unyago ambao hufanyika kipindi cha masomo.

Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa TAMWA, John Ambrose anasema zipo mila na desturi zenye manufaa kwa jamii lakini endapo mila hizo zinachochea mimba, kushuka kwa elimu, zinamzuia mtoto kupata haki yake basi hazina budi kupingwa.

“Ndiyo maana tumeandaa midahalo hii, kwa kushirikiana na Taasisi ya Foundation for Civila Society, ili wanafunzi waeleze wazi yanayowasibu nyumbani, shuleni na katika mazingira yao mengine, tumeshuhudia mengi yanayofanyika kwa watoto na yanachangia ukatili kwao,” anasema Ambrose

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Wakati dunia ikisherehekea Siku ya Wanawake Duniani, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA)kinakuletea wanahabari wakongwe waanzilishi wa TAMWA. Hiki ndicho wanachokisema katika maadhimisho haya ya Siku ya Wanawake Duniani.

Halima Shariff, yeye ni mtafiti, kiongozi na mwalimu . Ni miongoni mwa waasisi wa TAMWA aliyezaliwa kutoka katika familia ya kawaida kabisa, mkoani Tanga.
 
Akiwa ni mtaalamu na nguli wa habari nchini, Halima amewahi kuandika katika gazeti la Daily News miaka ya 80 na mtangazaji wa  Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani(Deustche Welle).
 
Pamoja na fani ya habari, Halima amewahi  kushika nafasi kubwa katika taasisi za kimataifa  na kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mradi wa Uzazi wa Mpango wa Advanced Family Planning Project(AFP).
 
Ni miongoni mwa wanawake waliosimamia kidete maendeleo ya wanawake na watoto katika masuala ya elimu, afya ya uzazi na Virusi vya Ukimwi. 
 
Amewahi kuongoza miradi mikubwa ya afya  ikiwamo ya Shirika la Misaada la watu wa Marekani USAID. Ameshiriki katika kutetea hadi  kufanikisha kupitishwa kwa muswada wa  masuala ya Ukimwi, kuanzishwa kwa sera ya HIV/AIDS katika maeneo ya kazi. Amewahi pia kuwa Kamishna wa Tume ya Ukimwi Tanzania (TACAIDS). 
 
Anachokisema katika kuadhimisha Sharif katika kuadhimisha Siku ya Wanawake duniani: 
 
“Kuimarisha nafasi ya mwanamke katika nyanja zote katika jamii ni harakati endelevu zinazohitaji jitihada za pamoja zenye kasi inayoongezeka kizazi hadi kizazi. Kwa mantiki hiyo Tanzania tumefanikiwa kujenga uelewe wa jamii kuhusu nafasi muhimu ya mwanamke katika kujenga familia na katika maendeleo kwa ujumla” 
 
“Lakini bado hatujawekeza vya kutosha katika kuhakikisha afya ya mwanamke inapewa kipaumbele ukizingatia kwamba bado wastani wa kuzaa wa taifa ni watoto sita kwa mwanamke wa rika la uzazi (15-49). 
 
“Inatia moyo kwamba serikali imekuwa ikielekeza nguvu huko lakini ni eneo linalohitaji kutazamwa zaidi kwani mara nyingi wanawake hukosa fursa za kujiendeleza kutokana na changamoto za uzazi,”

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Godwin Assenga, TAMWA.

In Summary

The Tazania Media Women's Association (TAMWA) has appointed Ms Rose Reuben as the new Executive Director effectively from January 7, 2019. 

The new Director is replacing Ms Edda Sanga, whose term in office has expired after saving the Association for over three years.

The new appointed TAMWA Executive Director, Ms Rose Reuben (Right), receiving office documents from the representative of the Association’s Board Chairperson, 

Ms Judica Losai during the handing over ceremony that took place at TAMWA Office in Dar es Salaam on Friday, January 11, 2019.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Aprili 7, 2020. Wakati dunia nzima ikigubikwa na mshtuko kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinapenda kuihadharisha jamii juu ya ongezeko la ukatili wa wanawake na watoto unaoweza kukithiri wakati wa janga la ugonjwa huu.

