News/Stories

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
Na Edina Salila
 
“Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikifanya kazi katika mazingira magumu sana huku nikikumbana na majaribu na matokeo yake, nimekuwa mtu wa bosi wangu kukejeli na kukashfu ili nionekane sijui kutafuta wala kuandika stori (habari) kisa, eti nimemkatalia bosi wangu kimapenzi…”
 
“Kinachoniumiza zaidi ni kuwa, licha ya kuwashirikisha wenzangu, nimeushirikisha uongozi ili kukomesha hali hii ambayo ni tatizo kubwa kwangu, lakini sijashirikishwa wala kuona mabadiliko au hatua zozote zikichukuliwa.”
 
Ndivyo anavyosema Kemmy Mang’ombe (si jina halisi), mmoja wa wandishi wa habari wanawake katika gazeti moja la kibinafsi litolewalo kwa Kiswahili kila siku nchini.
 
Kemmy ambaye ni kiwakilisha cha wandishi wa habari wengi wa kike waliopitia madhira hayo anasema, baada ya kuzidiwa na adha huku akisaka ufumbuzi kwa wandishi wenzake wa kike, alibaini kuwa, wengi walikuwa wakimshangaa kwa kuwa nao, wamekumbwa na madhira hayo; wakalegea na kutumbukia kwenye janga la rushwa ya ngono na wakubwa wao wa kazi.
 
Kwa mujibu wa uchunguzi, miongoni mwa hoja zinazotumiwa na watu wanaodai rushwa hii ambayo kwa kiasi kikubwa huwaathiri vibaya wandishi wa habari wa kike, ni ahadi za kuajiriwa hasa kwa wandishi wa kike ambao hawajaajiriwa, ahadi za kuongezwa vyeo na mshahara (kwa waajiriwa), upendeleo wa kupewa safari na kazi kubwa na msaada wa ziada kuhakikisha kazi (stori) za mlengwa zinatoka.
 
Kwa mujibu wa Kemmy, baada ya kumkatalia mhariri wake, mara kadhaa anapowasilisha habari zake kwa mhariri hasa kubwa, huambulia kejeli kuwa hajui kuandika na kutakiwa kutafuta nyingine.
 
“Cha ajabu, kwa kuwa mimi ni correspondent, ninalipwa kadiri ya kazi zangu zinazotoka, anapozikataa nikaamua kupeleka magazeti mengine, zinatoka na mara tatu zimetoka ukurasa wa mbele na nyingine mbili zikawa ‘lead’ (habari kuu katika gazeti).”
 
“Sasa ndipo ujiulize, huku wanasema sijui kuandika, magazeti mengine, habari hiyohiyo inakuwa kuu; tena magazeti yenye heshima maana stori zinajitosheleza,” anasema.
 
Anaongeza: “Kinachosikitisha, huko kwingine baada ya kuona stori zinatoka nikataka kuhamia huko, nikakumbana na yale yale; nikaangukia kwa bosi mmoja anayesisitiza kutaka nihusiane naye kingono eti stori zangu zitakuwa zinatoka kila siku… Kwa kweli, nikaona kama mambo ni haya, uandishi umenishinda; ngoja nikauze maandazi…”
 
Mwaka 2021, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania, (WFT-T) kupitia mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari, walifanya utafiti uliothibitisha kuwapo vitendo vya rushwa ya ngono na udhalilishaji mwingine wa kijinsia katika vyombo vya habari ukiwamo wa kimwili na maneno. 
 
Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara ya Mwaka 2021/2022 iliyozinduliwa Septemba 30, 2022 na Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), rushwa ya ngono dhidi ya waandishi wa habari wanawake ni janga kubwa linalokwamisha tasnia.
 
Ripoti inasema wanaotuhumiwa zaidi katika rushwa hiyo ni wahariri na maofisa rasilimaliwatu wakifuatiwa na meneja, wakurugenzi, wamiliki pamoja na vyanzo vya habari. 
 
