News/Stories

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI MH GEORGE SIMBACHAWENE KATIKA KONGAMANO LA USALAMA BARABARANI LILILOANDALIWA NA TAMWA

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
 

MUUNGANO WA ASASI ZA KIRAIA ZINAZOSHAWISHI MABORESHO YA SHERIA YA USALAMA BARABARANI

 

TAREHE: 23 MEI 2020

 

UKUMBI: PIUS MSEKWA DODOMA

 

KONGAMANO LA USALAMA BARABARANI

 

Ndugu Waheshimiwa Wabunge;

Ndugu wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani Ya Nchi;

Ndugu wawakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto;

Ndugu Wakurugenzi Asasi za Kiraia zinazoshawishi Maboresho ya Sheria ya Usalama Barabarani;

Ndugu Waandishi wa habari na wadau wote wa Usalama Barabarani, Mabibi na Mabwana;

Ndugu Waandaaji wa hafla hii Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mwananchi Communication; - Habari za asubuhi.

 

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo kuhudhuria Kongamano hili. Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa taasisi ya zilizo shiriki kuandaa kongamano hili kuanzia wafadhaili, Wabunge, Mwananchi Communications, na Asasi zote za kiraia zinazoshawishi maboresho ya sharia ya usalama barabarani. Aidha, ninawashukuru kwa kunialika kuwa Mgeni rasmi katika kongamano hili muhimu kwa usalama wa watumiaji wa barabara nchini Tanzania. Hakuna shaka kongamano hili ni ishara ya juhudi zinazofanyika katika kuhakikisha suala la usalama barabarani linatiliwa mkazo.

Ndugu Washiriki

Kipekee pia Namshukuru Mh Raisi Dkt John Pombe Magufuli kwa kuniteua kusimamia Wizara hii yenye changamoto mbalimbali Ikiwemo changamoto ya Ajali za barabarani. Ninatambua kwamba changamoto hii ni kubwa lakini nipo tayari kuikabili kwa kutumia uwezo wangu na kwa kushirikiana nanyi nyote.

Ndugu Washiriki

Naomba pia kutumia fursa hii kuwashukuru waheshimiwa Wabunge, Wanahabari pamoja na wadau wote wa Muungano wa asasi za kiraia unaoshawishi maboresho ya Sheria ya Usalama Barabarani. Nawashukuru wote kwa kuweza kuitikia wito huu na kushiriki nasi katika kongamano hili lenye mada isemayo Kuelekea Malengo ya Usalama Barabarani ya 2030: Tulipofikia, Fursa na Changamoto zijazo, ASANTENI SANA.

Ndugu Washiriki

Kongamano la usalama barabarani ni siku muhimu sana ya kukumbushana kuhusu masuala mbalimbali ya usalama barabarani. Masuala hayo ni pamoja na kuwakumbusha madereva juu ya kuwa waangalifu na kuzingatia sheria, hususani alama na ishara mbalimbali wanapoendesha au kuegesha magari yao barabarani. Lakini pia ni siku muhimu kama nchi kuweza kutathimini juhudi mbalimbali zilizofanywa na serikali na wadau katika kukabiliana na ajali, kubaini changamoto zinazokwamisha kufikia malengo, na kutambua fursa mpya katika kukabiliana na ajali.

Ndugu Washiriki

Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni zinaonyesha kwamba zaidi ya watu 1,350,000 hufariki kwa ajali za barabarani duniani kote. Pia Ajali za barabarani zinatajwa kama sababu namba moja ya vifo kwa watoto wa umri kati ya miaka 5 hadi 14 pamoja na vijana wa umri kati ya miaka 15 hadi 29 ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

Ndugu Washiriki

Ajali bado zimeendelea kuwa tatizo sugu katika taifa letu. Kama takwimu zinavyoonesha bado idadi ya vifo na majeruhi ni kubwa licha ya juhudi zinazofanyika. Mimi mwenyewe mara kwa mara nimesikia na kushuhudia ajali mbalimbali sehemu mbalimbali nchini Tanzania. Ajali hizi zimekuwa zikiigharimu serikali kurekebisha miundombinu, kufanya maokozi, kupoteza nguvu kazi ya taifa, mada na vifaa tiba hospitalini. Wananchi pia wamekuwa wakipoteza wapendwa wao katika ajali na baadhi kusababishiwa ulemavu na majeraha ya kudumu. Na hii ndio sababu serikali kupitia Wizara yangu ipo katika mchakato wa kurekebisha Sheria ya Usalama Barabarani 1973, ili iweze kuendana na mahitaji ya sasa. Wizara yangu itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kwamba tunaboresha Sheria hii ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973.