“Watoto wapo nyumbani wakati huu ambapo serikali imezifunga shule, lakini iwapo wazazi na walezi hawatakuwa makini basi huenda wakaathirika na ubakaji na mimba za utotoni katika kipindi hiki ambacho macho na masikio yapo katika kudhibiti virusi vya Corona,”

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto(UNICEF) linasema, ukatili wa watoto aghalabu hufanyika nyumbani, mtoto akielekea au akitoka shule wakati anapokuwa peke yake bila msaada.

TAMWA inaipongeza serikali kwa kuchukua hatua za haraka za kufunga shule ili kupunguza msongamano unaoweza kusababisha maambukizi, hata hivyo ni muhimu kuihadharisha jamii kuhusu ukatili wa kijinsia na ule wa watoto unaoweza kuongezeka wakati huu.

Endapo wazazi/walezi hawatawasimamia vizuri watoto katika kipindi hiki cha siku 30 zilizotolewa na serikali kupitia Waziri Mkuu, basi tunaweza kutengeneza kizazi kingine kilichoathirika na ukatili wa aina mbalimbali ikiwamo ubakaji, ulawiti na mimba zisizotarajiwa.

Kwa mfano, Ripoti ya UNICEF 2016 inaonyesha kuwa, wakati wa mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi 2014 hadi 2016, ulisababisha ongezeko la ajira kwa watoto, ukatili kwa wanawake na watoto na mimba za utotoni. Kwa mfano, mimba za utotoni nchini Sierra Leone ziliongezeka kufikia 14,000 kutoka 7,000.

“Ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwalinda watoto na virusi vya Corona lakini wakati huo huo tuangalie madhara wanayoweza kuyapata watoto wa kike na wa kiume wanapokuwa nyumbani au mitaani”

Tunapaswa kujiuliza iwapo watoto wetu wapo salama wawapo nyumbani au mitaani wanapotembea wakati huu wa likizo ndefu. Je, Mafataki hawawanyemelei? Je ndugu na jamaa wanaobaki na watoto hawa wanawalinda au wanawaharibu? Je watoto hawa hawatakuwa katika hatari ya kuozwa mapema?

Si hivyo tu, janga hili la Corona linaathiri zaidi wanawake kwani shule zinapofungwa, mzigo mkubwa wa malezi unawaangukia kinamama nyumbani ambao ndiyo walezi wakuu wa familia.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) zinaonyesha kuwa, dunia nzima, asilimia 70 ya watoa huduma za jamii na za afya ni wanawake. Majukumu haya huwaweka mstari wa mbele katika utoaji wa huduma, Je katika janga hili la Covid-19, wanawake wanalindwa ipasavyo wasidhurike?

TAMWA inaiomba serikali, wadau na watunga sera kwanza, kutosahau hatari nyingine zinazoweza kuwapata wanawake na watoto katika kipindi cha janga la Covid-19.

Pili, wadau wa afya, elimu na watoto kutoa mafunzo kuhusu namna ya kujilinda na ya kuripoti kuhusu ukatili kwa watoto wakati huu wa mlipuko.

Tatu, kuongeza upatikanaji wa taarifa na misaada mingine kwa watoto.

Nne, kubuni mfumo wa kuwapa watoto elimu wawapo nyumbani.

Tano, wahudumu wa afya wanawake wawekewe mazingira salama ya kutoa huduma ili wasiathirike.

Sita, wazazi na walezi kuimarisha ulinzi na kuzuia matembezi yasiyo ya lazima kwa watoto.

Rose Reuben

Mkurugenzi Mtendaji,

TAMWA.

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
Na Edina Salila
 
“Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikifanya kazi katika mazingira magumu sana huku nikikumbana na majaribu na matokeo yake, nimekuwa mtu wa bosi wangu kukejeli na kukashfu ili nionekane sijui kutafuta wala kuandika stori (habari) kisa, eti nimemkatalia bosi wangu kimapenzi…”
 
“Kinachoniumiza zaidi ni kuwa, licha ya kuwashirikisha wenzangu, nimeushirikisha uongozi ili kukomesha hali hii ambayo ni tatizo kubwa kwangu, lakini sijashirikishwa wala kuona mabadiliko au hatua zozote zikichukuliwa.”
 