UKIMYA KIKWAZO KIKUBWA
 
Kwa mujibu wa utafiti huu uliofanywa mkoani Dar es Salaam, asilimia 52 ya wanawake hawapo tayari kuweka wazi adha ya rushwa ya ngono wanayoyapata kazini.
 
Wadau wengi wanasema. licha ya kuwepo sera na miongozo ya kijinsia kwa baadhi ya vyombo vya habari, hakuna uzingatiwaji wala utekelezwaji sera hizo.
 
 
Utafiti uliofanywa na Asasi ya Wanawake katika Habari Afrika (WAN-IFRA) mwaka 2020/21 nao ulibaini kuwa, asilimia 41 ya wanawake wanahabari waliwahi kufanyiwa unyanyasaji wa kingono wakiwa kwenye maeneo ya kazi.
 
Kwamba, asilimia 74.5 ya wanahabari wanawake hawakuweka wazi kuhusu manyanyaso au kero ya rushwa ya ngono wanayokumbana nayo.
 
Mhariri Mkuu wa Vipindi,  Afya radio Ester Baraka anasema: 
“Wanawake tumeumbiwa weledi mkubwa katika kazi, tumeumbiwa kujituma na kufanya kazi kwa mapenzi yote sasa inapokuja madhila hayo ni wepesi sana kukumbwa na mawazo na kuathirika kisaikolojia kwani hujikuta tukitafakari sana namna ya kulikwepa suala hilo.” 
 
 
Naye Mratibu wa Gazeti la HabariLEO Afrika Mashariki, Joseph Sabinus anasema: “Rushwa ya ngono ipo kwa kuwa kwa wanaume wengi katika vyombo vya uamuzi kuliko wanawake na si wahariri pekee, ingawa si wanaune wote wenye kasumba hiyo....”
 
Anasema: “Waathirka wengi wa rushwa ya ngono wanahofia kutoa taarifa kwa kuhisi kwamba mhusika akichukuliwa hatua za haki kali, umma utamgeukia na kumsuta kuwa anafukuzisha watu kazi, hivyo atajidhalilisha na watu watamchukia.”
 
Meneja wa kituo cha redio cha Safari FM, Ashraf Mohamed, anasema tatizo la rushwa ya ngono halikomi kwa kuwa wapo baadhi ya wanahabari wanawake wanaojirahisisha na kutaka kufanya chochote ili wapate kazi.
 
Anasema kutokukoma kwa tatizo hili kunachochewa pia utandawazi unaofanya baadhi ya watu kudhani kuwa, rushwa ya ngono ni kitu cha kawaida kwa kuwa hufanyika kwa siri na kumfanya hata mtu asiye na sifa kupata kazi kirahisi.
 
MATOKEO
Katika utafiti wa TAMWA, Dk Rose anasema: “Tuligundua tatizo hilo lipo na limesababisha baadhi ya wanahabari kufukuzwa kazi, kuacha kazi na wengine wameweza kupingana na kuhimili japokuwa hawana furaha katika kazi hiyo na wengne hawakusema.”
 
Anasema kati ya asilimia 65-84 ya waandishi wa habari walisema tatizo lipo huku watuhumiwa wengi wakiwa ni wahariri wa habari ambao wana mamlaka ya kuamua habari ipi na ya nani itangazwe au ipi ichapishwe.
 
Rose anabainisha makundi yanayoathirika zaidi na rushwa ya ngono kuwa ni wanafunzi walio katika mafunzo kwa vitendo, wandishi wa mikoani na wale wanaotuma habari zao wakiwa hawajaajiriwa maarufu ‘correspondents’.
 
Utafiti uliofanywa na WFT-T kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mwaka 2020 ulibaini kuwa, udhaifu upo katika mfumo wa udhibiti wa rushwa ya ngono kazini huku asilimia 10.7 hadi 38.2 ya watu waliohojiwa wakikubali kuwepo kwa sera, miongozo na taratibu za udhibiti wa rushwa ya ngono. Zaidi ya asilimia 60 hawakufahamu kuwapo kwa mambo hayo.
 
