News/Stories

Makubwa yanayokwamisha vita kukabili rushwa ya ngono

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Na Edina Salila
Rushwa ya ngono ni tatizo linalowatesa watu wengi hasa wanawake na wasichana kazini na katika taasisi za elimu yaani vyuo na vyuo vikuu.
Chanzo kikuu cha rushwa hiyo kinatajwa kuwa ni mmomonyoko wa maadili na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya wahadhiri na viongozi na watumishi katika maeneo ya kazi.
Ingawa rushwa hii huwaathiri zaidi wanawake, kumekuwapo madai kutoka kwa watu na vyanzo mbalimbali kuwa, baadhi ya wasichana wamekuwa kichocheo na ushawishi kwa wahusika ili wapate upendeleo kwa malipo ya ngono.
Katika moja ya semina za hivi karibuni zilizoandaliwa na Tamwa kwa wahariri na wandishi wa habari Dar es Salaam, washiriki walisema kutokana na uwezo mdogo kimasomo, baadhi ya wanafunzi wa kike wanajenga mazoea ‘yanayovuka mipaka’ kwa wakufunzi na wahadhiri wa kiume ili wapewe upendeleo wa alama za juu katika mitihani.
Utafiti uliofanywa na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT- T) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mwaka 2020 katika baadhi ya vyuo vikuu nchini, ulibaini kuwa, zaidi ya asilimia 50 ya waliohojiwa walieleza kuwepo kwa rushwa ya ngono vyuoni.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa TAKUKURU, Joseph Mwaiselo, anasema kutokana na kuwapo rushwa ya ngono, mwaka 2007 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na katika sheria hiyo, kiliwekwa Kifungu cha 25 ili kuharamisha rushwa ya ngono.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, ni kosa kwa mtu mwenye mamlaka kutoa sharti lolote la kutaka rushwa ya ngono katika ili kutoa huduma husika.
“Tuligundua kuna rushwa ya ngono katika vyuo vikuu na kwamba, wapo wanaotumia mamlaka yao vibaya kwa kudai rushwa ya ngono, lakini pia wapo wanafunzi wanaowashawishi wahadhiri ili wapewe alama za kuwafanya wafaulu mitihani,” alisema.
Kwa mujibu wa utafiti huo, mifumo dhaifu na isiyo rafiki kwa waathirika kutoa taarifa na kushughulikia tatizo hilo, ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha mafanikio katika vita dhidi ya rushwa ya ngono.
Mkaguzi wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia Wilaya ya Ubungo, Evetha John, anasema: “Tumeshapokea kesi za wanafunzi wa vyuo wakilalamikia rushwa ya ngono, lakini kwa sababu tunashirikiana na taasisi nyingine husika ikiwemo Takukuru; waathirika tunawaunganisha na maofisa wa Takukuru ili kupata usaidizi zaidi wa kisheria.”
Mkufunzi wa Masuala ya Mawasiliano ya Jamii, Mary Kafyome, anasema kikwazo kingine katika mafanikio dhidi ya tatizo hilo, ni taasisi nyingine zikiwamo za elimu ya juu kutokuwa na sera zilizo wazi kuhusu masuala ya usawa wa kijinsia.
“Baadhi ya vyuo vikuu havina sera za kuzuia ukatili wa kingono na usawa wa kijinsia, hivyo ni ngumu kuzuia vitendo hivyo vyuoni, lakini pia vyuo vingine tumeona sera wanazo lakini hazijulikani kwa wafanyakazi na wanafunzi, hii huchangia kushamiri kwa vitendo hivyo,'' anasema Kafyome.
Kwa mujibu wa uchunguzi, ukimya wa wanawake wengi katika jambo hili hufanya lisisikike huku waathirika wengine wakiamini kuwa, wakifichua uovu huo, jamii itawanyanyapaa.
“Waathirika wengi wanahofia kusema kwa sababu hawana uhakika wa kupata haki yao na kuhofia mtuhumiwa kusikilizwa zaidi kuliko wao,” anasema Kafyome.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliyeomba jina lake lisitajwe anasema: “Wasichana tunateseka sana na hili tatizo maana sasa kiwango cha juu cha alama ndio dili na si elimu yenyewe… Ndio maana wengine hutumbukia katika huo mtego kwani hata wahadhiri wenyewe wanajali maksi na si elimu hali inayosababisha rushwa hii kuonekana jambo la kawaida vyuoni.”
Anaongeza: “Nashauri tupewe mbinu za kuripoti matukio haya."
Naye Anna Hangwa, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini (TUDARCo) kilichopo Dar es Salaam, anasema: “Tunatakiwa kujithamini, kuwajibika… Mwalimu akitaka kukurudisha nyuma kimasomo, kama umewajibika na kusoma ipasavyo utakuwa na uhakika wa ufaulu wako."
Wadau mbalimbali wa usawa wa kijinsia wanashauri kuwapo madawati ya kjinsia yaliyo rafiki zaidi kwa wanafunzi kuripoti matukio ya unyanyasaji yanayofanyika vyuoni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk Rose Reuben, anasema: “Ni wakati sasa wa madawati ya kijinsia kuwa hai katika kila upande.”

Latest News and Stories

Search