News/Stories

SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

MAADHIMISHO YA MIAKA 30 YA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI

 

Golden Tulip Airport Hotel Zanzibar

01-MAY, 2023

Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Tabia Mwita Maulid.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Mheshimiwa Fatma Hamad

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Tanzania Bara Gerson Msigwa,

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Hassan Khatib Hassan

Waheshimiwa Mabalozi na Wadau wa Maendeleo mliopo hapa leo,

Ndugu Waandishi wa Habari wenzangu

Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…..KAZI IENDENELEE

Awali ya yote nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha siku ya leo, siku ambayo ni muhimu, sio tu kwa sekta ya habari bali kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu. Kwa sababu kama kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inavyosema ““Kuunda Mustakabali wa Haki: Uhuru wa kujieleza kama kichocheo cha haki nyingine zote za binadamu” hivyo hatuna budi kutafakari namna ambayo tunahamasisha kuendelea kuwepo kwa uhuru wa kujieleza.

Ikiwa ni miaka 30 tangu tuanze maadhimisho haya ni muda muafaka kwetu sote kutafakari hali ya uhuru wa kujieleza na ya vyombo vya habari ili tupate suluhu ambazo zitakua chachu kuhakikisha kwamba jamii ya Tanzania ni jamii yenye fursa ya kujieleza hususani katika kudai haki.

Sote tunatambua na kuthamini kwamba, hali ya uhuru wa habari nchini Tanzania kwa kiwango chake inaridhisha na tunaziona jitihada zinazofanyika kuiboresha zaidi. Hivyo tutumie siku tatu hizi kutafakari na kujadiliana mambo ambayo yatatuvusha kutoka hapa tulipo na kuelekea fursa nzuri zaidi ambayo uhuru wa uhariri, uhuru wa kutafuta habari, uhuru wa kuhoji na uhuru wa kujieleza linakuwa  suala ambalo kila mtanzania anapaswa kujivunia.

Pamoja na kuthamini hali ilivyo sasa, tutumie jukwaa hili kuzizungumza kwa undani changamoto ambazo bado ni kero katika sekta ya habari. Changamoto hizo ni pamoja na hali ngumu ya uchumi ya vyombo vya habari ambayo yamepelekea waandishi kufanya kazi kwa ugumu, usalama na ulinzi kwa wanahabari.

Tumeona pia kuwa mchakato wa kurekebisha sheria za habari unachukua muda mrefu jambo ambalo tunahoji, sababu ni nini?

Changamoto nyingine ni masuala ya usawa wa kijinsia kwenye vyombo vyetu vya habari. Ni kweli usiopingika kwamba wanawake katika sekta ya habari wamekuwa wakiongezeka katika kipindi hichi cha miaka 30. Lakini bado nafasi za uongozi katika menejimenti, uhariri na nyanja za siasa bado uwakilishi ni mdogo.

Sauti  zao pia zimekuwa hazisikiki katika vyombo vya habari jambo ambalo linaondoa fursa la wanawake kutoa mawazo yao kuhusu masuala yanayowahusu. Hali kadhalika vyombo vya habari vimekuwa havitendi haki pale vinapoandika taarifa za jinsia. 

Pamoja na kudai uhuru wa vyombo vya habari lakini tukumbuke kwamba hakuna uhuru usio na mipaka. Waandishi wa habari wanapaswa kuzingatia misingi ya taaluma na maadili  na pia kujali faragha za watu wakati wakitimiza wajibu wao wa uandishi wa habari .

Tusipende kulaumu mamlaka husika pale tunapo kumbushwa kutekeleza majukumu yetu ya kila siku. Tukumbuke kwamba tunalo jukumu la kulinda Utanzania wetu kwa kuandika habari zenye kuhamasisha utamaduni wetu na kuchagiza maendeleo kwa kuzingatia maadili na taaluma.

Nitoe shukrani kwa serikali kwa namna ambayo imeendelea kushirikiana na vyombo vya habari, lakini pia kuwashukuru wadau wa maendeleo ambao wamekuwa wakiunga mkono sekta ya habari, bila kuwasahau wadhamini wa maadhimisho haya pamoja na kamati nzima ya maandalizi.

Kwa hayo machache, niwakaribishe katika mjadala utakaotujenga kimaadili, kiuweledi, na kitaaluma katika kuyaendeleza majukumu yetu ya kila siku.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Joyce Shebe

Mwenyekiti Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania – TAMWA.

Latest News and Stories

Search