MADHARA YA RUSHWA YA NGONO
 
“Hii ndio sababu wanafunzi wengi wanasoma uandishi wa habari, lakini ni wachache sana wanaoonekana katika vyombo vya habari na upande wa wandishi wa kujitegemea, tukagundua taarifa zao nyingi hazitumiki kwa sababu ya rushwa hiyo,” alisema Dk Rose. 
 
Kwa mujibu wa WAN-IFRA, udhalilishaji wa kingono kwa wanahabari wanawake umewafanya wengi wasioweza kupambana kuamua kuikimbia tasnia ya habari na kupoteza vipaji lukuki.
 
Ripoti inasema: “Ni asilimia 21 tu ya wanahabari wanawake wanaopaza sauti zao pindi wanapofanyiwa ukatili huu.”
 
Naye mkongwe katika tasnia ya habari, Rose Haji anasema: “Kama msichana atakuwa mwoga na asijue kujilinda, ‘atachezewa’ na ofisi nzima na hata kama ana uwezo mkubwa, watamuona si kitu jambo ambalo ni hatari.”
 
“Ukimkubali mwanaume tabu, ukimkataa ndio mara mbili, unapomkataa hasa kiongozi hapo ndipo anakuwekea chuki na kukusingizia mambo mengi, mara hujui kutafuta habari, mvivu hujui kuandika, na visingizo vingi ambavyo vitashusha hadhi yako ya utendaji kazi,” anasema Rose. 
 
Katika mkutano ulioandaliwa na TAMWA jijini Arusha, mei 5, 2022 Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alinukuliwa akisema: “Wanahabari wanawake wanapungua katika tasnia ya habari nchini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo mazingira yasiyo rafiki, ni wakati sasa wa kuwatia moyo wachache waliopo na kuwapongeza ili wasiondoke katika tasnia." 
 
Mkurugenzi wa Programu katika Shirika la Utu wa Mtu Tanzania ambaye pia ni mwanasaikolojia, Harrieth Baagae, anasema: “Rushwa ya ngono husababisha msongo wa mawazo na mwanamke kuchukia wanaume na kuweka kisasi kutokana na hasira ya umda mrefu.”
Anasema hii ni kwa kuwa mwathirika huendelea kufanya kazi na kukutana na aliyemfanyia kitendo na anapokumbuka, hasira na maumivu ya kiakili humrudia japo hasemi na hali hiyo, hushusha ufanisi katika kazi. 
 
Kwa mujibu wa Harrieth, mwathirika wa rushwa ya ngono hutibika kwa ushauri wa kisaikolojia wa muda mrefu ili kujengeka kiimani na kujikubali kuwa alikoseakukubali kutoa rushwa hiyo.
KANUNI ZA KIMAADILI
Miongoni mwa kanuni za kimaadili zilizotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa waandishi wa habari ni pamoja na kuheshimu utu na hadhi ya mtu kwa kulinda mambo yote yanayohusu hadhi ya mtu, kuzuia rushwa ya ngono, unyanyasaji, udhalilishaji wa kijinsia, kiumri na udhaifu wa changamoto ya maumbile ukiwemo ulemavu. 
SHERIA DHIDI YA RUSHWA YA NGONO
Kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya Mwaka 2007, rushwa ya ngono ni kitendo anachofanya mtu mwenye mamlaka, katika kutekeleza matakwa yake ya kudai ngono kwa mtu kama kishawishi cha kumpatia huyo mtu ajira, cheo, haki, fursa au upendeleo mwingine. 
 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa TAKUKURU, Joseph Kasongo hiyo inatoa ulinzi kwa mtoa taarifa na mtu yeyote anayebainika kutenda kosa hilo, anaweza kupata ya adhabu ya faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka mitatu.
Kasongo anasema: “Kutokana na utafiti tulioufanya na WFT mwaka 2020, vyuo vikuu vimeanzisha madawati ya kijinsia, kamati za kinidhamu na maadili, na  TAKUKURU tuimeimarisha klabu za wapinga rushwa katika vyuo ili wawe na mamlaka ya kuhoji vitendo hivyo vinapotokea…”
 