Ndivyo anavyosema Kemmy Mang’ombe (si jina halisi), mmoja wa wandishi wa habari wanawake katika gazeti moja la kibinafsi litolewalo kwa Kiswahili kila siku nchini.
 
Kemmy ambaye ni kiwakilisha cha wandishi wa habari wengi wa kike waliopitia madhira hayo anasema, baada ya kuzidiwa na adha huku akisaka ufumbuzi kwa wandishi wenzake wa kike, alibaini kuwa, wengi walikuwa wakimshangaa kwa kuwa nao, wamekumbwa na madhira hayo; wakalegea na kutumbukia kwenye janga la rushwa ya ngono na wakubwa wao wa kazi.
 
Kwa mujibu wa uchunguzi, miongoni mwa hoja zinazotumiwa na watu wanaodai rushwa hii ambayo kwa kiasi kikubwa huwaathiri vibaya wandishi wa habari wa kike, ni ahadi za kuajiriwa hasa kwa wandishi wa kike ambao hawajaajiriwa, ahadi za kuongezwa vyeo na mshahara (kwa waajiriwa), upendeleo wa kupewa safari na kazi kubwa na msaada wa ziada kuhakikisha kazi (stori) za mlengwa zinatoka.
 
Kwa mujibu wa Kemmy, baada ya kumkatalia mhariri wake, mara kadhaa anapowasilisha habari zake kwa mhariri hasa kubwa, huambulia kejeli kuwa hajui kuandika na kutakiwa kutafuta nyingine.
 
“Cha ajabu, kwa kuwa mimi ni correspondent, ninalipwa kadiri ya kazi zangu zinazotoka, anapozikataa nikaamua kupeleka magazeti mengine, zinatoka na mara tatu zimetoka ukurasa wa mbele na nyingine mbili zikawa ‘lead’ (habari kuu katika gazeti).”
 
“Sasa ndipo ujiulize, huku wanasema sijui kuandika, magazeti mengine, habari hiyohiyo inakuwa kuu; tena magazeti yenye heshima maana stori zinajitosheleza,” anasema.
 
Anaongeza: “Kinachosikitisha, huko kwingine baada ya kuona stori zinatoka nikataka kuhamia huko, nikakumbana na yale yale; nikaangukia kwa bosi mmoja anayesisitiza kutaka nihusiane naye kingono eti stori zangu zitakuwa zinatoka kila siku… Kwa kweli, nikaona kama mambo ni haya, uandishi umenishinda; ngoja nikauze maandazi…”
 
Mwaka 2021, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania, (WFT-T) kupitia mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari, walifanya utafiti uliothibitisha kuwapo vitendo vya rushwa ya ngono na udhalilishaji mwingine wa kijinsia katika vyombo vya habari ukiwamo wa kimwili na maneno. 
 
Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara ya Mwaka 2021/2022 iliyozinduliwa Septemba 30, 2022 na Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), rushwa ya ngono dhidi ya waandishi wa habari wanawake ni janga kubwa linalokwamisha tasnia.
 
Ripoti inasema wanaotuhumiwa zaidi katika rushwa hiyo ni wahariri na maofisa rasilimaliwatu wakifuatiwa na meneja, wakurugenzi, wamiliki pamoja na vyanzo vya habari. 
 
UKIMYA KIKWAZO KIKUBWA
 
Kwa mujibu wa utafiti huu uliofanywa mkoani Dar es Salaam, asilimia 52 ya wanawake hawapo tayari kuweka wazi adha ya rushwa ya ngono wanayoyapata kazini.
 
Wadau wengi wanasema. licha ya kuwepo sera na miongozo ya kijinsia kwa baadhi ya vyombo vya habari, hakuna uzingatiwaji wala utekelezwaji sera hizo.
 
 
Utafiti uliofanywa na Asasi ya Wanawake katika Habari Afrika (WAN-IFRA) mwaka 2020/21 nao ulibaini kuwa, asilimia 41 ya wanawake wanahabari waliwahi kufanyiwa unyanyasaji wa kingono wakiwa kwenye maeneo ya kazi.
 
Kwamba, asilimia 74.5 ya wanahabari wanawake hawakuweka wazi kuhusu manyanyaso au kero ya rushwa ya ngono wanayokumbana nayo.
 