Ndugu Washiriki

Sisi kama Serikali tunayo nia dhabiti ya kuhakikisha kwamba Ajali zinapungua kwa Asilia 50 ifikapo 2030 kama ambavyo tumeahidi katika mikataba ya kimataifa na kama matakwa ya sheria za kimataifa zinavyosema. Hivyo ninawaomba wadau waendelee kushirikiana na serikali kwa kutoa maoni ni kwa namna gani tunaweza kupunguza ajali kwa asilimia 50 ifikapo 2030.

Ndugu Washiriki

Pia ninatambua mjadala huu ulioandaliwa na Wadau wa Usalama barabarani na wenzetu wa Mwananchi communications ni mojawapo ya njia muafaka ya kuleta mawazo pamoja ya kujadiliana namna bora ya kupunguza ajali barabani.

Ndugu Washiriki

Natambua kuwa bado wapo madereva wanaendesha magari wakiwa wamelewa; wapo watembea kwa miguu wanavuka barabara wakiwa wamelewa; wapo madereva wanaendesha kwa mwendokasi hatarishi katika maeneo ya makazi ya watu au yasiyoruhusiwa na alama za barabarani, ikiwa ni pamoja na kuyapita magari mengine sehemu zisizoruhusiwa. Aidha, waendesha pikipiki, pamoja na abiria wao wamekuwa wakipuuzia kuvaa kofia ngumu (helmeti) kwaajili ya kujikinga na madhara yatokanayo na ajali za pikipiki. Mambo yote haya kwa pamoja ndiyo yanayotuletea majonzi kila siku. Hivyo nitumia fursa hii kuwaasa madereva kuendesha magari kwa uangalifu na kutii sheria zilizopo. Aidha, ninaliagiza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani.

Ndugu Washiriki

Ili kuweza kufikia lengo la kupunguza vifo na majeruhi wa ajali za barabarani, inampasa kila mmoja wetu kubadili tabia. Njia mojawapo ya kubadili tabia za watumiaji barabara ni elimu na adhabu. Kama elimu inatolewa lakini bado kukakuwa na ukaidi wa utii wa sheria za barabarani basi adhabu hutumika. Hata hivyo, kwa hali ilivyo sasa adhabu zilizopo kwenye sheria ya usalama barabarani yam waka 1973 hazina meno ya kutosha kuweza kubadilisha tabia ya watumiaji wa barabara wasiotaka kutii sheria. Hivyo, ipo haja ya kufanya mabadiliko ya sheria ili kuweza kuwa na adhabu zenye nguvu zaidi na zinazoendana na uzito wa kosa. Ni matarajio yetu kuwa mara sheria mpya itakapopitishwa na Bunge tutakuwa na sheria bora na yenye adhabu kali kwa wavunjifu wa sheria. Hivyo nawaomba wadau wote ikiwemo waheshimiwa Wabunge mara Sheria hiyo itakapoletwa Bungeni tuweze kuiunga mkono kwaajili ya kuipitisha.

Ndugu Washiriki

Nimeeleza mengi. Naomba niishie hapa. Lakini kabla sijahitimisha, napenda niwashukuru tena kwa kunialika kwenye shughuli hii. Nawaahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha usalama barabarani na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha maendeleo katika sekta ya usafiri.  Aidha tutasimamia na kutekeleza sheria ipasavyo kwa faida ya watumiaji wote wa barabara. Kila mmoja wetu hapa leo aondoke akiwa balozi mwema wa usalama barabarani ili tushuhudie kupungua au kuondoka kabisa kwa ajali zinazoepukika.

 

Mungu Ibariki Tanzania!

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”

Latest News and Stories

Search