SULUHISHO DHIDI YA JANGA
 
Vyanzo mbalimbali vinasisitiza wandishi wa habari wajengewe uwezo kufichua uhalifu huo na wahusika wachukuliwe hatua kali za kimaadili na kisheria.
Sabinus anasema: “Vyombo vya habari na taasisi ziwe na sera zinazofahamika na zilizo wazi kuhusu masuala ya usawa wa kijinsia na hususan zikitaja nini kinapaswa kufanyika, nini hatua zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya anayeoomba au kudai na pia, kuwepo mazingira salama kwa waathirka wanaotoa taarifa kuhusu matukio hayo….” 
 
Anaongeza: “Kuwe na uwiano wa wanawake na wanaume wanaotoa uamuzi katika vyombo vya habari na pia, kuwe na madawati ya jinsia yenye weledi ili iwe rahisi kwa mtu kuelezea tatizo lake ili pia lishughulikiwe kwa siri.”
 
Dk Rose yeye anasema: “TAMWA tunaamini ni wakati sasa wa kuanzisha kamati ama kitengo maalumu kushughulikia masuala ya rushwa ya ngono katika vyombo vya habari ili kuwashauri wanahabari wanawake waliokumbwa na majanga haya pamoja na kufundishwa mbinu mbalimbali za kukabili tatizo hili.”

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) leo Agosti 27, kimefanya uchaguzi wake Mkuu wa mwaka na kumchagua Joyce Shebe kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
 
Shebe ambaye ni Mhariri Mkuu wa Clouds Media Group, ataongoza kwa miaka mitatu. Huu ni muhula wa pili kwa Shebe baada ya kuongoza miaka mitatu ya mwanzo kuanzia 2019. Katika uchaguzi huo, Shebe alikuwa akichuana na Mwasisi wa TAMWA, Lyela Sheikh.
 
Nafasi nyingine katika uchaguzi huo ni wajumbe wa bodi, ambapo Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Tumaini, Mary Kafyome, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha St Augustine, Dk Kaanaeli Kaale nao walichaguliwa kuwa wajumbe wa bodi ya Tamwa.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Sekretarieti ya Chama cha Wanahabri Wanawake Tanzania – TAMWA, inapenda kuwakumbusha wanachama wake kuwa mkutano mkuu wa Chama kwa mwaka 2022, utahusisha uchaguzi wa wajumbe wa Bodi, hivyo tunawahimiza wanachama wanaowiwa kuwania nafasi hizo kutuma maombi yao mapema kupitia barua pepe This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. Cc: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Fomu za maombi zinapatikana katika tovuti ya Chama www.tamwa.org

Mwisho wa kutuma maombi ni Machi 11, 2022.

Kelvin Mtewele - Afisa Utawala, TAMWA.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinapenda kukanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha kuwa tumelishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wa kumchukulia hatua Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima.

Pia taarifa hizo zimekwenda mbali zaidi zikionyesha TAMWA imemtaka Askofu Gwajima kumuomba radhi Rais Samia  Suluhu na Waziri wa Afya, Doroth Gwajima kwa niaba ya wanawake wote nchini.

Tunapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa taarifa hizo ambazo zimewekwa katika nembo za vyombo vya habari kama ITV, AYO TV na katika tamko linaloonyesha kusainiwa na Mkurugenzi wa TAMWA Dkt. Rose Reuben, si za kweli. 

TAMWA haijafanya mkutano wa kihabari, haijatoa tamko wala kuzungumza na chombo chochote cha habari kuhusu sakata la Askofu Gwajima na Bunge. 