Mhariri Mkuu wa Vipindi,  Afya radio Ester Baraka anasema: 
“Wanawake tumeumbiwa weledi mkubwa katika kazi, tumeumbiwa kujituma na kufanya kazi kwa mapenzi yote sasa inapokuja madhila hayo ni wepesi sana kukumbwa na mawazo na kuathirika kisaikolojia kwani hujikuta tukitafakari sana namna ya kulikwepa suala hilo.” 
 
 
Naye Mratibu wa Gazeti la HabariLEO Afrika Mashariki, Joseph Sabinus anasema: “Rushwa ya ngono ipo kwa kuwa kwa wanaume wengi katika vyombo vya uamuzi kuliko wanawake na si wahariri pekee, ingawa si wanaune wote wenye kasumba hiyo....”
 
Anasema: “Waathirka wengi wa rushwa ya ngono wanahofia kutoa taarifa kwa kuhisi kwamba mhusika akichukuliwa hatua za haki kali, umma utamgeukia na kumsuta kuwa anafukuzisha watu kazi, hivyo atajidhalilisha na watu watamchukia.”
 
Meneja wa kituo cha redio cha Safari FM, Ashraf Mohamed, anasema tatizo la rushwa ya ngono halikomi kwa kuwa wapo baadhi ya wanahabari wanawake wanaojirahisisha na kutaka kufanya chochote ili wapate kazi.
 
Anasema kutokukoma kwa tatizo hili kunachochewa pia utandawazi unaofanya baadhi ya watu kudhani kuwa, rushwa ya ngono ni kitu cha kawaida kwa kuwa hufanyika kwa siri na kumfanya hata mtu asiye na sifa kupata kazi kirahisi.
 
MATOKEO
Katika utafiti wa TAMWA, Dk Rose anasema: “Tuligundua tatizo hilo lipo na limesababisha baadhi ya wanahabari kufukuzwa kazi, kuacha kazi na wengine wameweza kupingana na kuhimili japokuwa hawana furaha katika kazi hiyo na wengne hawakusema.”
 
Anasema kati ya asilimia 65-84 ya waandishi wa habari walisema tatizo lipo huku watuhumiwa wengi wakiwa ni wahariri wa habari ambao wana mamlaka ya kuamua habari ipi na ya nani itangazwe au ipi ichapishwe.
 
Rose anabainisha makundi yanayoathirika zaidi na rushwa ya ngono kuwa ni wanafunzi walio katika mafunzo kwa vitendo, wandishi wa mikoani na wale wanaotuma habari zao wakiwa hawajaajiriwa maarufu ‘correspondents’.
 
Utafiti uliofanywa na WFT-T kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mwaka 2020 ulibaini kuwa, udhaifu upo katika mfumo wa udhibiti wa rushwa ya ngono kazini huku asilimia 10.7 hadi 38.2 ya watu waliohojiwa wakikubali kuwepo kwa sera, miongozo na taratibu za udhibiti wa rushwa ya ngono. Zaidi ya asilimia 60 hawakufahamu kuwapo kwa mambo hayo.
 
MADHARA YA RUSHWA YA NGONO
 
“Hii ndio sababu wanafunzi wengi wanasoma uandishi wa habari, lakini ni wachache sana wanaoonekana katika vyombo vya habari na upande wa wandishi wa kujitegemea, tukagundua taarifa zao nyingi hazitumiki kwa sababu ya rushwa hiyo,” alisema Dk Rose. 
 
Kwa mujibu wa WAN-IFRA, udhalilishaji wa kingono kwa wanahabari wanawake umewafanya wengi wasioweza kupambana kuamua kuikimbia tasnia ya habari na kupoteza vipaji lukuki.
 
Ripoti inasema: “Ni asilimia 21 tu ya wanahabari wanawake wanaopaza sauti zao pindi wanapofanyiwa ukatili huu.”
 
Naye mkongwe katika tasnia ya habari, Rose Haji anasema: “Kama msichana atakuwa mwoga na asijue kujilinda, ‘atachezewa’ na ofisi nzima na hata kama ana uwezo mkubwa, watamuona si kitu jambo ambalo ni hatari.”
 
