News/Stories

WIKI YA KIMATAIFA YA USALAMA BARABARANI: MABORESHO YA SHERIA YA USALAMA BARABARANI NI MUHIMU ILI KUOKOA MAISHA YA WANANCHI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Wakati dunia ikiadhimisha wiki ya Umoja wa Mataifa ya Usalama Barabarani, viongozi wa ngazi mbalimbali nchini wametakiwa kuchukua hatua katika kudhibiti ajali za barabarani ili kuokoa maisha ya wananchi yanayopotea kila kukicha kwa kusababishwa na ajali za barabarani nchini.

Wiki ya Umoja Wa Mataifa ya Usalama Barabarani ilianzishwa kupitia Azimio la Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Oktoba 2005 ikiwa na lengo la kuboresha usalama wa barabarani duniani. Azimio hili liliitaka Tume ya Umoja wa Mataifa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuandaa kwa pamoja wiki hiyo. Kwa mara ya kwanza wiki ya umoja wa mataifa ya usalama barabarani iliazimishwa mwaka 2007 , ya pili mwaka 2013, ya tatu 2015, na ya nne 2017. Mwaka huu ni maadhirimisho ya tano, ambayo yanaadhimishwa kuanzia tarehe 6 mpaka tarehe 12 mwezi huu wa tano 2019.

 

Kauli mbiu ya wiki hii ni “Uongozi kwa usalama barabarani”. Kauli mbiu hii inaakisi nafasi ya viongozi katika kuleta mabadiliko kwenye eneo la usalama barabarani. Viongozi wako katika makundi mbalimbali mfano, jamii, wazazi, walezi, vyombo vya dini, jumuiya ya umoja wa mataifa, makampuni binafsi, bunge, mashirika yasiyo ya kiseriklai, serikali ya mtaa, serikali kuu . Wote hawa wana mchango mkubwa katika kuhakikisha usalama barabarani.

Lengo la wiki hii kwa mwaka 2019 ni kuhamasisha madai kwa ajili ya uongozi na maamuzi ya masuala ya usalama barabarani. Lengo pia ni kuwatia moyo viongozi ili wafanye maamuzi na kujumuisha wadau wa sekta mbalimbali zinazogusa masuala ya usalama barabarani. Uongozi thabiti ni muhimu sana ili kuweza kufikia malengo ya usalama wa barabara, ikiwa ni pamoja na lengo namba tatu la( Maendeleo Endelevu) ambalo ni kupunguza vifo vya barabarani na majeraha kwa asilimia 50 na lengo namba kumi na moja (11) linalolenga katika kuimarisha mifumo ya usafiri salama.

Mwamko wa viongozi wa ngazi mbalimbali katika jamii, ndiyo silaha itakayotumika katika kufanya maamuzi ya kisheria, kisera na kimkakati ili kuhakikisha kwamba Tanzania inapunguza au kumaliza kabisa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani pamoja na majeruhi. Tumeona viongozi wa serikali, vyama vya siasa, taasisi na mamlaka nyingine wakijitoa na kusimamia kidete masuala ya afya, elimu, miundombinu, rushwa, ubadhirifu, demokrasia na changamoto nyingine katika jamii. Hata hivyo kwenye suala la usalama barabarani bado kuna mwamko mdogo wa viongozi wa ngazi zote.

Tunachukua fursa hii kusisitiza kuwa suala la usalama barabarani ni suala la kiuchumi, kijamii na kiafya hivyo ni vyema likatiliwa mkazo ili kuzuia ajali na rasilimali inayotumika kuwatibu majeruhi na familia za waathirika zikatumila katika vipaumbele vingine kwa maendeleo ya nchi.

Asasi za kiraia zinazojihusisha na masuala ya usalama barabarani Tanzania kwa umoja wetu tumeona kuwa nafasi ya viongozi ni muhimu katika kuleta mabadiliko chanya hasa kwenye upande wa sera na sheria ya usalama barabarani. Na sisi kama mtandao wa taasisi za kiraia tumekua mstari wa mbele kutoa mchango wetu katika kuboresha sheria ya usalama barabarani.

Kadhalika tunaamini kuwa si viongozi wa kisiasa pekee wanaotakiwa kuchukua hatua katika suala la usalama barabarani bali ni pamoja na viongozi wa kuanzia ngazi ya kimataifa, kitaifa, mkoa, wilaya,kata, vijiji/mtaa jamii, familia pamoja na taasisi za kimataifa, asasi za kiraia, shule, vyuo, kampuni binafsi na kila mmoja wetu katika nafasi yake.

Suala la usalama barabarani licha ya kutopewa uzito mkubwa katika ngazi za juu za uongozi, bado ni eneo linalogharimu maisha ya watu, linasababisha ulemavuna hata kudidimiza uchumi. Kwa mfano kulingana na takwimu za shirika la afya duniani (WHO) za mwaka 2018 watu 1.35 milioni hufariki kila mwaka kutokana na ajali hizo. Pia ajali za barabarani hugharimu nchi husika karibu asilimia tatu ya pato la taifa na asilimia 93 ya ajali hizo hutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati ikiwemo Tanzania.

Hivyo basi tunatoa wito kuwa uongozi unahitajika katika kipindi hiki ambacho Tanzania inahitaji maboresho ya sheria ya usalama barabarani. Kwa sasa tunatumia sheria ya mwaka 1973 ambayo kimsingi bado ina mapungufu na hivyo kuleta changamoto katika usimamizi wa usalama barabarani. Mfano wa mapungufu hayo ni pamoja na suala zima la matumizi ya mikanda ambapo sheria ya sasa inasema dereva na abiria wa mbele tu ndio wanapaswa kufunga mkanda wawapo kwenye chombo cha moto lakini haisemi chochote juu ya abiria wanaokaa siti ya nyuma. Vilevile kwenye suala la matumizi ya kofia ngumu (Helmet) sheria inamtaka tu dereva wa chombo cha moto cha magurudumu mawili au matatu kuvaa kofia ngumu lakini iko kimya kwa abiria wa chombo hicho.

Vilevile kwa kupitia wiki hii tunaiomba serikali kulipa nguvu Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ili liweze kusimamia kikamilifu masuala ya usalama na kuweka mikakati ya muda mrefu ili kupunguza na ikiwezekana kumaliza kabisa ajali za barabarani. Tunaamini kuwa vifo hivi vitapungua endapo kutakuwa sera na sheria bora za usalama barabarani na katika hili mwamko wa viongozi unahitajika zaidi. Tunaendelea kuwaomba na kuwasihi viongozi hao watoe elimu na waendelee kutumia vyombo vya habari katika kufikisha ujumbe, maamuzi na matamko yao kuhusu sheria na masuala yote yahusuyo usalama barabarani.

Imetolewa na mtandao wa taasisi zisizo za serikali zinazotetea maboresho ya sheria ya usalama barabarani.

TAMWA

TAWLA

GHAI

TMF

SHIVYAWATA

SIKIKA

TLS

RSA

Latest News and Stories

Search