TAMWA inafanya kazi kwa kufuata maadili na taratibu za kiuandishi  na ina taratibu  zake pindi inapotakiwa kuzungumzia masuala ya jinsia, habari na afya.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Machi 18, 2021. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
 
TAMWA inaungana na watanzania wote kuomboleza kifo cha kiongozi  huyo mahiri, Rais John Pombe Magufuli. 
Kwa niaba ya wanachama wa TAMWA, bodi ya TAMWA, Wanahabari, Wanawake, na wapigania haki za jinsia, tunatoa pole kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu,  familia ya Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli viongozi wa serikali na watanzania wote kwa kumpoteza kiongozi wa nchi. 
 
TAMWA inaomboleza msiba huu kwa kukumbuka mafanikio yaliyofanywa na Rais Magufuli katika kipindi cha uongozi wake tangu mwaka 2015. 
 
Rais Magufuli alikuwa na juhudi katika kujenga miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa ilisaidia kumkomboa mwanamke kuanzia ngazi za chini. 
Miundombinu aliyojenga kuanzia ya maji, barabara na mingineyo, ilikuwa inalenga kumkomboa mwanamke, kumtua mama ndoo kichwani na kumsaidia mjasiriamalia mwanamke kufanya shughuli zake kwa umakini na ufasaha, 
Aliwahi kusema kuwa, katika wizara inayomnyima raha  ni wizara ya maji, na hivyo akaamua kuimairisha eneo hilo ili kuhakikisha adha ya maji inatoweka. Kwa kufanya hivyo alimsaidia sana mwanamke wa kijijini na mjini, mwanamke na mtoto wa kike, kwa sababu ukosefu wa maji ulichangia kwa kiasi kikubwa ukatili wa kijinsia, ukosefu wa masomo na ufinyu wa kipato. 
 
Rais Magufuli alikuwa akijipambanua kuwa rais wa wanyonge na kweli alijitahidi kuimarisha miundombinu ya maji, umeme na kuwatazama wajane waliodhulumiwa kwa namna moja au nyingine, kuondoa riba kwa mikopo ya wanawake ya Halmashauri. 
 
TAMWA tulitamani Rais Magufuli, akamilishe kipindi chake  cha uongozi ili Watanzania tupate hasa kile alichodhamiria kukamilisha, kwa sababu alikuwa na maono makubwa.
TAMWA itamkumbuka Rais Magufuli kwa kuwa rais wa kwanza kumteua mwanamke kuwa Makamu wa Rais. 
Kwa hili aliweka historia nchini, ya kuwepo Makamu wa kwanza wa Rais mwanamke, hata kama hatujaifikia ile asilimia 50 kwa 50 ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, 
 
Rais Magufuli atakumbukwa kama kiongozi aliyekuwa anatamani kuwakomboa wananachi kwa ujumla na sio kuwepo kwa mafanikio ya mtu mmoja mmoja. 
 
Mungu ailaze roho ya Hayati John Pombe Magufuli Mahali pema Amina!
 
Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji 
TAMWA.

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinawatangazia wanahabari wanawake wenye uwezo wa kufanya habari za uchunguzi, kuwasilisha maombi kupitia barua pepe ya TAMWA This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. Mwombaji anatakiwa  kuambatanisha habari mbili za uchunguzi zilizowahi  kuchapishwa/kurushwa  katika chombo cha habari kinachotambulika. 
Habari hizo ni sehemu ya mradi wa Wanawake katika Vyombo vya habari, unaolenga kuwajengea uwezo wa wanahabari wa kike kupambana na ukatili wa kijinsia, ikiwamo rushwa ya ngono, haki sawa ndani ya vyumba vya habari na ufinyu wa maslahi kwa wanahabari wa kike ndani ya taasisi za habari. 
Mwisho wa kutuma maombi hayo, ni Machi 22, 2021 saa 6 kamili usiku.

Latest News and Stories

Search