“Ukimkubali mwanaume tabu, ukimkataa ndio mara mbili, unapomkataa hasa kiongozi hapo ndipo anakuwekea chuki na kukusingizia mambo mengi, mara hujui kutafuta habari, mvivu hujui kuandika, na visingizo vingi ambavyo vitashusha hadhi yako ya utendaji kazi,” anasema Rose. 
 
Katika mkutano ulioandaliwa na TAMWA jijini Arusha, mei 5, 2022 Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alinukuliwa akisema: “Wanahabari wanawake wanapungua katika tasnia ya habari nchini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo mazingira yasiyo rafiki, ni wakati sasa wa kuwatia moyo wachache waliopo na kuwapongeza ili wasiondoke katika tasnia." 
 
Mkurugenzi wa Programu katika Shirika la Utu wa Mtu Tanzania ambaye pia ni mwanasaikolojia, Harrieth Baagae, anasema: “Rushwa ya ngono husababisha msongo wa mawazo na mwanamke kuchukia wanaume na kuweka kisasi kutokana na hasira ya umda mrefu.”
Anasema hii ni kwa kuwa mwathirika huendelea kufanya kazi na kukutana na aliyemfanyia kitendo na anapokumbuka, hasira na maumivu ya kiakili humrudia japo hasemi na hali hiyo, hushusha ufanisi katika kazi. 
 
Kwa mujibu wa Harrieth, mwathirika wa rushwa ya ngono hutibika kwa ushauri wa kisaikolojia wa muda mrefu ili kujengeka kiimani na kujikubali kuwa alikoseakukubali kutoa rushwa hiyo.
KANUNI ZA KIMAADILI
Miongoni mwa kanuni za kimaadili zilizotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa waandishi wa habari ni pamoja na kuheshimu utu na hadhi ya mtu kwa kulinda mambo yote yanayohusu hadhi ya mtu, kuzuia rushwa ya ngono, unyanyasaji, udhalilishaji wa kijinsia, kiumri na udhaifu wa changamoto ya maumbile ukiwemo ulemavu. 
SHERIA DHIDI YA RUSHWA YA NGONO
Kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya Mwaka 2007, rushwa ya ngono ni kitendo anachofanya mtu mwenye mamlaka, katika kutekeleza matakwa yake ya kudai ngono kwa mtu kama kishawishi cha kumpatia huyo mtu ajira, cheo, haki, fursa au upendeleo mwingine. 
 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa TAKUKURU, Joseph Kasongo hiyo inatoa ulinzi kwa mtoa taarifa na mtu yeyote anayebainika kutenda kosa hilo, anaweza kupata ya adhabu ya faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka mitatu.
Kasongo anasema: “Kutokana na utafiti tulioufanya na WFT mwaka 2020, vyuo vikuu vimeanzisha madawati ya kijinsia, kamati za kinidhamu na maadili, na  TAKUKURU tuimeimarisha klabu za wapinga rushwa katika vyuo ili wawe na mamlaka ya kuhoji vitendo hivyo vinapotokea…”
 
SULUHISHO DHIDI YA JANGA
 
Vyanzo mbalimbali vinasisitiza wandishi wa habari wajengewe uwezo kufichua uhalifu huo na wahusika wachukuliwe hatua kali za kimaadili na kisheria.
Sabinus anasema: “Vyombo vya habari na taasisi ziwe na sera zinazofahamika na zilizo wazi kuhusu masuala ya usawa wa kijinsia na hususan zikitaja nini kinapaswa kufanyika, nini hatua zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya anayeoomba au kudai na pia, kuwepo mazingira salama kwa waathirka wanaotoa taarifa kuhusu matukio hayo….” 
 
Anaongeza: “Kuwe na uwiano wa wanawake na wanaume wanaotoa uamuzi katika vyombo vya habari na pia, kuwe na madawati ya jinsia yenye weledi ili iwe rahisi kwa mtu kuelezea tatizo lake ili pia lishughulikiwe kwa siri.”
 
Dk Rose yeye anasema: “TAMWA tunaamini ni wakati sasa wa kuanzisha kamati ama kitengo maalumu kushughulikia masuala ya rushwa ya ngono katika vyombo vya habari ili kuwashauri wanahabari wanawake waliokumbwa na majanga haya pamoja na kufundishwa mbinu mbalimbali za kukabili tatizo hili.”

Search